Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mali: MINUSMA yaendelea kufunga virago 

Mlinda amani kutoka Nigeria anayehudumu katika mpango wa MINUSMA nchini Mali akitoa Ulinzi Mashariki mwa Mali.
© MINUSMA/Harandane Dicko
Mlinda amani kutoka Nigeria anayehudumu katika mpango wa MINUSMA nchini Mali akitoa Ulinzi Mashariki mwa Mali.

Mali: MINUSMA yaendelea kufunga virago 

Amani na Usalama

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Mali, MINUSMA umeendelea kufunga vituo vyake nchini humo ikiwa ni katika kutekeleza mpango wa Umoja wa Mataifa wa kuondoka kwa ujumbe huo nchini Mali. 

Stéphane Dujarric, ambaye ni msemaji wa Umoja wa Mataifa, hii leo akizungumza na wanahabari katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani amesema  kituo cha hivi karibuni zaidi kufungwa cha ya MINUSMA, ni kile cha Ansongo, katika eneo la Gao, mashariki mwa Mali.  

Kituo kimefungwa Jumamosi tarehe 18 Novemba na kukabidhiwa kwa mamlaka za kiraia.  

Katika muongo mmoja uliopita wa huduma huko Ansongo, walinda amani wa MINUSMA wamekuwa na jukumu muhimu katika kuleta utulivu eneo hilo na kuchangia kupunguza athari za vikundi vya kigaidi, kwa kuunga mkono mamlaka za mitaa na Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Mali.”   

Bw. Dujarric vilevile amesema kuwa MINUSMA imebainisha kuwa juhudi hizi ni pamoja na kupata barabara ya kuvuka mipaka inayounganisha nchi za Niger na Mali, ambayo imekuwa muhimu kwa nchi hizo na eneo nzima.   

Ili kulinda raia na kurejesha mamlaka ya serikali, ujumbe huo pia ulifanya shughuli nyingi, ikiwa ni pamoja na kujenga na kuandaa vifaa kwa ajili ya vikosi vya Mali na polisi wa eneo hilo, kutoa mafuta kwa ajili ya doria zao za usalama, na kulinda uwanja wa ndege kwa ajili ya shughuli za kibinadamu.   

Kwa kumalizia, Bw.Dujarric aliongeza kuwa ujumbe wa kulinda amani nchini Mali pia ulitoa huduma za msingi ili kusaidia kuzuia migogoro ya jamii na kuboresha hali ya maisha, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa maji safi ya kunywa na umeme. 

Licha ya maboresho hayo, ukosefu wa usalama unaoendelea bado ni changamoto, hasa kutokana na uwepo mdogo wa mamlaka za kitaifa.   

“Kambi ya Ansongo ni ya tisa kati ya vituo 13 ambavyo vimefungwa chini ya mpango wa MINUSMA kujiondoa kutoka Mali ifikapo tarehe 31 Desemba mwaka huu.  

Hiyo ni kwa mujibu wa azimio la Baraza la Usalama.   

Kambi ya Mopti itafungwa mapema Desemba, na awamu ya kufilisi katika maeneo yaliyosalia ya Timbuktu, Gao na Bamako itaanza tarehe 1 Januari mwaka wa 2024.