Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gaza: 'Hospitali sio uwanja wa vita', mateso ya watoto lazima yakome

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell anatembelea hospitali ya Nasser huko Khan Yunis, Gaza, ambako alikutana na wagonjwa na familia zilizokimbia kutafuta makazi na usalama.
© UNICEF
Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell anatembelea hospitali ya Nasser huko Khan Yunis, Gaza, ambako alikutana na wagonjwa na familia zilizokimbia kutafuta makazi na usalama.

Gaza: 'Hospitali sio uwanja wa vita', mateso ya watoto lazima yakome

Haki za binadamu

Watoto wameuawa, wamekuwa walemavu, wametekwa nyara na kunyimwa msaada huko Gaza, na wahusika katika mzozo lazima "wakomeshe hali hii ya kutisha", amesema Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, Catherine Russell wakati wa ziara yake huko Gaza wakati huu ambapo operesheni za kibinadamu zikitarajiwa kusimama hii leo Jumatano kutokana na ukosefu wa mafuta.

Kauli yake hii imekuja huku kukiwa na ripoti za leo kuwa hii leo Jumatano  huko Gaza kumekuwa na uvamizi unaoendelea wa Jeshi la Israeli ndani ya hospitali ya Al-Shifa , ambapo wagonjwa wakiwemo watoto njiti wamekufa katika kipindi cha siku chache zilizopita baada ya mashine za kuwapa joto na vifaa vingine vya kuokoa maisha kutokuwa na umeme.

Katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kutoa misaada Martin Griffiths aliandika "Hospitali si uwanja wa vita," na kwamba "ulinzi wa watoto wachanga, wagonjwa, wafanyakazi wa sekta ya afya na raia wote lazima uondoe wasiwasi mwingine wote".

Akizungumza na Idhaa ya Habari ya Umoja wa Mataifa hapo awali, amesisitiza kwamba "Hamas lazima isitumie mahali kama hospitali kama ngao kwa uwepo wao" na kwamba "hospitali haipaswi kuwa eneo la hatari".

"Tunaona masuala haya mawili ni muhimu kwa usawa," anasisitiza.

'Ukiukaji mkubwa'

Bi.Russell amelaani "ukiukaji mkubwa" dhidi ya watoto uliofanywa na wahusika kwenye mzozo na akasema kwamba alikuwa Gaza "kufanya chochote niwezacho kutetea ulinzi wa watoto".

"Ndani ya Ukanda huo, hakuna mahali salama kwa watoto milioni moja wa Gaza kugeukia," akisisitiza kwamba zaidi ya watoto 4,600 wameripotiwa kuuawa na karibu 9,000 kujeruhiwa.

Watoto wengi wanaaminika kuzikwa chini ya vifusi vya majengo yaliyoporomoka, "matokeo ya kutisha ya matumizi ya silaha za milipuko katika maeneo yenye watu wengi", amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell(kulia) ametembelea hospitali ya Nasser huko Khan Yunis, Gaza, ambako alikutana na wagonjwa na familia zilizokimbia kutafuta makazi na usalama.
© UNICEF
Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell(kulia) ametembelea hospitali ya Nasser huko Khan Yunis, Gaza, ambako alikutana na wagonjwa na familia zilizokimbia kutafuta makazi na usalama.

Sitisha mapigano sasa

Mkuu huyo wa UNICEF alielezea kusikia simulizi za kuhuzunisha kutoka kwa wafanyakazi wa shirika lake na kusisitiza hatari kubwa kwa watendaji wa kibinadamu wanaofanya kazi ndani ya Gaza. Tangu tarehe 7 Oktoba wafanyakazi 102 wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA wameuawa katika eneo hilo.

Bi. Russell amerejea wito wa "kusitishwa kwa mapigano mara moja kwasababu za kibinadamu", kuachiliwa kwa watoto wote waliotekwa nyara na kuzuiliwa, na "ufikiaji salama, endelevu na usiozuiliwa" kwa wafadhili kwa watu wenye uhitaji.

OCHA: "Hali ya kutisha"

Mratibu mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura Martin Griffiths ameiambia Idhaa ya Umoja wa Mataifa kwamba kwa mtazamo wa kibinadamu na nje ya masuala yoyote ya kijeshi, "tatizo letu ni kulinda watu wa Gaza".

Amesisitiza  kwamba Wananchi wa Gaza wako katika "hali ya kutisha ambayo hawana njia ya kutoroka na wanaombwa kuhama wakiwa katika mazingira ya hatari".

Zaidi ya watu milioni 1.5 huko Gaza wanakadiriwa kuwa wakimbizi wa ndani, wakiwemo takriban 787,000 ambao wanakaa katika makazi 154 ya UNRWA, ambapo msongamano mkubwa unasababisha kuenea kwa magonjwa.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu OCHA inayoongozwa na Bwana Griffiths imeripoti leo Jumatano kwamba watu waliokimbia makazi yao waliokuwa kwenye mahema ya muda nje ya makazi huko kusini mwa Gaza kwa kukosa nafasi, sasa wanateseka kutokana na kuanza kwa mvua kubwa na mafuriko.

Malori ya misaada yamesimama

Kuhusu ukosefu wa mafuta, ambao haujaruhusiwa kuingia katika Ukanda huo tangu kuanza kwa mzozo huo, Bwana Griffiths amesema kwamba "tunahitaji angalau lita laki kadhaa ili kutufanya tusogee tena".

UNRWA ilisema jana Jumanne usiku kwamba malori yake ndani ya Gaza hayakuweza kuchukua msaada unaoingia kupitia mpaka wa Rafah kutoka Misri siku hiyo kwa sababu hayana mafuta.

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari usiku wa Jumanne, Israel ilitoa idhini ya lita 24,000 za mafuta ya dizeli kutumiwa na malori pekee kwa shughuli za Umoja wa Mataifa lakini haikufahamika ni lini na jinsi gani mafuta hayo yangetolewa.

‘Tuko tayari kwenda’

Bwana Griffiths ameeleza kuwa kusitishwa kwa mapigano pia kunahitajika ili kuruhusu sekta kibinafsi kufanya kazi na kuruhusu maduka yaliyopungua bidhaa kuuzwa tena. "Hiyo ni muhimu kama sio lazima zaidi, kwa shughuli zetu," alisema.

"Tuko pale pale, tumeketi mbele ya watu hao, kwenye mipaka ya Gaza, huko Rafah, tayari kwenda" na "kujaribu kuwafikia watu walipo", amesisitiza katika ombi lake la kupata kibali cha kuweza kuwafikia wananchi.

Amesema hii "Ni njia ya kawaida ya kufanya kazi katika shida kama hii".