Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkimbizi wa zamani Abdullahi Mire atwaa tuzo ya UNHCR ya Nansen 2023

Mwanaharakati mkimbizi na mwandishi wa habari, Abdullahi Mire (kushoto) ndie mshindi wa kimataifa wa tuzo ya Nansen ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR kwa mwaka huu wa 2023. Hapa akiwa kambini Dadaab nchini Kenya akitekeleza maj…
© UNHCR/Anthony Karumba
Mwanaharakati mkimbizi na mwandishi wa habari, Abdullahi Mire (kushoto) ndie mshindi wa kimataifa wa tuzo ya Nansen ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR kwa mwaka huu wa 2023. Hapa akiwa kambini Dadaab nchini Kenya akitekeleza majukumu yake.

Mkimbizi wa zamani Abdullahi Mire atwaa tuzo ya UNHCR ya Nansen 2023

Wahamiaji na Wakimbizi
  • Alizaliwa Somalia, akakulia kambini Dadaab Kenya kisha akahamia Norway
  • Sasa ni mwanahabari na alirejea Kenya kuhudumia jamii yake na kusongesha elimu kwa watoto wakimbizi
  • Mkuu wa UNHCR ampongeza; mwenyewe asema tuzo si ya kwake peke yake

Shirika la Umoja sagini Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR leo limemtangaza Abdullahi Mire mkimbizi wa zamani na mwandishi wa habari ambaye amekuwa kinara wa kupigania haki ya elimu huku akikabidhi vitabu 100,000 mikononi mwa watoto wakimbizi nchini Kenya kuwa ndiye mshindi wa kimataifa wa tuzo ya wakimbizi ya Nansen mwaka huu 2023.

Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa ya UNHCR, iliyotolewa leo jijini Geneva, Uswisi.

Kauli ya Mkuu wa UNHCR

Kamishi Mkuu UNHCR Filippo Grandi, amesema “Abdullahi Mire ni thibitisho hai kwamba mawazo ya mageuzi yanaweza kutoka ndani ya jamii zilizotawanywa. Ameonesha ustadi mkubwa na ukakamavu katika kuimarisha ubora wa elimu ya wakimbizi."

Chimbuko lake

Mire alizaliwa nchini Somalia, na alikulia katika kambi za wakimbizi za Dadaab nchini Kenya.

Hatimaye alipewa makazi mapya Norway, lakini hamu ya kutumikia jamii yake ilimrudisha nyuma alikokulia.

Alipata kazi nchini Kenya kama mwandishi wa habari na kuanzisha Kituo cha Elimu kwa Vijana Wakimbizi, shirika linaloongozwa na wakimbizi wenyewe ambalo limefungua maktaba tatu katika kambi hizo za wakimbizi, maktaba zilizo na vitabu vilivyotolewa bure kama msaada na kupanua fursa za kujifunza kwa makumi ya maelfu ya watoto na vijana waliokimbia makazi yao.

Baada ya kutangazwa kuwa ndiye mshini Mire mwenye umri wa miaka 36 amesema “Ushidi huu sio wangu peke yangu ni wa watu wote wanaojitolea ninaofanyanao kazi, ni kwa ajili ya watoto walio mashuleni”

Abdullahi Mire mkimbizi wa zamani mchagizaji mkuu wa elimu kwa watu waliotawanywa ndiye mshindi wa tuzo ya UNHCR ya Nansen mwaka huu
© UNHCR/Anthony Karumba
Abdullahi Mire mkimbizi wa zamani mchagizaji mkuu wa elimu kwa watu waliotawanywa ndiye mshindi wa tuzo ya UNHCR ya Nansen mwaka huu

Washindi wa kikanda wa Nansen 2023

Tuzo ya Nansen pamoja na kuwa na mshindi wa jumla wa kimataifa, huwa ina kipengele cha washindi wa kikanda ambao mwaka huu ni:

•   Elizabeth Moreno Barco – Kanda ya Amerika Mtetezi wa Haki za Binadamu kwa jamii zilizoathiriwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe Colombia;

•   Asia Al-Mashreqi – Kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini. Yeye ni Musisi na Mwenyekiti wa Mfuko wa Maendeleo Endelevu uliosaidia takribani watu milioni 2 walioathiriwa na mzozo nchini Yemen. 

•   Abdullah Habib, Sahat Zia Hero, Salim Khan na Shahida Win – Kanda ya Asia na Pasifiki. Hawa ni wasimulizi wanne wa simulizi za warohingya wakiandika uzoefu wa wakimbizi wa Rohingya wasio na utaifa. 

•   Lena Grochowska na Władysław Grochowski – Kanda ya Ulaya. Hawa ni wanandoa ambao hoteli na shirika lao linatoa malazi na mafunzo kwa wakimbizi.

Tuzo zitatolewa kwenye hafla itakayofanyika Geneva, Uswisi tarehe 13 mwezi ujao wa Desemba wakati wa Jukwaa la Wakimbizi la mwaka huu wa 2023 au Global Refugee Forum 2023

Hafla hiyo itanadi pia kazi za washindi hao na hafla hiyo itaambatana na burundani kutoka kwa wasanii Lous na the Yakuza, MIYAVI na Ricky Kej.

Tuzo ya Nansen

Tuzo hizo zinawezekana kupitia msaada kutoka kwa serikali za Norway na Uswisi, wakfu wa IKEA, na jiji na jimbo la Geneva.

Tuzo hiyo imepewa jina la mgunduzi, mwanasayansi, mwanadiplomasia na mfadhili wa kibinadamu Fridtjof Nansen kutoka  nchini Norway.

Tuzo ya Wakimbizi ya UNHCR ya Nansen iliyoanzishwa mwaka wa 1954 inawaenzi watu binafsi, makundi na mashirika ambayo yanavuka mipaka ya wajibu wa kuwalinda wakimbizi, wakimbizi wa ndani na na watu wasio na utaifa.

Kufahamu zaidi kuhusu usuli wa tuzo ya Nansen bofya hapa