Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabadiliko tabianchi ni ‘mwiba mkali’ kwa wajawazito na watoto

Mwanamke mmoja huko Udaipur, India, anaelekea kliniki na mwanae kwa ajili ya uchunguzi wa ujauzito. Wanawake wajawazito na watoto wanakabiliwa na hatari kubwa za kiafya kutokana na majanga ya mabadiliko ya tabianchi ambayo yanahitaji tahadhari ya haraka.
© UNICEF/Ruhani Kaur
Mwanamke mmoja huko Udaipur, India, anaelekea kliniki na mwanae kwa ajili ya uchunguzi wa ujauzito. Wanawake wajawazito na watoto wanakabiliwa na hatari kubwa za kiafya kutokana na majanga ya mabadiliko ya tabianchi ambayo yanahitaji tahadhari ya haraka.

Mabadiliko tabianchi ni ‘mwiba mkali’ kwa wajawazito na watoto

Tabianchi na mazingira

Wanawake wajawazito, watoto wachanga na watoto wanakabiliwa na hatari kubwa za kiafya kutokana na majanga ya mabadiliko tabianchi hivyo hatua zote za kukabili mabadiliko ya tabianchi zisiwaengue, yamesema leo mashirika ya Umoja wa Mataifa wakati huu wa kuelekea mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP28 utakaoanza mwishoni mwa mwezi huu huko Dubai, Falme za Kiarabu.

Kauli hiyo imo kwenye waraka wa Wito wa Kuchukua hatua uliozinduliwa mtandaoni na mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa, lile la afya WHO, kuhudumia watoto, UNICEF na Idadi ya Watu na Afya ya  Uzazi, UNFPA pamoja na Ubia wa Wajawazito, Watoto wachanga na Afya ya Mtoto, PMNCH. 

Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa Huduma ya Afya katika shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani (WHO) Bruce Aylward, amesema mabadiliko ya tabianchi yanaleta tishio kwa wote lakini wanawake wajawazito, watoto wachanga na watoto wanakabiliwa na baadhi ya matokeo mabaya zaidi.  

Bwana Aylward amenukuliwa kwenye waraka huo uliotolewa mjini Geneva, nchini Uswisi na New York, nchini Marekani akisema mustakabali wa watoto unahitaji kulindwa kwa uangalifu, ambayo inamaanisha kuchukua hatua kwa tabianchi sasa kwa ajili ya afya zao na kuishi, wakati wa kuhakikisha mahitaji yao ya kipekee yanatambuliwa katika majibu ya hali ya hewa. 

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF wa Programu, Omar Abdi amesema hatua juu ya mabadiliko ya tabianchi mara nyingi hupuuza suala kwamba miili na akili za watoto viko katika hatari ya kipekee ya uchafuzi wa mazingira, magonjwa hatari na madhara ya tabianchi. 

“Tunafanya hivi kwa hatari yetu, janga la tabianchi linahatarisha haki ya msingi ya kila mtoto ya afya na ustawi, ni jukumu letu la pamoja kuwasikiliza na kuwaweka watoto katika kitovu cha hatua za dharura dhidi ya madhara ya tabianchi, kuanzia COP28, huu ni wakati wa kuwaweka watoto kwenye ajenda ya mabadiliko ya tabianchi”. 

Madhara hutokea kwa mtoto aliyeko tumboni 

Mwaka wa 2023 umekuwa na mfululizo wa majanga ya tabianchi ikiwa ni pamoja na mioto ya nyika, mafuriko, mawimbi ya joto na ukame kuhamisha watu, na kuua mimea na mifugo, na kuzidisha uchafuzi wa hewa, huku ulimwengu wa joto kupita kiasi unaongeza kuenea kwa magonjwa hatari kama kipindupindu, malaria na dengue, na matokeo mabaya kwa wanawake wajawazito na watoto ambao maambukizi haya yanaweza kuwa makali zaidi. 

Utafiti unaonesha kuwa madhara yanaweza kutokea hata tumboni, hivyo kusababisha matatizo yanayohusiana na ujauzito, mtoto kuzaliwa njiti, kuzaliwa na uzito mdogo na mtoto kufia tumboni; madhara haya yanaweza kudumu maisha yote, na kuathiri ukuaji wa miili na akili zao wanapokua. 

Mikakati ya kushughulikia janga hilo 

Wito wa Kuchukua Hatua unaangazia hatua saba za dharura za kushughulikia hatari hizi zinazoongezeka, ikiwa ni pamoja na upunguzaji endelevu wa uzalishaji wa gesi chafuzi na hatua juu ya ufadhili kwa tabianchi, sambamba na ujumuishaji mahsusi wa mahitaji ya wanawake wajawazito, watoto wachanga na watoto ndani ya sera zinazohusiana na tabianchi na maafa. 

Mashirika hayo pia yametoa wito wa kufanyika kwa utafiti zaidi ili kuelewa vyema athari za mabadiliko ya tabianchi kwa afya ya uzazi na mtoto. 

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Mipango katika UNFPA, Diene Keita amesema "ili kupata masuluhisho ya mabadiliko tabianchi ambayo yanakabili mahitaji ya kiafya na udhaifu wa wanawake na wasichana lazima tuanze kwa kuuliza maswali sahihi,". 

Wakati wa mikutano ya COP28, wajumbe wataadhimisha kwa mara ya kwanza Siku ya Afya, wakibainisha uhusiano usioweza kuyumbishwa kati ya afya ya watu na sayari.