Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres aonya juu ya athari za hali ya Gaza kwa amani na usalama wa kikanda

Katibu Mkuu UN António Guterres akitoa hotuba jukwaani wakati wa sherehe ya ufunguzi wa Jukwaa la Doha 2023 nchini Qatar.
UN/Florencia Soto Nino-Martinez Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia wakati wa sherehe za ufunguzi wa Jukwaa la Doha 2023 nchini Qatar

Guterres aonya juu ya athari za hali ya Gaza kwa amani na usalama wa kikanda

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ameonya kwamba "tunakabiliwa na hatari kubwa inayowakilishwa na kuporomoka kwa mfumo wa kibinadamu huko Ukanda wa Gaza.”

Guterres ametoa onyo hilo wakati wa hotuba yake aliyoitoa kwenye jukwaa linalofanyika Doha leo Jumapili kwamba hali inayoshuhudiwaa ni kuzorota kwa kasi kuelekea zahma kubwa, na matokeo ya athari zake ni kwamba kunaweza kuwa hakuna njia ya kutokomeza hali hiyo au kubadili mwelekeo wake kwa Wapalestina na  kwa amani na usalama katika ukanda huo.

Guterres amesema kuwa mashambulizi ya kutisha yaliyoanzishwa na Hamas tarehe 7 Oktoba, na mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel dhidi ya Gaza, yalipokelewa kwa ukimya mkubwa na Baraza la Usalama, na kubainisha kuwa Baraza hilo lilitoa azimio kuhusu hali hiyo zaidi ya mwezi mmoja baadaye.

Ingawa alikaribisha uamuzi huo, amesema kuwa ucheleweshaji huu unakuja na gharama, na akaonya kuwa mamlaka na uaminifu wa Baraza hilo umepunguzwa sana, akionyesha kuwa uamuzi huo haujatekelezwa.

Mfanyakazi wa misaada WFP akikabidhi kifurushi cha chakula kwa mwanamke na mtoto walioketi kwenye mkokoteni wa punda huko Gaza.
© WFP/Ali Jadallah Wanawake huko Gaza wakisafirisha vifurushi vya chakula vinavyosambazwa na WFP. (Maktaba)

Idadi kubwa ya watu wamekufa Gaza

Jumatano iliyopita, Guterres alituma barua kwa Rais wa Baraza la Usalama ambapo alitumia kifungu cha 99 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa kwa mara ya kwanza tangu awe Katibu Mkuu mwaka 2017.

Katibu Mkuu alisema katika hotuba yake aliandika kwamba hakuna ulinzi madhubuti kwa raia na kuongeza kuwa "Kwa kweli, katika kipindi changu cha uongozi idadi ya vifo na majeruhi kwa raia huko Gaza katika kipindi kifupi kama hicho haijawahi kutokea."

Katibu Mkuu ameeleza kuwa mfumo wa huduma za afya unaporomoka na anatarajia utaratibu wa umma kuporomoka kabisa hivi karibuni, "na hali mbaya zaidi inaweza kutokea, ikiwa ni pamoja na magonjwa ya milipuko na shinikizo la kuongezeka kwa watu wengi wanaoingia Misri."

Guterres amesema alilitaka Baraza la Usalama kuweka shinikizo ili kuepusha janga la kibinadamu, na amesisitiza upya wito wake wa kutangaza kusitisha mapigano kwa misingi ya kibinadamu.

Pia ameelezea masikitiko yake kwamba Baraza la Usalama limeshindwa kufanya hivyo, lakini ameahidi kutokata tamaa.

Alimshukuru kiongozi na serikali ya Qatar kwa jukumu la upatanishi iliyocheza, haswa katika kukubaliana juu ya usitishaji uhasama kwa minajili ya kibinadamu, kuongeza misaada ya kibinadamu, na kuwaachilia mateka.

Kamishna Mkuu wa UNRWA, Philippe Lazzarini, akizungumza kwenye jukwaa wakati wa mkutano wa waandishi wa habari kuhusu ufadhili wa UNRWA.
UN Photo/Evan Schneider Kamishina Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina Philippe Lazzarini

Usawa na mshikamano ni muhimu

"Tunahitaji juhudi za dhati kuleta miundombinu ya kimataifa katika hali ya kisasa, iliyokita mizizi katika usawa na mshikamano na kwa kuzingatia Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa", amesema, akibainisha kuwa mgawanyiko wa Baraza "unadhoofisha suluhu kuanzia Ukraine hadi Myanmar na Mashariki ya Kati.”

