Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nigeria: Maadhimisho ya Siku ya Watoto Duniani  yaangazia athari za mabadiliko ya tabianchi kwa watoto

Watoto wakisimama kwenye maji ya mafuriko katika Jimbo la Borno, Nigeria.
© UNICEF/Vlad Sokhin
Watoto wakisimama kwenye maji ya mafuriko katika Jimbo la Borno, Nigeria.

Nigeria: Maadhimisho ya Siku ya Watoto Duniani  yaangazia athari za mabadiliko ya tabianchi kwa watoto

Haki za binadamu

Ikiwa leo ni siku ya mtoto duniani, nchini Nigeria wametumia siku hii kutathmini athari wanazozipata watoto kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Katika taifa hilo lililopo Afrika Magharibi lenye jumla ya watu milioni 233 watoto wanachukua asilimia 51 ya taifa hilo ndio maana mashirika ya Umoja wa Mataifa , serikali na wadau wengine wakaona haja ya kutumia siku hii kuzungumza namna bora ya kuwasaidia. 

Katika maadhimisho yaliyofanyika jijini Abuja nchini Nigeria Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF nchini humo Cristian Munduate, amesema, “sherehe hizi ni jukwaa muhimu kwa watoto wetu, walioathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi, kuelezea wasiwasi na uzoefu wao. Maoni yao ni muhimu katika kuunda njia yetu ya pamoja kuelekea mustakabali endelevu na thabiti.”  

Matukio ya hali mbaya ya hewa yalishuhudia watoto wakiathirika zaidi katika mikoa mbalimbali ikiwa Abuja, Kano, Lagos, Enugu, Sokoto, na Maiduguri. Takwimu zinaonesha kuwa kati ya mwaka 2016 hadi 2021 watoto 650,000 walilazimika kuyahama makazi yao kutokana na mjanga ya kimazingira.

Majadiliano yaliyofanyika hii leo yamehusisha kuangalia athari za moja kwa moja za kiafya zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi kwa watoto, kama vile ongezeko la hatari za kimwili, magonjwa yatokanayo na maji na utapiamlo ambayo yanakuwa na athari kwa mustakabali wa maisha yao.

Mwanamke akijarivu kuvuka maji ya mafuriko mjini Jakusko jimbo la Yobe Nigeria
© WFP/Arete/Ozavogu Abdul
Mwanamke akijarivu kuvuka maji ya mafuriko mjini Jakusko jimbo la Yobe Nigeria

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Kitaifa la Mpango Kazi wa Mabadiliko ya Tabianchi, Dkt. Salisu Dahiru, akizungumza katika katika maadhimisho hayo amesema Nigeria, ikiwa ni nchi ya pili kuwa na mazingira magumu duniani kote kwa watoto kukabiliwa na mabadiliko ya tabianchi, inakabiliwa na changamoto kubwa akitaja “Zaidi ya watoto milioni 110 wa Nigeria wako hatarini, baada ya kukabiliwa na hali mbaya ya joto inayoongezeka, mafuriko, ukame na dhoruba kali.” 

Dkt. Dahiru amesema mwitikio wa Nigeria katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi lazima iwe wa haraka na wa jumla, ukizingatia mahitaji ya watu wanaoishi katika mazingira magumu, wakiwemo watoto na wanawake, katika ngazi ya maamuzi, pamoja na utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Mabadiliko ya Tabianchi. 

Maadhimisho hayo pia yaliangazia juhudi za ushirikiano kati ya Serikali, washirika wa maendeleo, asasi za kiraia, na sekta binafsi, kwa kuzingatia utetezi, ushirikiano na elimu ya hali ya hewa.