Madhila Gaza imetosha mambo 10 lazima yatekelezwe kuleta afueni: Griffiths

Madhila Gaza imetosha mambo 10 lazima yatekelezwe kuleta afueni: Griffiths
Umoja wa Mataifa leo umesisitiza kwa mara nyingine kwamba kinachoendelea Gaza ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu huku kukiwa na ripoti kwamba vikosi vya Israel vimevamia Hospitali ya Al-Shifa jana usiku ambako mbali ya wagonjwa kuna maelfu ya raia waliotawanywa wanapata hifadhi na umeonya kwamba hospital sio uwanja wa vita na madhila hayo kwa raia wakiwemo watoto lazima yakome kwa kutekeleza mambo 10 ya muhimu.
Hali inaendelea kuwa janga kubwa la kibinadamu kwa watu wa Gaza kwa kumujibu wa mkuu wa masuala ya kibinadamu na msaada wa dharura wa Umoja wa Mataifa Martin Griffis ambaye kupitia tarifa yake iliyotolewa leo amesema “Wakati mauaji ya Gaza yakifikia viwango vipya vya kutisha kila siku, ulimwengu unaendelea kutazama kwa mshtuko huku hospitali zikiteketea, watoto wanaozaliwa njiti wanakufa, na watu wote wananyimwa njia za msingi za kujikimu. Hii haiwezi kuruhusiwa kuendelea.
Pande zinazozozana lazima ziheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu, zikubali kusitishwa kwa mapigano kwa minajili ya kibinadamu na kukomesha kabisa mapigano hayo.”

Kwa niaba ya jumuiya ya kibinadamu anayowakilisha, Griffiths amehimiza pande zote, wale wote walio na ushawishi juu pande kinzani, na jumuiya pana ya kimataifa kufanya kila liwezalo kuunga mkono na kutekeleza mambo kumi yafuatayo;
Mosi: Kuwezesha juhudi za mashirika ya misaada kuwa na mtiririko endelevu wa misafara ya misaada na kufanya hivyo kwa njia ya usalama.
Pili: Kufungua sehemu za ziada za kuvuka kwa ajili ya misaada na malori ybiashara kuingia, ikiwa ni pamoja na Kerem Shalom.
Tatu: Kuruhusu Umoja wa Mataifa, mashirika mengine ya kibinadamu na mashirika ya umma na ya kibinafsi kupata mafuta kwa wingi wa kutosha ili kutoa misaada na kutoa huduma za msingi.
Nnne: Kuwezesha mashirika ya kibinadamu kutoa misaada kote Gaza bila vikwazo au kuingiliwa.
Tano: Kuruhusu kupanua wigo wa idadi ya makazi salama kwa watu waliohamishwa katika shule na vituo vingine vya umma kote Gaza na kuhakikisha kwamba wanasalia kuwa sehemu za usalama wakati wote wa vita.
Sita: Kuboresha utaratibu wa taarifa za kibinadamu ambao ungesaidia kuwaepusha raia na miundombinu ya kiraia kutokana na uhasama na kusaidia kuwezesha ufikiaji wa kibinadamu.
Saba: Kuruhusu kuweka vituo vya usambazaji wa misaada kwa raia, kulingana na mahitaji.

Nane: Kuruhusu raia kuhamia maeneo salama na kurudi kwa hiari katika makazi yao.
Tisa: Kufadhili ombi la misaada ya kibinadamu, ambalo sasa linafikia dola bilioni 1.2.
Kumi: Tekeleza usitishaji mapigano wa kibinadamu ili kuruhusu huduma za msingi kuanza upya na biashara muhimu kuanza tena. Usitishaji huo wa mapigano pia ni muhimu kuwezesha utoaji wa misaada, kuruhusu kuachiliwa kwa mateka, na kutoa afueni kwa raia.
Amehitimisha tarifa yake kwa kusema kwamba “Hivi ndivyo vitendo vinavyohitajika kudhibiti mauaji. Mpango huu ni wa kina, na tumedhamiria kusukuma kila hatua, lakini tunahitaji uungwaji mkono mkubwa wa kimataifa.D unia lazima ichukue hatua kabla haijachelewa.”