Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hospitali Gaza hazina uwezo tena, ni janga la kibinadamu: WHO

Mtu aliyejeruhiwa anakimbizwa kwenye mkeka na wafanyakazi wa matibabu na umati mkubwa wa watu, ikiwa ni pamoja na waandishi wa habari, nje ya Hospitali ya Al-Shifa huko Gaza.
© WHO Mtoto wa Kipalestina aliyejeruhiwa anakimbizwa katika hospitali ya Al Shifa huko Gaza. (Maktaba)

Hospitali Gaza hazina uwezo tena, ni janga la kibinadamu: WHO

Afya

Hospitali ya mwisho ambayo inafanya kazi kwa shida kaskazini mwa Gaza ni "eneo la maafa ya kibinadamu", limesema leo Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO likiangazia matokeo mabaya ya mashambulizi yanayoendelea ya Israel kwa wagonjwa mahututi na kujeruhiwa kwa raia kote katika eneo hilo.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kutokaa Gaza, Dkt Richard Peeperkorn, mwakilishi wa WHO katika eneo la Palestina linalokaliwa, ameelezea kuwa shoroba zilizofurika wagonjwa wa kiwewe katika hospitali ya Al-Ahli kwenye mji wa Gaza, ambapo madaktari huhudumia watu wakiwa sakafuni na mafuta, hewa ya oksijeni, chakula na maji ni haba. 

Katika siku 66 tu za mapigano, Ukanda huo umebadilishwa kutoka "mfumo wa afya unaofanya kazi ipasavyo, unaozalisha viashiria vya afya sawa na nchi jirani hadi hali ambapo zaidi ya theluthi mbili ya hospitali zake 36 na zaidi ya asilimia 70 ya huduma za afya ya msingi na vituo vya huduma kutofanyakazi”, amesema Dk. Peeperkorn.

Wakati huo huo msemaji wa WHO Christian Lindmeier amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi kwamba hospitali ya Kamal Adwan pia iliyoko kaskazini  mwa Gaza "wagonjwa wamekuwa wakihamishwa kwa nguvu leo  Jumanne asubuhi, kulingana na mamlaka ya afya ya Gaza. Takriban wagonjwa 68 wakiwemo 18 walio katika uangalizi mkubwa na watoto wachanga sita wanaripotiwa kuwa kwenye hospital hiyo, pamoja na maelfu ya watu waliokimbia makazi yao na kutafuta usalama hopitalini hapo.”

Hospitali hiyo imezingirwa na wanajeshi na vifaru vya Israel kwa siku kadhaa, huku mapigano ya silaha yakiripotiwa karibu, na eneo hilo imesema ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu OCHA. 

Jana Jumatatu, idara ya uzazi ya hospitali hiyo iliripotiwa kushambuliwa kwa risasi na akina mama wawili waliuawa.

Madaktari bingwa wa upasuaji waliovaa vitambaa vya bluu wakimfanyia upasuaji mgonjwa katika chumba cha upasuaji katika hospitali ya Al-Quds huko Gaza.
© WHO Mgonjwa akipatiwa huduma katika chumba cha upasuaji kwenye hospitali ya Al-Quds Gaza

Changamoto kubwa katika huduma za afya

Huku kukiwa na mahitaji makubwa ya kibinadamu katika eneo la kaskazini lililoharibiwa la Gaza, Hospitali ya Al-Ahli ina upungufu wa wahudumu amesema Dkt. Peeperkorn , hospital hiyo ikiwa na wagonjwa zaidi ya 200 lakini ni rasilimali zilizopo ni za kutosha kusaidia wagonjwa 40 pekee. 

Ameongeza kuwa “Kwa kuwa madaktari hawawezi kufanya upasuaji wa mishipa, inawabidi kuwakata wagonjwa viungo kama suluhu ya mwisho kuokoa maisha".

Jumamosi iliyopita msafara wa Umoja wa Mataifa na Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina (PRCS) ulioongozwa na WHO ulikumbana na "Purukshani kubwa wakati wa kupeleka vifaa vya wagonjwa wa kiwewe na vya upasuaji kwa wagonjwa 1,500 hospitalini na kuhamishwa kwa wagonjwa 19 mahututi na wafanyakazi wenzao hadi katika kituo cha tiba cha Nasser Medical Complex kilichopo kusini mwa Gaza”, kwa mujibu wa WHO.

Kuzuiliwa kwa mtutu wa bunduki

Dkt. Peeperkorn ameelezea vikwazo vingi vilivyokabili ujumbe huo, ikiwa ni pamoja na ukaguzi njiani katika kizuizi cha kijeshi cha Israeli huko Wadi Gaza kaskazini, ambapo wafanyakazi wawili wa PRCS walizuiliwa kwa zaidi ya saa moja. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na shirika la WHO leo Jumanne, "wafanyakazi wa WHO walishuhudia mmoja wao akipigwa magoti kwa mtutu wa bunduki na kisha kuondolewa asionekane, ambapo inasemekana alinyanyaswa, kupigwa, kuvuliwa nguo na kupekuliwa".

Mganga wa WHO amesisitiza kuwa "hakuna mtu anayeweza kuzuiliwa akiwa sehemu ya operesheni ya matibabu" na kusisitiza ukweli kwamba msafara muhimu kama hiyo ya kibinadamu "haiwezi kumudu ucheleweshaji wowote".

