Hali si hali Somalia, mafuriko makubwa baada ya ukame wa miaka minne mfululizo
Hali si hali Somalia, mafuriko makubwa baada ya ukame wa miaka minne mfululizo
Mkutano wa COP28 ukiendelea Dubai, Falme za kiarabu kusaka suluhu dhidi ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi, huko Somalia mafurikio makubwa yameendelea kusababisha zahma kwa wananchi ambapo Umoja wa Mataifa kupitia ofisi yake ya uratibu wa misaada ya dharura, OCHA umezungumzia hali halisi na nini kinafanyika.
Kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwa njia ya mtandao kutokea Mogadishu,Somalia, OCHA imebainisha kuwa Somalia inakabiliana na mafuriko yaliyoyaathiri maeneo mengi.
Tangu mvua za msimu kuanza mwezi wa Oktoba,zaidi ya watu milioni 2 wameathirika.Milioni wameachwa bila makazi na wengine 100 wameuawa hasa katika maeneo ya Kusini Magharibi, Galmudug, Puntland, Hirshabelle, Banadir na Jubaland.
Kwenye mkutano huo, Naibu mwakilishi maalum wa Katibu Mmkuu wa Umoja wa Mataifa,na mratibu wa misaada ya dharura, George Conway, alielezea kuwa ametiwa moyo na mashirika ya kibinadamu yanayoshirikiana na uongozi pamoja na jamii kuokoa maisha katika mazingira magumu.
Mvua zinazoendelea na mafuriko yamesababisha mawasiliano kukatika, vijiji kuporomoka na barabara kuharibika.
Kwa upande wake,Mkurugenzi wa muungano wa mashirika yasiyo ya kiserikali ya Somalia, Nimo Hassan, amebainisha kuwa uharibifu mkubwa umetokea na ipo haja ya kuwekeza katika suluhu za kudumu za kupambana na mafuriko kadhalika kutoa tahadhari ya mapema ili kuokoa maisha ya Wasomali.
Takwimu rasmi zinaashiria kuwa wahudumu wa dharura wamewafikia kiasi ya watu laki Nane na Elfu Ishirini (820,000) na kuwapa usaidizi wa kuokoa maisha ila mahitaji bado yanaongezeka kwasababu ya mafuriko.
Kamishna wa mamlaka ya udhibiti wa hali ya dharura nchini Somalia Mahamud Moalim anasema hatua ya muhimu kwa sasa ni kuwaokoa walionasa kwenye mafuriko na kuwapa msaada wa haraka wa kibinadamu.
Duru zinaeleza kuwa zahma hiyo inatokea wakati ambapo mamilioni ya raia wa Somalia wanakabiliana na njaa na utapiamlo huku watoto kiasi ya milioni 1.5 walio na umri wa chini ya miaka 5 huenda wakatatizwa na utapiamlo sugu katika kipindi cha agosti 2023 na Julai 2024.
Mpango wa usaidizi wa dharura kwa Somalia kwa mwaka huu wa 2023 unahitaji dola bilioni 2.6 kukimu mahitaji ya watu milioni 7.6.