Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi vijana dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kambini Tongogara, Zimbabwe

Wavulana wawili wakicheza kwenye maji ya mafuriko kufuatia kimbunga idai kupiga kambi ya wakimbizi ya Tongogara kusini mashariki mwa Zimbabwe. (Maktaba)
UNHCR/Zinyange Auntony
Wavulana wawili wakicheza kwenye maji ya mafuriko kufuatia kimbunga idai kupiga kambi ya wakimbizi ya Tongogara kusini mashariki mwa Zimbabwe. (Maktaba)

Wakimbizi vijana dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kambini Tongogara, Zimbabwe

Tabianchi na mazingira

Ikiwa leo Kongamano la Kimataifa la Wakimbizi ambalo hufanyika kila baada ya miaka minne linaanza huko Geneva, Uswisi na kuwaleta pamoja wadau mbalimbali wakiwemo wakimbizi kutafuta suluhu na kuahidi hatua kwa ajili ya wakimbizi duniani na nchi na jamii zinazowahifadhi, nikupeleke sasa nchini Zimbabwe ambako kuna mfano wa wazi namna wakimbizi wanavyoweza kuwa na mchango chanya katika jamii zinazowahifadhi.

Kundi la wakimbizi vijana katika Kambi ya Wakimbizi ya Tongogara nchini Zimbabwe wanaongoza juhudi za kurejesha mazingira yao katika hali nzuri wakiungwa mkono na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR.

Kambi ya wakimbizi ya Tongogara iliyoko kusini mwa Zimbabwe ni makazi ya wakimbizi 16,000, hasa kutoka Burundi, Msumbiji, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. 

“Miti ina faida nyingi, inavutia mvua, inatupatia kivuli, inakinga vumbi.”  

Faida alizozitaja Mugisha Everiste, mtoto huyu mkimbizi kutoka Burundi zisingepatikana kambini Tongogara kama si juhudi za vijana wakimbizi kupitia taasisi yao ya Refugee Coalition for Climate Action (RCCA). 

Elie Nsala Tshikuna, Mkimbizi kutoka DR Congo anaeleza akisema kwamba (Nats)…walianza kupanda miti mwaka 2020. Na kuanzia mwaka huo hadi sasa wamepanda miti zaidi ya 2,000 kambini. Hili limeleta mabadiliko makubwa kwa sababu wameona kwamba jukumu ambalo jamii sasa inalo la kulinda miti limekuwa bora zaidi.  

Jeanne Muhimundu, yeye ni mkimbizi kutoka Rwanda, mshiriki wa harakati hizi za utunzaji mazingira kambini, ana matumaini makubwa na hatua waliyoichukua,   

"Natumai kuona miti zaidi. Natumai kuona watu wanachukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.”