Kisukari ni moja ya muuaji mkubwa kwa wenye VVU Uganda: WHO
Kisukari ni moja ya muuaji mkubwa kwa wenye VVU Uganda: WHO
Jijini Kampala, nchini Uganda, zaidi ya watu milioni 1.4 wanaishi na virusi vya ukimwi VVU na kati ya hao, asilimia 5.8 wana ugonjwa wa kisukari. Ugonjwa wa kisukari ni kawaida miongoni mwa watu wanaoishi na virusi vya ukimwi na ni mojawapo ya sababu kuu za vifo miongoni mwa watu hao kwa mujibu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO.
Shirika hilo linasema kwa ujumla, magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanachangia asilimia 36 ya vifo vya kila mwaka nchini Uganda. Kisukari hutokea wakati mwili hautoi insulini ya kutosha au hauwezi kutumia insulini kutokana na kushindwa kemikali ya mwili inayodhibiti sukari ya kwenye damu.
Ili kukabiliana na tishio hili la kiafya, Uganda inatekeleza mpango wa kuunganisha huduma kwa magonjwa yasiyoambukiza katika huduma za VVU. Mpango huo uliozinduliwa mwaka wa 2019 na unalenga kuboresha kinga, utambuzi kwa wakati, na udhibiti wa muda mrefu wa magonjwa sugu miongoni mwa watu wanaoishi na virusi vya ukimwi.
Ushirikiano mkubwa kati ya serikali ya Uganda, Shirika la WHO, Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa Maendeleo UNDP na Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na ugonjwa wa ukimwi umewezesha uhamasishaji wa zaidi ya dola milioni 6 ili kuongeza utekelezaji wa mpango huo mwaka wa 2022 na mwaka wa 2023.
Juhudi hizi, pamoja na upatikanaji bora wa matibabu ya VVU, zimesababisha kupungua kwa idadi ya vifo kati ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi, kutoka vifo 24,245 mwaka wa 2017 hadi vifo 16,450 mwaka wa 2023.
Kila baada ya miezi mitatu, Didas Byaruhanga, mwenye umri wa miaka 64 anayeishi na VVU na kisukari anazingatia matibabu yake ya kika siku ya kawaida ya udhibiti wa VVU katika taasisi ya Magonjwa ya Kuambukiza, IDI katika jiji la Kampala Uganda. Tangu alipogunduliwa mwaka wa 1998, anapokea huduma za mara kwa mara za VVU kutoka kwenye vituo mbalimbali vya afya nchini humo.
Miaka 14 baadaye, mwaka wa 2012, Byaruhanga aligundua kuwa alikuwa na ugonjwa wa kisukari alipokuwa akipatiwa matibabu katika taasisi hiyo baada ya kuugua kiharusi. Ugonjwa wa kisukari ni sababu ya hatari ya kupata kiharusi, na anasema, “nilipopatwa na kiharusi miaka 11 iliyopita, muuguzi aligundua kuwa kiwango changu cha sukari kilikuwa juu. Mara moja niliwekwa kwenye matibabu na nikapendekezwa kukutana na mtaalamu wa kisukari katika hospitali nyingine. Lkini, ilikuwa changamoto kwenda kwa madaktari wawili kutoka vituo tofauti vya afya kwa wakati mmoja."
Ili kurahisisha usimamizi wa magonjwa yanayoambukiza kama ya Byaruhanga, Uganda ilianzisha mkakati mwaka 2019 wa kuunganisha huduma za magonjwa yasiyoambukiza ndani ya huduma za virusi vya ukimwi.
Hii ina maana kwamba watu wanaoishi na VVU sasa wanaweza kudhibiti magonjwa yao kama vile shinikizo la damu, kisukari na saratani ya shingo ya kizazi katika kituo kimoja ambapo wanapokea udhibiti wa virusi vya ukimwi.
