Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS watumia ngoma za kitamaduni kuleta jamii pamoja

Wanawake wa Sudan Kusini wakiwa wamevalia mavazi ya kitamaduni wakitumbuiza katika tamasha la amani huko Aweil, Sudan Kusini.
UNMISS Wananchi wa Sudan Kusini washerehekea tamasha la utamaduni la amani.

UNMISS watumia ngoma za kitamaduni kuleta jamii pamoja

Utamaduni na Elimu

Katika kukuza utangamano ndani ya jamii yenye makabila tofauti ambayo hapo awali yalikuwa na misuguano Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS kwakushirikiana na wizara ya Utamaduni ya Sudan Kusini imefanya huko katika jimbo la Equatoria Magharibi. 

Ni sauti za ngoma, marimba, filimbi , vuvuzela na mirindimo mbalimbali ikisikika katika mji wa Yambio ulioko jimboni Equatoria Magharibi hapa Sudan Kusini, mamia ya wananchi wengine wakiwa wamevalia vibwebwe viunoni na mavazi ya asili wakicheza kwa pamoja kufurahia utajiri wao wa utafauti wa makabila. 

Afisa wa masuala ya kiraia wa UNMISS Emmanuel Dukundane anasema makabila tisa yamekutanishwa hapa,

“Shughuli hii ni kwa ajili ya kuonesha tofauti zetu, utofauti wetu kwenye masuala ya utamaduni na lengo ni sote tuwe na furaha. Na kupitia furaha hiyo tunaweza kukuza mshikamano wa kijamii, tunaweza kufahamiana zaidi, kuthaminiana zaidi, na kusahau changamoto zetu za zamani.” 

Na ama hakika wananchi hapa wamefurahi na hawataki kabisa kukumbuka ya kale kwani yanaumiza kama anavyoeleza Mama Hellen Mading mkazi wa Yambio, “Wakati tunapokuwa na migogoro sisi wanawawake na watoto ndio tunateseka. kwakweli tunahitaji amani, acha tuishi kwa amani kila siku. Tunataka watoto wetu wakue katika mazingira mazuri ili wapate elimu na waje kuwa viongozi wetu wa baadae.” 

Tamasha hili limeandaliwa na UNMISS wakishirikiana na wizara ya utamaduni, vijana na michezo na kijana James Amabele anasema walikuwa wakisubiri tukio hili kwa hamu, “Matukio kama haya ndio yataleta amani miongoni mwa wanajamii na Sudan Kusini kwa ujumla. Hili ndilo tulikuwa tukilitamani litokee, lazima tuwe na umoja, na ikiwa kila kitu kitaenda vizuri, basi amani itatawala. Hii ndio amani yenyewe. Tulikuwa tukililia amani na hapa tupo katika umoja na amani; makabila yote yameungana.”

Kwa UNMISS, hii ni hatua moja kuelekea kujenga amani ya kudumu na endelevu miongoni mwa jamii ambazo zimekumbwa na mgogoro, mmoja baada ya mwingine katika taifa lote la Sudan Kusini.