Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COP28: Viwango vya joto vikiongezeka, zaidi ya nchi 60 zaahidi kupunguza utoaji wa hewa chafuzi

Wanaharakati katika mkutano wa COP28 waandamana kupinga kuendelea kufadhiliwa kwa nishati ya mafuta ya kisukuku.
© COP28/Christopher Edralin
Wanaharakati katika mkutano wa COP28 waandamana kupinga kuendelea kufadhiliwa kwa nishati ya mafuta ya kisukuku.

COP28: Viwango vya joto vikiongezeka, zaidi ya nchi 60 zaahidi kupunguza utoaji wa hewa chafuzi

Tabianchi na mazingira

Viwango vya joto vinavyozidi kuongezeka kila uchao na mahitaji ya viyoyozi na vifaa vingine vya kuleta ubaridi yakiongezeka, ripoti mpya iliyotolewa hii leo kwenye mkutano wa COP28 huko Dubai, Umoja wa Falme za kiarabu inalenga kupunguza utoaji wa hewa chafuzi kwenye sekta ya vifaa vya kupoza joto duniani kote. 

Zaidi ya nchi 60 zimetia saini kile kiitwacho “ahadi ya kupoza joto,’ kwenye mkutano huo wa 28 wa nchi wanachama wa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi, UNFCCC

Mpango huo unaweza kutoa fursa ya kila mtu duniani kupata mfumo wa kupoza joto, na hivyo kuondoa shinikizo kwenye gridi za umeme za kitaifa na hatimaye kuokoa matrilioni yad ola ifikapo mwaka 2050. 

Mifumo ya kupoeza ni mchangiaji mkubwa wa mabadiliko ya hali ya hewa.
© Unsplash/Sergei A
Mifumo ya kupoeza ni mchangiaji mkubwa wa mabadiliko ya hali ya hewa.

Gharama ya kupoza joto 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira duniani, UNEP linakadiria kuwa zaidi ya watu bilioni 1 wako hatarini kukumbwa na viwango vya joto kupindukia kutokana na ukosefu wa mifumo ya kupoza joto, wengi wao wakiwa barani Asia na Afrika. 

Halikadhalika, kwa zaidi ya siku 20 kila mwaka, takribani theluthi moja ya idadi ya watu wote duniani wanakumbwa na mikondo joto hatari inayoweza kusababisha vifo. 

Sasa mpango huo uliotiwa saini unaweza kuleta unafuu kwa binadamu na pia katika sekta nyingine muhiu kama vile uhakika wa kupata chakula duniani na usambazaji wa chanjo kwa njia ya uwekaji kwenye majokofu. 

Lakini wakati huo huo, mbinu za kawaida za kupoza joto kupitia viyoyozi, ni kichocheo kikubwa cha mabadiliko ya tabianchi, ikihusika na asilimia zaidi ya 7 ya hewa chafuzi inayotolew duniani. 

UNEP inasema iwapo mbinu hiyo haitadhibitiwa, basi mahitaji ya nishati kwa ajili ya kupoza joto yataongezeka mara tatu ifikapo mwaka 2050. 

“Kwa ufupi, kadri tunavyojaribu kupoza joto, ndivyo joto linazidi kuongezeka kwenye sayari dunia. Iwapo kiwango cha sasa cha ongezeko kitaendelea, vifaa vya kupoza joto vitasababisha asilimia 20 ya matumizi ya umeme kwa siku – na inatarajiwa kuongezeka maradufu ifikapo mwaka 2050. 

Watumiaji wakubwa wa umeme 

Mifumo ya sasa ya kupoza joto, kama vile viyoyozi na majokofu, vinatumia kiwango kikubwa cha umeme na mara nyingi hutumia vifaa vinavyoongeza joto duniani. 

Ripoti hii mpya ya UNEP, inaonesha kuwa kwa kuchukua hatua za kupunguza matumizi ya umeme kwenye vifaa vya kupoza joto, kunaweza kupunguza kwa angalaru asilimia 60 kutoka viwango vinavyokadiriwa kisekta mwaka 2050. 

“Sekta ya kupoza joto lazima ipanuliwe ili iweze kumlinda kila mtu dhidi ya ongezeko la viwango vya joto, kuimarisha ubora wa chakula, usalama na kuhifadhi chanjo, halikadhalika uchumi uwe na ufanisi,” amesema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, ambaye amezindua ripoti hiyo wakati wa mkutano na waandishi wa habari kwenye jiji la maonesho, au Expo City huko Dubai ambako mkutano wa COP28 umekuwa ukiendelea tangu Alhamis iliyopita. 

“Hata hivyo upanuzi wa sekta ya kupoza joto usije na gharama kwenye kipindi cha mpito cha nishati kwani italeta madhara makubwa zaidi kwenye tabianchi,” amesisitiza Bi. Andersen. 

Katibu Mkuu atembelea Antarctica
UN Photo/Mark Garten
Katibu Mkuu atembelea Antarctica

Ahadi ya kupoza joto duniani 

Ripoti hiyo ilitolewa kuunga mkono ‘Ahadi ya kupoza joto duniani’, ambao ni mpango wa pamoja kati ya Umoja wa Falme za Kiarabu, (UAE) ambao ni wenyeji wa COP28 na mpango unaongozwa na UNEP uitewao ‘Ushirika wa kupoza joto.” 

Mpango unaainisha hatua za kuchukua ili kutumia mbinu tulivu za kupunguza joto kama vile vivuli vya kiasili, kuweko kwa mzunguko wa hewa, viwango vya juu vya matumizi ya nishati kwa ufanisi na kuondokana na dutu aina ya hydrofluorocarbons hususan kwenye majokofu, ambazo zinaongoza katika kukwangua ukanda wa ozoni. 

Kwa kufuatia mapendekezo ya ripoti hiyo, makadirio ya kupunguza hewa chafuzi kwenye sekta ya biashara yanaweza kupungua ifikapo mwaka 2050 kwa kukata takribani tani bilioni 3.8 za hewa ya ukaa. 

Sasa hiyo ina maana kwamba: 

  1. Itaruhusu nyongeza ya watu bilioni 3.5 kunufaika na majokofu, viyoyozi au mbinu tulivu za kupoza joto ifikapo mwaka 2050. 
  2. Itapunguza Ankara za umeme kwa watumiaji kwa dola trilioni 1 mwaka 2050, na dola trilioni 17 kwa ujumla kati ya mwaka 2022 na 2050.