Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sajenti Renita Rismayanti kutoka Indonesia ashinda tuzo ya polisi wa mwaka

Sajenti wa Polisi Renita Rismayanti Raia wa Indonesia, ambaye anahudumu katika ujumbe wa Umoja wa Matifa nchini CAR MINUSCA ni mshindi wa mwaka 2023 wa Tuzo ya Afisa wa Polisi Mwanamke wa Mwaka.
© Herve Serefio
Sajenti wa Polisi Renita Rismayanti Raia wa Indonesia, ambaye anahudumu katika ujumbe wa Umoja wa Matifa nchini CAR MINUSCA ni mshindi wa mwaka 2023 wa Tuzo ya Afisa wa Polisi Mwanamke wa Mwaka.

Sajenti Renita Rismayanti kutoka Indonesia ashinda tuzo ya polisi wa mwaka

Masuala ya UM

Sajenti wa Polisi Renita Rismayanti Raia wa Indonesia, ambaye anahudumu katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati MINUSCA, ametangazwa kuwa mshindi wa mwaka huu wa Tuzo ya Afisa wa Polisi Mwanamke wa Mwaka.

Sajenti huyo akiwa na umri wa miaka 27, ndiye Afisa wa Polisi Mwanamke wa Mwaka wa Umoja wa Mataifa mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kutokea tuzo hiyo ambayo atakabidhiwa katika hafla maalum kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani siku ya Jumatano tarehe 15 Novemba 2023 kwenye maadhimisho ya mwaka ya Wiki ya Polisi ya Umoja wa Mataifa iliyoanza leo tarehe 13 mpaka tarehe 17 Novemba, 2023.

Sajenti Rismayanti anafanya kazi kama Afisa Hifadhidata za Uhalifu wa MINUSCA na katika majukumu yake amesaidia kufikiria na kuunda hifadhidata muhimu inayowawezesha Polisi wa Umoja wa Mataifa kupanga na kuchambua maeneo yenye uhalifu na machafuko.

Kupitia jukumu hili amefanikiwa kusaidia vikosi vya usalama vya nchi kupanga vyema shughuli zao ili kusaidia raia wa ndani.

‘Mchango mkubwa’

Mkuu wa Operesheni za Amani za Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix amesema ubunifu na juhudi za Sajenti huyo kuongeza data ndani ya ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa na polisi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati zimetoa mchango mkubwa katika kuimarisha usalama kwa jamii zilizo hatarini, wakiwemo wanawake na wasichana. 

“Anatumika kama mfano mzuri wa jinsi ushiriki na uongozi wa wanawake katika ulinzi wa amani unaboresha ufanisi wa kazi yetu ya ulinzi na kujenga amani ili kukabiliana vyema na changamoto za leo na kesho." Amesema Lacroix

Sajenti wa Polisi Renita Rismayanti Raia wa Indonesia, ambaye anahudumu katika ujumbe wa Umoja wa Matifa nchini CAR MINUSCA ni mshindi wa mwaka 2023 wa Tuzo ya Afisa wa Polisi Mwanamke wa Mwaka.
© Herve Serefio
Sajenti wa Polisi Renita Rismayanti Raia wa Indonesia, ambaye anahudumu katika ujumbe wa Umoja wa Matifa nchini CAR MINUSCA ni mshindi wa mwaka 2023 wa Tuzo ya Afisa wa Polisi Mwanamke wa Mwaka.

Mara baada ya kupokea taarifa ya kushinda tuzo hiyo Sajenti Rismayanti ameeleza kujisikia mwenye bahati kuweza kutumia ujuzi wake wa kiteknolojia kwa manufaa ya wale ambao MINUSCA iko pale kuwahudumia.

Sajenti Rismayanti amesema “Natumai kutangazwa huku kwa Ushindi wangu wa tuzo hii kutaimarisha miongoni mwa wanawake na wasichana kwamba nyanja zote za utaalamu katika polisi ziko wazi kwetu."

Mshindi huyu alianza kazi yake na Polisi wa Kitaifa wa Indonesia kama afisa habari wa umma mwaka 2014 na pia amefanya kazi katika mafunzo, usimamizi, na usafirishaji.

Kutengeneza njia

“Baada ya kufanikiwa sana kwa kukumbatia teknolojia katika nyanja ya kitamaduni inayotawaliwa na wanaume, Sajenti wa Polisi Rismayanti anawakilisha mustakabali wa polisi wa Umoja wa Mataifa,” alisema Mshauri wa Polisi wa Umoja wa Mataifa Faisal Shahkar.

Aliongeza kuwa “Yeye na wenzake wanasaidia kujenga uaminifu na imani kati ya mamlaka za mitaa na jumuiya, ambayo inafanya kazi yetu kuwa na ufanisi zaidi na watu salama.”

Tuzo ya Afisa wa Polisi Mwanamke wa Mwaka wa Umoja wa Mataifa ilianzishwa mwaka 2011 ili kutambua mchango wa kipekee wa maafisa wa polisi wanawake katika operesheni za amani za Umoja wa Mataifa na kukuza uwezeshaji wa wanawake.

MINUSCA ilianzishwa chini ya mamlaka ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi Aprili 2014 ili kusaidia kukomesha ghasia za wenyewe kwa wenyewe ambazo ziliibuka mwaka mmoja kabla wakati wanamgambo wengi wa Kiislamu walipomuondoa madarakani Rais wa wakati huo, na kusababisha kulipizwa kisasi kutoka kwa wanamgambo wengi wa Kikristo.

MINUSCA ina wafanyakazi chini ya 18,000 wakiwemo zaidi ya wafanyakazi 16,300 wanajeshi na Polisi ambao karibu 2,415 wanahudumu kama maafisa wa polisi. MUNISCA kumekuwa na vifo vya zaidi ya watu 160.