Jinamizi hospitali Gaza linaendelea huku mvua zikisababisha hofu mpya ya kiafya: UN
Jinamizi hospitali Gaza linaendelea huku mvua zikisababisha hofu mpya ya kiafya: UN
Shirika la afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO leo lipongeza juhudi za kishujaa za wahudumu wa afya katika hospitali ya Al-Shifa iliyozingirwa mjini Gaza na kuelezea wasiwasi wake kwa mamia ya maelfu ya watu waliokimbia makazi yao katika eneo ambalo mvua kubwa imesababisha mafuriko na kuzidisha hali mbaya ya kiafya.
Msemaji wa WHO Margaret Harris amewaambia waandishi wa habari huko Geneva Uswis hii leo kwamba "Mvua itaongeza zaidi mateso kwa watu katika Ukanda huo, wakati ambapo kukatika kwa bomba la maji taka na uhaba wa maji vimesababisha kuongezeka kwa magonjwa yanayosababishwa na maji na maambukizi ya bakteria.”
WHO ilionya wiki iliyopita kwamba tangu katikati ya Oktoba, zaidi ya visa 33,500 vya kuhara vimeripotiwa, haswa miongoni mwa watoto chini ya umri wa miaka mitano, ikiwa ni mara 16 ya wastani wa kila mwezi.
Vituo vinavyoendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, ambako zaidi ya watu 580,000 waliokimbia makazi yao kusini mwa Gaza wamesaka hifadhi kutokana na mashambulizi ya Israel ya kulipiza kisasi kufuatia mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7, ni zaidi ya mara tisa ya uwezo wake na na msongamano unazidi kuongezeka na kuongeza hatari za kiafya.
"Tunaomba kusitishwa kwa mapigano sasa," amesisitiza Dkt. Harris.
Familia za mateka huko Geneva
Wakati huo huo huko Geneva, familia za baadhi ya mateka 238 wanaoshikiliwa na Hamas huko Gaza tangu tarehe 7 Oktoba leo walipaswa kuendelea na utetezi wao wa kuachiliwa kwa wapendwa wao.
Mkutano ulitangazwa kati ya familia za mateka na Mirjana Spoljaric, Rais wa Kamati ya Kimataifa ya chama cha Msalaba Mwekundu ICRC, shirika ambalo ni mshirika wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu.
Katika taarifa yake, ICRC imesema kwamba Bi. Spoljaric pia atakutana na mamlaka ya Israel na kwamba shirika hilo "limekuwa likitetea mara kwa mara kwa niaba ya mateka walioshikiliwa huko Gaza, ikiwa ni pamoja na moja kwa moja na Hamas na wahusika ambao wanaweza kuwa na ushawishi kwa pande zote.”
Wahudumu wa afya wanafanya kila wawezalo
Dkt. Harris wa WHO ameelezea kwa kina hali mbaya katika hospitali ya Al-Shifa, ambayo kwa sasa inalengwa na operesheni za jeshi la ulinzi la Israeli ambalo linadai kuwa Hamas ilianzisha kituo chake chini ya hospitali hiyo madai ambayo yamekanushwa na wahudumu wa afya wa hospitali hiyo.
Akizungumzia wahudumu wa afya wa kishujaa, Dkt. Harris amesema "Wahudumu hao wanafanya chochote wanachoweza kuendelea wakati kituo hicho hakina umeme tangu Novemba 11 na hakukuwa na chakula cha kutosha na maji safi.”
Wagonjwa takriban 700 bado walikuwepo katika eneo hilo na zaidi ya wahudumu 400 wa afya, pamoja na watu wapatao 3,000 waliokimbia makazi yao ambao walikuwa wametafuta hifadhi hapo. Dkt. Harris amesema vifo vya wagonjwa 28 vimeripotiwa katika saa 48 zilizopita.
Wakati huo huo, duru za habari asubuhi ya leo zimeonyesha kuwa jeshi la Israeli lilijitolea kutoa vifaa vya kupashajoto watoto njiti katika hospitali ya Al-Shifa, ambapo watoto 36 waliozaliwa kabla ya wakati wanahitaji uangalizi wa kila mara.
Takriban watoto sita waliozaliwa njiti wameripotiwa kufariki dunia katika muda wa siku tatu zilizopita kutokana na kwamba mashine zao za kupasha joto hazikuweza kufanya kazi kutokana na ukosefu wa umeme.
Uhamishaji wa wagonjwa ni mgumu sana
Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kuwahamisha wagonjwa, Dkt. Harris ameeleza kwamba wote waliosalia Al-Shifa walihitaji msaada muhimu ili waendelee kuishi.
Kuwahamisha "itakuwa jambo gumu sanahata katika mazingira bora", ukiachilia mbali huku kukiwa na milipuko ya mabomu, mapigano ya silaha na ukosefu wa mafuta kwa magari ya wagonjwa.
"Njia bora itakuwa kukomesha uhasama hivi sasa na kuzingatia kuokoa maisha, sio kupoteza maisha," amesisitiza.
Mashjambulizi kwenye huduma za afya yamekithiri
Mashambulizi 135 dhidi ya vituo vya afya yamerekodiwa huko Gaza katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, na Dkt. Harris wa WHO amesema hii ilikuwa idadi kubwa zaidi kurekodiwa katika muda mfupi kama huo.
"Natumai hii ndiyo rekodi mbaya zaidi ambayo tumewahi kuona," amesema.
Msemaji wa WHO ameashiria kuongezeka kwa mwelekeo wa mashambulizi dhidi ya huduma za afya, pia kuonekana katika migogoro mingine inayoendelea nchini Sudan na Ukraine. "Inaonekana kwamba kwa namna fulani kuelewa kuwa hospitali lazima iwe mahali salama, mahali ambapo watu wanakuja kutibiwa wanapokuwa na uhitaji, kumesahaulika," amewaambia waandishi wa habari.