Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sasa hatuchomi tena viatu vya watoto kuangazia nyumba, tunatumia sola - Loveness

Kijana wa Kimasai aliyevaa fulana ya chungwa akiangalia taa ya jua huko Arusha, Tanzania.
COP28 Loveness Sabaya wa jamii ya kimasai kutoka Arusha nchini Tanzania akiuza taa za nishatii ya jua.

Sasa hatuchomi tena viatu vya watoto kuangazia nyumba, tunatumia sola - Loveness

Tabianchi na mazingira

Loveness Sabaya mwanaharakati wa mazingira kutoka Arusha ni kiashiria cha jinsi hatua kwa tabianchi zinapofikishwa mashinani zinaleta manufaa ya kimkakati kwa kaya na jamii nzima kwa ujumla.

Tweet URL

Kupitia mafunzo kutoka shirika la kiraia la Solar Sister linalojengea uwezo wanawake barani Afrika kutumia nishati salama, Loveness ameweza kufundisha jamii yake kutumia taa za nishati ya jua au sola na hivyo kuondokana na matumizi ya kibatari au kutia moto vitu kama viatu vya watoto ili kuangazia nyumba wakati wa usiku.

Tulichoma viatu vya watoto wetu kuangazia mwanga nyumbani

Kupitia video iliyochapishwa kwenye ukurasa wa X wa mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, UNFCCC, au COP28 unaoendelea huko Dubai, Falme za Kiarabu, Loveness anasema, “siishi yale maisha ambayo tulikuwa tunaishi. Nyumba zetu zilikuwa zinaungua kila wakati kutokana na matumizi ya koroboi.”

Koroboi ni taa iliyotengenezwa kwa kopo na kujazwa mafuta ya taa na utambi.

Loveness anasema iwapo kuna siku hana mafuta ya taa, “unapata mgeni, unachukua kiatu cha mtoto, na kesho yake mtoto anakuwa hana kiatu cha kutembelea.”

Solar Sister ikamkomboa Loveness

Hali hii ilimfanya Loveness ajiunge na Solar Sister ambapo alipata mafunzo ya kutengeneza taa za sola na kusambazia sola majumbani.

“Kilichonifanya mimi nianze katika ujasirimali, nilitaka watoto wangu baadaye waishi maisha mazuri, niwapatie elimu na baadaye waendelee mbele zaidi,” anasema Loveness kuhusu lengo la kujiunga na Solar Sister.

Baada ya kujiunga na kuanza kusambaza taa za sola majumbani, Loveness na wenzake walisaidia kuepusha madhara ya moto majumbani kwani jamii zilianza kutumia sola.

Sasa ameweza kupeleka watoto shule, na kusaidia familia yangu

“Kwanza malazi nimeyapata, na watoto wangu wako shuleni na naendeleana biashara ya sola. Halikadhalika familia inayonizunguka kama faida yangu kama mama yangu na bibi yangu wakihitaji msaada, natapa kitu cha kuwapatia kupitia faida ninayoipata kwenye biashara ya sola,” anasema Loveness.

Loveness anasema kwa sasa mtazamo wake ni wa chanya, “kwa sababu nimesonga kimaisha, kiuchumi na hata kiakili maana unajua ukipata elimu ni sawa sawa umechanganua na akili.”