Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa G20 hakikisheni joto duniani linasalia nyuzi joto 1 .5º. C: Guterres

Katibu Mkuu UN António Guterres akizungumza wakati wa mkutano wa G20 kwa njia ya video.
UN Photo/Mark Garten Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihudhuria mkutano wa G-20 kwa njia ya mtandao akiwa Santiago Chile

Viongozi wa G20 hakikisheni joto duniani linasalia nyuzi joto 1 .5º. C: Guterres

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kuhakikisha haki ya kifedha, kimuundo na mabadiliko ya tabianchi katika mkutano wa kilele wa nchi 20 zenye uchumi mkubwa zaidi duniani au G-20.

Katika ujumbe wake kwa njia ya video leo kwenye mkutano huo unaofanyika kwa njia ya mtandao Guterres amesema “Umoja wa Mataifa unawataka wanachama hao watoke na matokeo kabambe, ya kuaminika na ya haki ili kupunguza ongezeko la joto duniani hadi kufikia chini ya nyuzi joto 1.5º C."

António Guterres ameelezea hali halisi na kuongezeka kwa ukosefu wa usawa, changamoto ya mabadiliko ya tabianchi, migogoro na njaa.

Amesisitiza kuwa fursa ya fedha inapungua, huku mzigo wa madeni na bei za kila kitu zikipanda. 

Ameonya kwamba mambo haya yanasababisha mazingira ya "kichocheo cha ukosefu wa utulivu na madhila ulimwenguni kote."

Marekebisho ya kimataifa ya benki za maendeleo

Wakati akitoa wito wa haki ya kimuundo, mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ametaja mwelekeo wa urais wa Brazil katika kuleta mageuzi kwenye benki za maendeleo za kimataifa na uongozi wa kimataifa kuhusiana na suala hilo. 

Tangu Septemba, Brazil imekuwa kichwa cha G20.

Guterres ametoa wito pia wa kupewa kipaumbele katika haki ya fedha alipozungumzia kuundwa kwa kikosi cha viongozi kufuata utekelezaji wa kichocheo cha malengo ya maendeleo endelevu SDGs. Lengo ni kuruhusu kifurushi cha zaidi ya dola bilioni 500 kwa ajili ya hatua za maendeleo za muda mrefu.

Kwa Katibu Mkuu, ulimwengu pia unahitaji haki dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Wakati mkutano wa 28 wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi au COP28 ukikaribia, Guterres ameziomba nchi za G20 kuwasilisha "matokeo kabambe, ya kuaminika na ya haki ili kutimiza lengo la kupunguza ongezeko la joto duniani la kusalia nyuzi joto 1.5º C ikilinganishwa na viwango vya kabla ya maendeleo ya viwanda.

Mfuko wa Hasara na Uharibifu

Guterres pia ameutaka umoja huo wa G-20 kutekeleza mfuko wa hasara na uharibifu kwa kuhakikiza zinatimiza ahadi zake za usaidizi wa kifedha.

Mapendekezo mengine yalikuwa ni kuongeza mara tatu uwezo wa nishati mbadala, ufanisi wa nishati maradufu na kuhakikisha kuwa nishati safi inamfikia kila mtu ifikapo mwaka 2030. 

Katibu Mkuu pia ametetea hoja ya uondoaji endelevu wa nishati ya mafuta kisukuku, kwa kuweka ratiba iliyo wazi kulingana na kiwango cha choto kilichowekwa ili kuhakikisha kinasalia nyuzi joto 1 .5º. C.