Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nimejikomboa nataka kila anayekatiliwa kujikomboa pia: Angela Muhindo

Angela Muhindo kutoka Uganda, mwanamke ambaye baada ya kukatiliwa sasa amekuwa mchagizaji mkubwa wa kupambana na ukatili dhidi ya wanawake.
UN Women
Angela Muhindo kutoka Uganda, mwanamke ambaye baada ya kukatiliwa sasa amekuwa mchagizaji mkubwa wa kupambana na ukatili dhidi ya wanawake.

Nimejikomboa nataka kila anayekatiliwa kujikomboa pia: Angela Muhindo

Wanawake

Wakati dunia ikiendelea na maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia zilizoanza November 25 na zitafikia ukingoni December 10,2023, juhudi za kukabiliana na makovu yatokanayo na vitendo vya ukatili, unyanyasaji  na ubaguzi wa kijinsia zimeanzakuzaa matunda kwa wanawake kujua na kutambua haki zao za msingi. Angela Muhindo ni mkazi wa Wilaya ya kasese nchini Uganda,ni miongoni mwa waathirika wa ukatili wa kijinsia na licha ya mikikimikiki aliyokutana nayo  amefanikiwa kufungua ukurasa mpya na sasa anawatetea wanawake wengine baada ya kupata mafunzo kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya Wanawake  UN Women

Angela ambaye baada ya kukatiliwa sasa amekuwa mchagizaji mkubwa wa kupambana na ukatili dhidi ya wanawake, anasema, "Wanawake wana nguvu kidogo, lakini kama wewe ni mlemavu uko katika hatari zaidi ya kukatiliwa."

Ulimwenguni kote wanawake na wasichana wenye ulemavu wana uwezekano zaidi ya mara mbili ya wanawake wengine kukumbwa na ukatili wa kijinsia, Angela anaeleza jinsi mambo yalivyo badilika, 

“Baada ya mama kufariki nilirithi ardhi yake lakini wajomba zangu walijaribu kuichukua kwa nguvu, kwani wameamini sina haki, bila ardhi, huna nyumba, chakula, na kipato huna hivyo wanaume watakutumia vibaya.”

Angela(wa pili kushoto), akishiriki mafunzo kuhusu haki za wanawake na ukatili wa kijinsia.
UN Women
Angela(wa pili kushoto), akishiriki mafunzo kuhusu haki za wanawake na ukatili wa kijinsia.

Angela anaongeza kwamba, “Nilipata mafunzo ya haki za wanawake, haki za walemavu na haki ya ardhi, nilijifunza mimi ni sawa na kila mtu, naweza kumiliki ardhi kama mtu mwingine yeyote, hivyo nilianza mchakato wa kuidai, haikuwa rahisi lakini hatimaye ikawekwa jina langu. Ninakuwa sauti kwa wasio na sauti ili kuwazuia wasipate kile ninachotaka kupitia, natumai wengine watasimamia haki zao kama nilivyofanya, nina ardhi yangu, ardhi hii ndio kila kitu nina nyumba inanipatia chakula na kipato.”

Angela baada ya kujikomboa sasa amekuwa mkombozi kwa wanawake wengine. zaidi ya watu 300,000 nchini Uganda wamehudhuria programu za jumuiya kuhusu haki za wanawake tangu 2009, huku wakiungwa mkono na mpango wa uangalizi kupitia UN Women, chombo cha Umoja wa Mataifa kinachopambania usawa wa kijinsia.