Akihutubia pia mkutano huo nchini Qatar, mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA Philippe Lazzarini.

 amesema “udhalilishaji wa Wapalestina umeruhusu jumuiya ya kimataifa kuvumilia mashambulizi ya Israel yanayoendelea Gaza, ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 17,000 tangu tarehe 7 Oktoba.”

Ameongeza kuwa "Hakuna shaka kwamba usitishaji mapigano wa kibinadamu unahitajika ikiwa tunataka kukomesha hali ya jehanamu kwa dunia hivi sasa huko Gaza." 

Utawala dhaifu wa kimataifa

Pamoja na nguvu nyingine za kugawanyika kupata msingi, Bwana Guterres amesema sasa ni wakati wa kujenga madaraja na kutafuta suluhisho kwa pamoja ya changamoto za kimataifa.

Zaidi ya Baraza la Usalama, Bwana Guterres amesema utawala wa kimataifa unashindwa kudhibiti vitisho viwili vilivyopo.

Mosi: juu ya janga la mabadiliko ya tabianchi, akisema matarajio zaidi yanahitajika ili kupunguza uzalishaji wa gesi chafu na kuhakikisha haki ya tabianchi.

Waandamanaji wana mabango mekundu yenye kaulimbiu kama 'FAIR FUNDED FEMINIST FULL FOREVER FAIR' katika mkutano wa COP28 katika Jiji la Expo Dubai.
© COP28/Mahmoud Khaled Mtazamo wa jumla wa hatua ya "Usiwashe Moto: Matumizi ya Mafuta ya Kisukuku itokomezwe" na Mtandao wa Hatua za Hali ya Hewa Ulaya katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP28 huko Dubai, Falme za Kiarabu.

Guterres ameongeza kuwa "Licha ya ahadi na ahadi, mabadiliko ya tabianchi yamefikia pabaya. Uzalishaji wa hewa chaguzi upo katika kiwango cha juu sana. Na nishati ya kisukuku ndiyo sababu kuu,” na kuongeza kuwa “Nishati mbadala ni nafuu, safi, na haina kikomo, na inaweza kukidhi mahitaji ya nishati yanayoongezeka ulimwenguni bila kutia sumu mazingira na kudumaza sayari yetu.”

Amezitaka kampuni za mafuta na wasaidizi wao kutumia rasilimali zao kubwa kuongoza mapinduzi mapya. 

Na vivyo hivyo amewataka viongozi katika COP28 huko Dubai kukubaliana juu ya kupunguzwa kwa kasi kwa uzalishaji wa hewa ukaa, kulingana na kikomo cha kusalia na nyuzi joto 1.5C.

"Hii ndiyo njia pekee sio tu kwa uendelevu wa kudhibiti mabadiliko ya tabianchi, lakini uendelevu wa kiuchumi," Katibu Mkuu amesema.

Benki za maendeleo za kimataifa lazima zibadilishe mtindo wao wa biashara na kutumia fedha za binafsi zaidi kwa gharama inayofaa kwa nchi zinazoendelea kuwekeza katika hatua za hali ya hewa na Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Pili: ameangazia tishio linaloletwa na teknolojia mpya, akisema akili mnemba au AI inayozalishwa inaweza kutoa suluhisho kwa changamoto nyingi za ulimwengu, lakini bila udhibiti wa kutosha, pia itatupeleka kwenye maji ya kina kirefu na yenye shida."

Bwana Guterres aliendelea, kusema kwamba "Teknolojia hizi zinalia kwa ajili ya utawala," akilaumu kwamba AI tayari inazidisha kauli za chuki na migawanyiko, kuwezesha uvunaji wa takwimu na ufuatiliaji wa watu wengi, na kuzidisha ukosefu mkubwa wa usawa.

Ili kusaidia kuendeleza utafutaji wa suluhu, ameteua Bodi ya Ushauri ya Ngazi ya Juu ya Wadau mbalimbali kuhusu AI ambayo itatoa mapendekezo ya awali mwishoni mwa mwaka huu. Ilikutana mjini New York wiki iliyopita.