Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kushindwa kuzuia mizozo ni aibu kubwa

Katibu Mkuu António Guterres (kushoto mezani) akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu kudumisha amani na usalama wa kimataifa, kudumisha amani kupitia maendeleo ya pamoja.
UN Photo/Eskinder Debebe
Katibu Mkuu António Guterres (kushoto mezani) akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu kudumisha amani na usalama wa kimataifa, kudumisha amani kupitia maendeleo ya pamoja.

Kushindwa kuzuia mizozo ni aibu kubwa

Amani na Usalama

Hakuna kushindwa ambako ni kubaya na janga la kupita kiasi kama kushindwa kuzuia mzozo, amesema Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa António Guterres hii leo akizungumza kwenye Baraza la Usalama la umoja huo jijini New York, Marekani. 

Guterres amesema cha kwanza kuathiriwa vibaya na vita na mizozo ni mafanikio ya maendeleo. 

Amesema hayo akihutubia mkutano wa Baraza hilo uliofanyika leo ukijikita kwenye kuendeleza amani endelevu kupitia maendeleo ya pamoja. 

Mizozo inapobisha hodi, maendeleo hutoweka 

“Tumeshuhudia mwelekeo huu wa vita kurudisha nyuma maendeleo yaliyopatikana duniani kote: kadri nchi inavyokaribia kutumbukia kwenye mzozo, ndivyo inazidi kuwa mbali na maendeleo endelevu na jumuishi,” amesema Guterres. 

Katibu Mkuu amegusia kuwa nchi 9 kati ya 10 zenye maendeleo duni au LDCs zikiwa na viwango vya chini zaidi vya vipimo vya maendeleo ya kibinadamu, zimekuwa zikikumbwa na mizozo au ghasia kwa kipindi cha miaka 10. 

Amesema ukosefu wa usawa na fursa, ajira zenye staha na uhuru wa kujieleza vinaweza kuchochea mkanganyiko na kuibua ghasia na ukosefu wa utulivu. 

Taasisi dhaifu na rushwa huchochea mizozo 

Zaidi ya hapo taasisi dhaifu na rushwa vinaongeza hatari za kuweko kwa mizozo, amesema Katibu Mkuu. 

Guterres amesema kama ambavoy ukosefu wa maendeleo unachochea hatari ya mizozo, kinyume chake pia ni sahihi kwani maendeleo ya biinadamu huangazia matumaini – yakichochea kuzuia mizozo, na kuendeleza amani na usalama. 

“Ndio maana kusongesha amani na kuchochea maendeleo endelevu na jumuishi vinaenda sambamba,” amesema Katibu Mkuu. 

Halikadhalika humaanisha kuhakikisha upatikanaji wa chakula, watu kupata elimu na stadi, huduma za afya na utu kwa wote. 

Umaskini pekee si kichocheo cha ghasia- Dilma 

Akihutubia Baraza, Dilma Rousseff ambaye ni Rais wa Benki Mpya ya Maendeleo, NDB, amesema amani endelevu inahitaji mfumo wa kina unaozingatia visababishi vya ghasia, lakini vile vile hali ya kiuchumi na kijamii. 

“Umaskini pekee hauelezei ghasia. Na sio watu wote au makundi yote yanayokumbwa na umaskini hujitumbukiza kwenye  mizozo,” amesema Dilma. 

Mizozo mikubwa huchochewa  kutoka nje ya nchi 

Jeffrey Sachs, Rais huyu wa Mtandao wa Umoja wa Mataifa kuhusu Majawabu ya Maendeleo Endelevu (UN Sustainable Development Solutions Network) amesema sababu moja ni kwamba vita kubwa lazima vichochewe kutoka nje; kifedha na kisilaha. 

Hivyo amesema “Baraza la Usalama linaweza kukubaliana kutokomeza vita hizo kwa kuzuia fedha na silaha kutoka nje ya nchi husika. Hili linahitaji makubaliano kutoka mataifa makubwa yenye nguvu.” 

Akigusia mizozo mikubwa minne inayoendelea, Bwana Sachs amesema “sababu nyingine vita hivi vinaweza kumalizika haraka ni kwa sababu ni matokeo ya masuala ya kiuchumi na kisiasa ambayo yanaweza kushughulikiwa kidiplomasia badala ya vita kwa kutatua mambo ya kiuchumi na kisiasa kwa Baraza la Usalama kuanzisha mazingira kwa ajili ya amani na maendeleo endelevu.”