Afrika inakabiliwa na janga kubwa chakula ambalo halijawahi kushuhudiwa
Afrika inakabiliwa na janga kubwa chakula ambalo halijawahi kushuhudiwa
Takriban watu milioni 282 barani Afrika (karibu asilimia 20 ya idadi ya watu) hawana lishe bora, ongezeko la watu milioni 57 tangu janga la COVID-19 lianze. Zaidi ya watu bilioni moja hawawezi kumudu lishe bora. Takriban asilimia 30 ya watoto wamedumaa kwa sababu ya utapiamlo.
Haya yote yamo kwenye ripoti iliyozinduliwa leo huko Johannesburg, Afrika Kusini na mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa lile la chakula na kilimo FAO, la mpango wa chakula duniani WFP, Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) na Kamisheni ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Afrika (ECA).
Ripoti hiyo ya uhakika wa chakula na lishe kanda ya Afrika 2023 imeangazia takwimu za kutisha za ukosefu wa chakula na utapiamlo ambazo zinasisitiza haja ya haraka ya hatua za kina kuchukuliwa ili kuepusha zahma kubwa.
Afrika bado inaendelea kuwa nje ya mkondo wa kufikia malengo ya uhakika wa chakula na lishe ya Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs ifikapo mwaka 2030, na shabaha za Malabo za kumaliza njaa na aina zote za utapiamlo ifikapo mwaka 2025.
Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa FAO na Mwakilishi wa Kanda ya Afrika Abebe Haile-Gabriel aakizungumza katika utangulizi wa ripoti hiyo amesema “Kuzorota kwa hali ya uhakika wa chakula na kukosekana kwa maendeleo kuelekea malengo ya lishe ya kimataifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani - WHO kunafanya kuwa muhimu kwa nchi kuongeza juhudi zao ili kufikia ulimwengu usio na njaa na utapiamlo ifikapo 2030.”
Ripoti hiyo imezinduliwa leo katika mkutano wa FAO wa Kamisheni ya Kilimo ya Afrika ya Takwimu za Kilimo (AFCAS).na umekuja wakati huu mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabia nchi COP28 ukiendelea huko Dubai, Falme za Kiarabu ukiangazia changamoto za hali ya hewa na uhaba wa chakula barani Afrika.
Utapiamlo katika aina zake zote unaikumba Afrika
Ripoti hiyo iligundua kuwa kiwango cha udumavu miongoni mwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kilikuwa asilimia 30 mwaka wa 2022, ambacho bado kiko juu licha ya kuimarika kwa kiasi kikubwa katika miongo miwili iliyopita. Kiwango cha maambukizi ya upotevu kwa watoto katika eneo hilo kilisalia chini kidogo ya makadirio ya kimataifa ya asilimia 6.8 mwaka 2022 na kilikuwa kikubwa katika kanda zote isipokuwa Kusini mwa Afrika.
Kuenea kwa upungufu wa damu miongoni mwa wanawake watu wazima bado tatizo kubwa barani Afrika, kiwango kikiwa juu ya makadirio ya kimataifa, na hasa katika nchi za Afrika Magharibi na Afrika ya Kati.
Ripoti hiyo pia ina habari njema, ikisema kuwa kiwango cha unyonyeshaji maziwa ya mama pekee barani Afrika ni kikubwa katika Afrika Mashariki, huku kukiwa na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Afrika ya Kati na Afrika Magharibi tangu mwaka 2012.
Waafrika wengi hawawezi kumudu lishe yenye afya
Idadi kubwa ya watu barani Afrika - karibu asilimia 78, au zaidi ya watu bilioni moja - bado hawawezi kumudu lishe bora, ikilinganishwa na asilimia 42 katika kiwango cha kimataifa, na idadi inaongezeka.
Gharama ya wastani ya lishe bora imekuwa ikiongezeka kila baada ya muda, na ilikuwa dola 3.57 kwa kila mtu kwa siku mwaka wa 2021 barani Afrika, kiwango hicho cha fedha ni cha juu zaidi kuliko kiwango cha umaskini uliokithiri cha dola 2.15 kwa kila mtu kwa siku. Hii ina maana kwamba siyo tu maskini bali pia idadi kubwa ya watu wanaokadiriwa kutokuwa maskini hawawezi kumudu mlo wenye afya barani Afrika.
Afrika Magharibi na Afrika Mashariki zilikuwa na ongezeko kubwa zaidi la gharama ya lishe bora kati ya mwaka 2019 na 2021.
Mashirika hayo yamehimiza kuwa matokeo ya ripoti hiyo yatachochea kasi mpya ya mabadiliko ya mifumo ya kilimo barani Afrika, na kuunda mifumo bora zaidi ya chakula cha kilimo kwa watu na sayari nzima.
Kuisoma ripoti yote bofya hapa