UNICEF yafafanua ni kwa vipi mabadiliko ya tabianchi yanabebesha watoto mzigo wa magonjwa na ujinga.
UNICEF yafafanua ni kwa vipi mabadiliko ya tabianchi yanabebesha watoto mzigo wa magonjwa na ujinga.
Mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi hauathiri sayari dunia pekee bali pia unawabadilisha kabisa watoto. Watoto wanalazimika kubeba mzigo mkubwa wa magonjwa ya moyo, yale yanayosababishwa na matumizi ya maji machafu, yale yasababishwayo na kuvuta hewa chafu, pamoja na madhara ya kiakili na kihisia.
Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya watoto UNICEF linasema madhara sio kwenye afya pekee bali pia yanaonekana katika ustawi wa watoto, kwani ukuaji wa miili yao na akili zao pia unatatizika na hili ni jambo bayo zaidi kwani madhara yake yanaendelea katika maisha yao yote.
Mbali na athari za kiafya watoto pia wanaathirika kielimu, na hili limethibitishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa mfuko wa kimatifa wa elimu haiwezi kusubiri ECW Yasmine Sherif anayeshiriki mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi COP28 huko Dubai, katika Falme za kiarabu. "Tumetoa takwimu mpya hivi karibuni, watoto na vijana milioni 62 elimu yao imetatizika na haya ni matokeo ya moja kwa moja ya mabadiliko ya tabianchi. Nitakupa mfano mmoja tu. Kwa mfano, shule 29,000 ambazo ziliharibiwa na mafuriko nchini Pakistani, mabadiliko ya tabianchi ambayo tunayaona kupitia ukame nchini Somalia, huko Pembe ya Afrika, matetemeko ya ardhi nchini Afghanistan, na kadhalika.”
Akijikita na upande wa elimu Bi. Sherif amesema anachotaka kutoka kwa viongozi wa dunia, “Ni kufungua macho na kuelewa uhusiano uliopo kati ya mabadiliko ya tabianchi na kuvurugika kwa elimu, ambao nao unahusiana na kizazi kipya, kwanza kabisa, kisicho na elimu na, pili, hakina ufahamu wa mabadiliko ya tabianchi na kwa hakika hakiwezi kuchukua nafasi ya kufanya mabadilika, kupunguza, au kuzuia mabadiliko ya tabianchi.”
Mkuu huyo wa Mfuko wa Elimu haiwezi Kusubiri ametoa matumaini, “Hata hivyo, ikiwa tutawekeza sehemu ndogo tu ya kile tunachowekeza katika mabadiliko ya tabianchi kama sekta, katika elimu kwa watoto walio katika mizozoz na ukimbizini, tunaweza kuhakikisha kuwa kizazi kipya kinaweza kuendelea na shule na pia kuwa waleta mabadiliko, watakuwa wahandisi, wanasayansi, walimu ambao siku moja wanaweza kuendelea katika njia ya kuokoa Mama Dunia, kutokana na mabadiliko ya tabianchi.”
Na iwapo uwekezaji katika elimu hautafanyika ameeleza nini madhara yake “Ikiwa hatutawekeza katika elimu, kwa madhumuni ya kuzuia, madhumuni ya urekebishaji, na kwa siku zijazo kupunguza, nadhani, mabilioni yote ambayo tunaweka katika mabadiliko ya tabianchi ni fedha zilizopotea.”