Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asante FAO kunijengea mnepo sasa najikimu mimi na familia yangu: Lilly Kiden

Lilly Kiden akibeba mazao ya mbogamboga kutoka kwa shamba lake.
FAO
Lilly Kiden akibeba mazao ya mbogamboga kutoka kwa shamba lake.

Asante FAO kunijengea mnepo sasa najikimu mimi na familia yangu: Lilly Kiden

Tabianchi na mazingira

Wakati mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi COP28 ukijiandaa kufunga pazia hapo kesho nakupeleka Sudan Kusini jimbo la Equatorial Mashariki ambako wakulima walioathirika na mabadiliko ya tabianchi sasa wanajengewa mnepo na mradi wa shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO na wengi wameweza kujikwamua pamoja na familia zao. Ungana na Flora Nducha akikuletea safari ya mafanikio ya mmoja wa wanuafa wa mradi huo wa FAO. 

Kutana na Lilly Kiden mama mjasiriamali anayelima na kuchuza mboga za majani  katika eneo la Lopit Sudan Kusini

Bi. Kiden anasema ana watoto 7 na jamaa wengine 10 wa familia ambao wote wanamtegemea . Shukran kwa FAO  kwa kuwajengea wanawake mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kupitia ufadhili kutoka Benki ya Maendeleo Afrika sasa wana mabwa yanayotumia pampu za sola na kumuwesha Lilly na wanawake wengine wakulima wadogo kumwagilia mashamba yao.  

Lilly Kiden na wakulima wenzake wanawake wakikagua mradi wa umwagiliaji, sehemu ya msaada kwa wakulima wadogo unaotekelezwa na FAO IN Sudan Kusini.
FAO
Lilly Kiden na wakulima wenzake wanawake wakikagua mradi wa umwagiliaji, sehemu ya msaada kwa wakulima wadogo unaotekelezwa na FAO IN Sudan Kusini.

Kwa Lilly anasema kibarua ni kigumu kueedesha familia kubwa kama aliyonayo bila msaada mwingine.

Ingawa sasa amekuwa mchumia juani anayelia kivulini, ukame wa muda mrefu Sudan umekuwa mwiba kwa wakulima hawa,  

“Mabadiliko ya tabianchi yametuathiri sana, na mwaka huu umekuwa mbayá zaidi, kila tulichopanda kilikauka na jua hali ikiendelea hivi wanangu hawatakuwa na chakula na wengine watashindwa kwenda shule.”

Lilly mwenye umri wa miaka 38 kutokana na kuuza mbogamboga yeye na wenzake 25 wamewekeza fedha wanazopata na sasa wanapena mikopo kupitia jumuiya yao ya akiba ya kijiji. Ama kwa hakika jembe halimtupi mkulima,  

”Hela ninayopata kwa kuuza mbogamboga imenisaidia sana naweza kununua chakula kwa ajili ya familia yangu, na kuweka akiba kidogo ambayo imekuwa mkombozi wangu yote ni kwa kulima na kuuza mbogamboga. Ndoto yangu ni kuongeza bidii ili watoto wangu waendelee na masomo.”

FAO mbali ya kuwajengea mabwawa kwa ya umwagiliaji wakulima hawa pia inawapa mafunzo, mbegu na mikopo.