Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Njaa haipaswi kamwe kuruhusiwa kutokea Gaza asema mkuu wa OHCHR

Watu waliofurushwa makwao kutokana na mapigano huko Gaza wakisubiri mgao wa chakula kwenye kambi ya Al-Shaboura huko Rafah, kusini mwa Gaza
© WHO
Watu waliofurushwa makwao kutokana na mapigano huko Gaza wakisubiri mgao wa chakula kwenye kambi ya Al-Shaboura huko Rafah, kusini mwa Gaza

Njaa haipaswi kamwe kuruhusiwa kutokea Gaza asema mkuu wa OHCHR

Amani na Usalama

Wakati Baraza la Usalama linakutana tena leo mjini New York kwa ajili ya kupiga kura iliyocheleweshwa kwa muda mrefu kuhusu kusitisha mapigano ili kuruhusu misaada zaidi ya kibinadamu kuingia Gaza, mkuu wa haki za Umoja wa Mataifa Volker Türk ameongeza Sauti yake kwa wasiwasi mkubwa juu ya tishio la njaa linaloongezeka kote Ukanda wa Gaza.

Kupitia mtandao wa X, amesema "Njaa haipaswi asilani kuwa njia au matokeo ya vita," akijibu ripoti ya kutisha ya kuto kuwa na uhakika wa chakula iliyotolewa Alhamisi ambayo ilithibitisha maonyo ya mara kwa mara ya viwango vya njaa katika eneo lililozingirwa huku kukiwa na mapigano yanayoendelea.

Katika ujumbe wa kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X, Bwana Türk ameiitaka Israel kuchukua hatua mara moja ili kuhakikisha kwamba wale wote ambao hawajahusika katika mapigano kati ya Jeshi la Ulinzi la Israel na wapiganaji wa Hamas " kuwawezesha kupata mgao wa chakula cha kibinadamu kulingana na mahitaji".

Ripoti ya tathimini ya viwango vya chakula  (IPC) imeeleza kuwa njaa inaweza kutokea ndani ya miezi sita ijayo ikiwa hali ya sasa ya mgogoro mkubwa na vikwazo vya upatikanaji wa misaada vitaendelea.

Idadi ya watu wote wa Gaza takriban watu milioni 2.2 tayari wanaishi na shida au viwango vya juu vya uhaba wa chakula.

Ripoti ya IPC imesisitiza kuwa ingawa kizingiti cha njaa hakijavuka kiwango, wasaidizi wa kibinadamu wana wasiwasi hasa kuhusu utapiamlo miongoni mwa watoto, wanawake wajawazito na wanaonyonyesha na wazee.

Changamoto kwa wasichana vigori

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, limeonya kuwa zaidi ya wanawake 690,000 na wasichana vigori hawawezi kupata bidhaa za usafi wakati wa hedhi.

"UNRWA inasambaza taulo za kike, lakini kama kila kitu kingine tunachosambaza, ni kiwango kidogo ikilinganishwa na mahitaji ya wale wa Gaza," msemaji wa shirika hilo Tamara Alrifai amesema kupitia ukurasa wa X.

Wakati huo huo, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA, imeripoti mashambulizi makubwa ya Israel jana Alhamisi kutoka angani, nchi kavu na baharini katika sehemu kubwa ya Ukanda wa Gaza, pamoja na makombora ya Hamas yakishambulia Israel.

Kulingana na taarifa ya OCHA "Operesheni kali za ardhini na mapigano kati ya wanajeshi wa Israel na makundi yenye silaha za Palestina ziliendelea, katika maeneo mengi ya Gaza, isipokuwa Rafah. Urushaji wa maroketi na makundi yenye silaha ya Palestina kwenda nchini Israel uliendelea”.