Dkt. Noella Owarwo, daktari na Naibu Mkurugenzi wa Taasis ya Magonjwa ya Kuambukiza, IDI anasema, "kupitia mpango wetu wa magonjwa yasiyoambukiza na virusi vya ukimwi, tunaona kupungua kwa matatizo yanayohusiana na kisukari miongoni mwa wateja, kwani ugonjwa huo hugunduliwa mapema, na hivyo kuwezesha usimamizi wa mgonjwa kwa wakati”.
Mable Azairwegye, mgonjwa mwingine katika Taasis ya IDI, ambaye pia anaishi na VVU na kisukari, anasema anafurahishwa na huduma anazopata katika taasisi hiyo. "Mazungumzo ninayofanya na daktari anaponisindikiza kwenye chumba cha mashauriano hunifanya nijisikie vizuri. Najihisi kukubalika na kuheshimiwa,".
Mojawapo ya vipengele vya mkakati huo wa magonjwa yasioambukiza na VVU ni uwezo wa kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza ambayo ni ya kawaida miongoni mwa watu wanaoishi na virusi vya ukimwi.
Zaidi ya vituo 1800 vya VVU nchini kote vina watoa huduma wenye uwezo wa kupima na kudhibiti saratani ya shingo ya kizazi, kisukari na shinikizo la damu.
"Udhibiti wa magonjwa yasiyoambukiza miongoni mwa watu walio na VVU, kwa kutumia miongozo na zana za Shirika la WHO, umechangia matokeo ya kushangaza. Nchi imepunguza vifo miongoni mwa watu wanaoishi na virusi vya ukimwi kwa karibu theluthi moja tangu mwaka wa 2017 hadi sasa.
Baada ya kufika kwenye dawati la daktari, Byaruhanga anachunguzwa kwa kina. Kwa kutumia nyundo ya patellar, ambayo hujaribu kupia uwezo wa nenva kwa kina, Dkt. Owarwo hukagua utendakazi wa mishipa yake ili kuhakikisha kwamba hapati kupoteza hisia, mojawapo ya matatizo ya ugonjwa wa kisukari.
Sukari kwenye damu isiyodhibitiwa kwa muda mrefu huharibu mishipa ya fahamu na kudhoofisha utendaji kazi wake, hivyo kusababisha matatizo ya kiafya kuanzia kufa ganzi kidogo hadi maumivu ambayo hufanya iwe vigumu kufanya shughuli za kawaida. Kwa hivyo anasema kuwa "Wakati wa mashauriano yangu, Dkt. Owarwo ananielezea jinsi ya kudhibiti utendaji kazi wangu wa neva na kuagiza lishe ninayotakiwa ili kubaki na afya," anasema Byaruhanga.
Baada ya mashauriano yake, Byaruhanga anapokea dawa yake, bila malipo, ambayo atatumia kwa muda wa miezi mitatu hadi atakaposhauriwa tena. "Tangu mwaka wa 2019 nimekuwa nikipokea dawa za virusi vya ukimwi na kisukari pamoja, bila usumbufu, na sijawahi kulazwa hospitalini," anasema.
Afya njema inamaanisha kwamba Byaruhanga anaweza kuendelea kutimiza mapenzi yake kama mwalimu rika katika kituo cha afya kilicho karibu, ambapo anawahimiza wenzake kuzingatia matibabu yao ya VVU. Pia alianzisha kikundi cha maigizo kiitwacho "Karibobo" katika taasisi hiyo ambapo wenzake wanasaidiana kupitia ngoma, mashairi na maigizo.
Miongoni mwa changamoto katika utekelezaji wa mkakati huo ni kuhakikisha upatikanaji wa dawa na elimu ya mara kwa mara juu ya magonjwa sugu ili kuhamasisha watu kufanyiwa uchunguzi, kuzingatia matibabu, kupunguza unyanyapaa na kuwa na maisha bora.
Dkt. Hafisa Kasule, afisa wa kiufundi wa Shirika la WHO anayehusika na magonjwa yasiyoambukiza anasema, "masomo yaliyopatikana katika utekelezaji wa mkakati huu yanapaswa kuongezwa ili kujumuisha kila mtu na uwekezaji endelevu ni muhimu. Shirika la WHO liko tayari kuunga mkono mchakato huu,”