Dkt. Peeperkorn amesema kwamba walipofika eneo la kaskazini mwa Gaza, ambalo sasa "inaonekana kama jangwa, wahudumu waliona watu wengi mitaani wakishangaa kuona msafara huo, kwani kumekuwa na msaada mdogo sana kaskazini mwa eneo hilo kwa miezi sasa.”

Ucheleweshaji misaada wa hatari

Baada ya kuingia katika mji wa Gaza lori la msaada likiwa na vifaa vya matibabu na moja ya magari ya kubeba wagonjwa ambayo yalikuwa sehemu ya msafara huo yalipigwa risasi, wakati wa kurudi kuelekea kusini mwa Gaza na wagonjwa kutoka Hospitali ya Al-Ahli wakiwa ndani limesema shirika la WHO. 

"Msafara huo ulisimamishwa tena katika kituo hicho cha ukaguzi, ambapo wafanyikazi wa PRCS na wagonjwa wengi walilazimika kushuka kwenye gari la kubeba wagonkwa kwa ajili ya ukaguzi wa usalama".

Wagonjwa mahtuti waliosalia kwenye gali la wagonjwa walipekuliwa na askari wenye silaha, na mmoja wa wafanyikazi wawili wa PRCS waliozuiliwa kwa muda mapema wakati wa kuingia alichukuliwa kwa mahojiano kwa mara ya pili. Ucheleweshaji mkubwa ulitokea na "PRCS iliripoti baadaye kwamba wakati wa mchakato wa uhamisho, mmoja wa wagonjwa waliojeruhiwa alikufa, kutokana na majeraha yake ambayo hayajatibiwa", WHO imesema.

Baada ya kuachiliwa baadaye usiku huo na "baada ya juhudi za pamoja za Umoja wa Mataifa mfanyakazi wa PRCS alisema kwamba alikuwa amepigwa na kudhalilishwa, kisha akaondoka kuelekea kusini na mikono yake bado imefungwa nyuma yake, na bila nguo au viatu".

Mwanamume akikagua vifaa vya matibabu vya Shirika la Afya Duniani katika ghala moja huko Gaza.
© WHO Vifaa vya matibabu katika ghala la WHO huko Gaza vinatayarishwa kwa ajili ya kutolewa. (Maktaba)

Mfumo wa afya lazima ulindwe

Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus ameelezea kwenye ukurasa wake wa jukwaa la kijamii la X leo wasiwasi wake kuhusu "ukaguzi wa muda mrefu na kuwekwa kizuizini kwa wafanyikazi wa huduma za afya hali ambayo huweka maisha ya wagonjwa ambao tayari ni dhaifu hatarini zaidi".

Ameongeza kuwa "Watu wa Gaza wana haki ya kupata huduma za afya. Mfumo wa afya lazima ulindwe hata katika vita."

Magonjwa yanaongezeka

Idadi ya watu waliokimbia makazi yao katika Ukanda huo, ambapo takriban watu milioni 1.9, ikiwa ni idadi kubwa ya wakazi wa Gaza, wamelazimika kukimbia makazi yao, na hali katika makazi walikokimbilia yenye msongamano mkubwa wa watu ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vyoo bora, imesababisha ongezeko kubwa la magonjwa amesema Dkt. Peeperkorn. 

Tayari kulikuwa na visa 60,000 vya kuhara kwa watoto wa chini ya umri wa miaka mitano na zaidi ya visa 160,000 vya maambukizo ya magonjwa ya kupumua. Upele, upele wa ngozi, tetekuwanga na hata uti wa mgongo vinaongezeka, sambamba na majeraha makubwa na majeraha ya uti wa mgongo.

Wakati huo huo wahudumu wa afya wanakosa vifaa muhimu na "wanaghubikwa kabisa na hofu ya usalama wa familia zao".

Afisa huyo wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa ni muhimu kufanya mfumo wa afya ya msingi kufanya kazi tena na kurudisha afya ya mama na mtoto, huduma ya uzazi, matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza, kama saratani na usaidizi wa afya ya akili miongoni mwa mengine.

Vitanda zaidi vinahitajika hospitali Rafah

Upande wa Kusini mwa Gaza, ambako Dkt. Peeperkorn amekuita "Uti wa mgongo wa mfumo wa afya wa Gaza”, jana Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Palestina ilianza maandalizi ya kuanzisha hospitali ya mashinani kwa ushirikiano na Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Qatar, katika mkoa wa Rafah. 

WHO imesema hospitali hiyo ina vitanda 50 vikiwemo chumba cha upasuaji, chumba cha wagonjwa mahututi, mapokezi na kituo cha radiolojia.

WHO imesisitiza umuhimu wa kuongeza uwezo wa hospitali katika eneo hilo ikiwemo vitanda vya wagonjwa. 

Kwa mujibu wa mamlaka ya afya ya Gaza ni asilimia moja tu ya Wapalestina waliojeruhiwa katika mapigano, au takriban watu 400, hadi sasa wamehamishwa nje ya Gaza kwa ajili ya kulazwa hospitalini kupitia kivuko cha mpaka cha Rafah.

Takriban watu 50,000 wamejeruhiwa huko Gaza tangu Oktoba 7 na 8,000 kati yao wanahitaji "uingiliaji wa haraka wa matibabu", limesema shirika la WHO