Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN Women na wadau wasaidia waathirika wa ukatili wa kijinsia Kakamega Kenya

Mama Priscilla Oparanya ( kushoto) muasisi wa Touch A Life Foundation na wadau wa JHPIEGO. Rammah Mwalimu ( katikati) na Irene Choge ( meneja wa uenezi).
UN News/Thelma Mwadzaya
Mama Priscilla Oparanya ( kushoto) muasisi wa Touch A Life Foundation na wadau wa JHPIEGO. Rammah Mwalimu ( katikati) na Irene Choge ( meneja wa uenezi).

UN Women na wadau wasaidia waathirika wa ukatili wa kijinsia Kakamega Kenya

Wanawake

Wakati ulimwengu ukijiandaa kuadhimisha siku 16 za harakati kukabiliana na ukatili wa kijinsia katika jamii zinazoendeshwa na Umoja wa Mataifa, baadhi ya sehemu duniani zimeanza kulipa suala hilo uzito mkubwa ikiwemo Kenya. 

Kwa ushirikiano wa Shirika la Umoja wa mataifa la masuala ya wanawake UN Women na mengine yasiyo ya kiserikali, Kaunti ya Kakamega nchini nchini humo imefanikiwa kuzindua mpango maalum wa kuwapa waathirika wa ukatili wa kijinsia huduma za mahakamani pasi na malipo. 

UN Women imewashika mkono baadhi ya walioathirika kwa kuwapa bidhaa za matumizi na pia mtaji kuwawezesha kuanza biashara baada ya kuondoka kwenye vituo salama na vya staha. 

Kakamega ni moja ya maeneo yenye changamoto kubwa ya dhulma za kijinsia nchini Kenya na kuandaa makala hii.

Eneo la kaunti ya Kakamega ni tulivu na kijani kimetawala kwani Lina rutba na mvua za kuaminika.Hata hivyo jinamizi la unajisi na ubakaji unaozua mimba za utotoni limetandaza mbawa zake.Takwimu za hivi Karibuni za Wizara ya afya zinaashiria kuwa mtoto wa kike yuko katika hatari zaidi katika kaunti za eneo la magharibi ya Kenya. 

Ukatili wa kijinsia umeshamiri Kakamega

Takwimu za serikali za idadi ya watu na afya za 2022, ziazotolewa na  KDHS, zinaonyesha kuwa Kakamega ni ya nne kwenye orodha ya kaunti za magharibi mwa Kenya ambako mtoto wa kike yuko hatarini ukizingatia madhila ya kubakwa au kunajisiwa. 

Ili kupambana na jinamizi hilo, serikali ya kaunti ya Kakamega imezindua kituo cha kwanza cha kuwasitiri waliofanyiwa ukatili huo katika jamii. 

Rose Shitanda ni afisa wa tiba katika kaunti ya Kakamega na anabainisha kuwa tangu wachukue hatua hii mambo yamebadilika, kwani, “Wale wahudumu wa afya wamefundishwa jinsi ya kuwahudumia na kuwatibu. Kitu cha pili hawalipi. Sasa wanajua wakija kwenye vituo vyetu hakuna malipo na wanakuja saa yoyote na tunawahudumia saa 24 kwani vituo vyetu viko tayari. Tukipata kwamba msichana amedhulumiwa na kupata pia uja uzito,tunazungumza naye ili aweze kubeba mimba na hatimaye arejee shule.” 

Soundcloud

Msaada wa kisheria pasi na malipo

Ukatili wa ubakaji na unajisi unahitaji kuzuiwa na mkono mrefu wa sheria . 

Kwa msumeno wa sheria, serikali ya kaunti ya Kakamega ilizindua mpango wa kuwapa waathirika huduma za mahakamani pasi na malipo. Viviane Mbaka ni afisa wa sheria katika kaunti ya Kakamega na anakiri kuwa mpaka sasa kesi mbili zimepata matokeo yanayoleta tabasamu, “ Tulianzisha mpango huu kwani tuliona kuwa waathirika  wa dhulma za kijinsia wanahangaika. Mpango wenyewe ni wa bila malipo na wanapata huduma za mahakamani. Tumepata mawakili wanaotoa huduma hizo na kesi mbili tayari zimefanikiwa. Tunafurahia matokeo.”

Kimbilio na msaada

Waathirika wa dhulma za kijinsia wanahitaji sehemu salama za staha na kuwa mbali na waliowadhuru.Shirika la Umoja wa mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN Women limeunga mkono juhudi hizo hasa katika kaunti za magharibi ya Kenya. 

Christine Okeno ni mtaalam wa masuala ya dhulma za kijinsia na anafafanua kuwa waathirika wanahitaji kushikwa mkono,“ Kitu cha kwanza tulifanya ni kutathmini hali yao ili tujue tutakavyoweza kuwasaidia. Pili ilikuwa kuwapa mafunzo ili kutoa huduma salama kwa waathiriwa. Tunajua kuwa wanaopitia ukatili kama huo wanatatizika na ipo haja kuwasaidia ili warejee katika hali Sawa kijamii na kujitegemea. Tatu, tuliwanunulia bidhaa za matumizi wanazohitaji kama vile vyakula, vitanda na kadhalika. Mwisho tuliwaunganisha na huduma nyengine muhimu kama vile polisi na hospitali .” 

Vituo salama vya staha kwa waathirika

Kulingana na takwimu za mpango wa sekretarieti ya Generation Equality ya utekelezaji wa haki za wanawake unaosimamiwa na shirika la UNWomen, kati ya kaunti zote 47, Kuna vituo 54 kwenye kaunti 18 pekee vya kuwasitiri wathirika wa dhulma za kijinsia.

Generation Equality inabainisha kuwa kuwa kila wanawake 3 mmoja amepitia madhila ya dhulma za kijinsia.

Changamoto nyingine inayoandamana na unajisi na ubakaji ni mimba za utotoni. 

Kaunti ya Kakamega inajitahidi kupambana nazo kwa hali zote. Kupitia mpango maalum uliozinduliwa na shirika lisilo la kiserikali la Marekani la JHPIEGO, wanawake Sasa wanapata huduma za afya ya uzazi. Mpango huo ulifanikishwa na ofisi ya mke wa gavana wa kwanza wa kaunti ya Kakamega Priscilla Oparanya anayebainisha kuwa,“ Mara nyingi nilikuwa napigiwa mtoto amenajisiwa, mama au nyanya amebakwa,Visa vingi tu. Sasa nikajiuliza nitakachofanya ili Kina mama waone nimewasaidia wao pamoja na watoto katika kaunti yetu ya Kakamega. Kwa ujumla,watu wamejua Ukinajisi mtoto utachukuliwa hatua.”

Usawa wa kijinsia

Juhudi za jamii na mashirika kama JHPIEGO zimeleta tija katika vita dhidi ya unajisi, ubakaji na mimba za utotoni.

Harakati hizi zinaendana na Lengo la 5 na la 16 la orodha ya maendeleo endelevu ya umoja wa mataifa, SDGs ya kudumisha usawa wa kijinsia katika jamii.