Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maisha ya watoto yanaendelea kupotea Gaza huku hali ya kukata tamaa ikitawala: UN

(Maktaba) Mtoto akilia wakati mhudumu wa afya akimsogelea kutibu jeraha lake, Ni katika hospitali ya Al-Shifa mjini Gaza
UNICEF/Eyad El Baba
(Maktaba) Mtoto akilia wakati mhudumu wa afya akimsogelea kutibu jeraha lake, Ni katika hospitali ya Al-Shifa mjini Gaza

Maisha ya watoto yanaendelea kupotea Gaza huku hali ya kukata tamaa ikitawala: UN

Afya

Hali hatika hospitali za Gaza ni mbaya sana wagonjwa wakiendelea kupoteza maisha wakiwemo watoto njiti katika hospitali ya Al-Shifa ambayo kwa siku ya tatu mfululizo hakuna umeme huku mashambulizi ya Israel yakiongezeka, umesema Umoja wa Mataifa ambao leo unawaomboleza pia wafanyakazi wake 101 waliopoteza maisha katika mzozo huo na kusisitiza kwamba usitishwaji uhasama ni lazima sasa kuliko wakati mwingine wowote. 

Mashirika yote ya Umoja wa Mataifa yaliyotoa tarifa leo yamerejea wito wa kusitisha machafuko kwani hali inazidi kuwa mbaya zaidi kila uchao, lile la afya duniani WHO limesema watoto sita sita wamefariki dunia leo katika hospitali ya Al-shifa na wengine 37 njiti walilazimika kuhamishiwa katika chumba cha upasuaji mwishoni mwa wiki bila machine zao za kuwapasha joto wakati wahudumu wa afya wakihaha kupasha chumba joto kutokana na ukosefu wa umeme. 

Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus amesisitiza kwamba “Dunia haiwezi kunyamaza kimya wakati hospitali ambazo zinapaswa kuwa mahala salama zimegeuzwa kuwa vituo vya vifo, madhila na kukata tamaa” akirejea wito wa kusitisha uhasama mara moja.

Ameongeza kuwa Al-Shifa ndio kitovu cha mapigano ya silaha katika mji wa Gaza kufuatia madai ya jeshi la Israel kwamba Hamas imejenga kituo chake chini ya hospitali hiyo. Madai hayo yamekanushwa na wataalamu wa matibabu wanaofanya kazi hapo.

Sherehe ya kuteremsha bendera ya UNRWA nusu mlingoti katika Ofisi ya UNRWA Lebanon huko Beirut.
© UNRWA/Fadi El Tayyar
Sherehe ya kuteremsha bendera ya UNRWA nusu mlingoti katika Ofisi ya UNRWA Lebanon huko Beirut.

Umoja wa Mataifa unaomboleza

Wakati huo huo leo bendera ya Umoja wa Mataifa inapepea nusu mlingoti katika ofisi za Shirika hilo duniani kote kuwakumbuka wafanyakazi 101 wa shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, waliouawa Gaza tangu kuanza kwa mashambulizi ya Israel kulipiza kisasi mauaji yaliyofanywa na  Hamas kusini mwa Israeli Oktoba 7.

Hadi sasa zaidi ya watu 11,000 wamepoteza maisha Gaza tangu kuanza kwa mzozo wakiwemo hao wafanyakazi 101 wa UNRWA ambao leo wanaombolezwa ikiwemo hapa makao makuu jijini New York Marekani.

Wakuu wa mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa wametoa kauli zao akiwemo mkuu wa shirika la kuhudumia watoto UNICEF Cindy McCain ambaye amesema “Leo tunaungana na jumuiya ya kimataifa katika wakati wa ukimya kuwakumbuka na kuwaeznzi wafanyakazi wenzetu waliouawa huko Gaza” naye mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa Geneva Tatiana Valovaya amewashukuru wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa huko Gaza kwa kujitolea kwao akiainisha umuhimu wa kazi yao wakati huu mshikamano wa kimataifa ukiwa katika tishio kubwa.

Katibu Mkuu António Guterres akiongoza dakika 1 ya ukimya katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York kuwakumbuka wenzake waliouawa huko Gaza.
UN Photo/Eskinder Debebe
Katibu Mkuu António Guterres akiongoza dakika 1 ya ukimya katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York kuwakumbuka wenzake waliouawa huko Gaza.

Nyumba ya wageni ya UN yashambuliwa

Gaza kwa mujibu wa kamishina mkuu wa UNRWA Philippe Lazzarini mashambulizi yanaendelea na jumapili nyumba ya wageni ya UNRWA iliyoko Rafah imeharibiwa na kombora la jeshoi la majini la Israel ingawa hakuna aliyejeruhiwa.

Amesema hii inadhihirisha jinsi gani sheria za kimataifa zinavyokiukwa  na jinamizi wanalopitia watu kila siku kwa kutojali “ulinzi wa raia, miundombinu yao ikiwemo vifaa vya Umoja wa Mataifa, shule, hospitali, makambi ya wakimbizi na maeneo ya kuabudu.”

Wahudumu wa kibinadamu hawapaswi kulengwa

Haijalishi ni wapi mizozo itatokea, Umoja wa Mataifa umesisitiza kuwa wahudumu wa kibinadamu hawapaswi kamwe kulengwa, na kwamba hospitali na wahudumu wa afya wanalindwa mahsusi chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA, imesema pamoja na watoto wachanga waliofariki dunia, wagonjwa wengine 10 wamefariki katika hospital ya Al-Shifa, huku wauguzi watatu wakiuawa wakati kukiwa na mashambulizi ya mabomu na mapigano ya silaha yanayoendelea. 

Miundombinu muhimu, ikiwa ni pamoja na kituo cha oksijeni, matangi ya maji na kisima, kituo cha magonjwa ya moyo na mishipa na wodi ya uzazi, vimeharibiwa.

Wakati wakimbizi wengi wa ndani ambao walikuwa wakihifadhiwa katika hospitali hiyo na baadhi ya wafanyakazi na wagonjwa wameweza kukimbia, "wengine wamekwama ndani, wakiogopa kuondoka au hawawezi kimwili kufanya hivyo", OCHA imesema. 

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari Jumatatu asubuhi, maelfu ya watu bado wanaweza kuwa ndani ya jengo hilo.

Mashambulizi mengine kwenye vituo vya afya yameripotiwa mwishoni mwa juma. OCHA imesema siku ya Jumamosi shambulizi la anga liliripotiwa kugonga na kuharibu zahanati ya Uswidi katika kambi ya Ash Shati, magharibi mwa mji wa Gaza, ambapo takriban watu 500 waliokimbia makazi yao walikuwa wakihifadhiwa.

Jumamosi usiku shambulio lingine la anga lilipiga hospitali ya Al Mahdi katika mji wa Gaza, na kuripotiwa kuwaua madaktari wawili na kuwajeruhi wengine.

Mahmoud, Mpalestina aliyejeruhiwa katika Hospitali ya Al-Shifa huko Gaza.
UN News/Reem Abaza
Mahmoud, Mpalestina aliyejeruhiwa katika Hospitali ya Al-Shifa huko Gaza.

Watu wanahaha kuishi

OCHA imesema Jumapili, kwa siku ya pili mfululizo, kufuatia kuporomoka kwa huduma na mawasiliano katika hospitali kaskazini mwa Gaza, wizara ya afya katika eneo hilo haikusahihisha takwimu za majeruhi.

Taarifa iliyotolewa Ijumaa imeonyesha kuwa watu 11,078 wameuawa katika Ukanda huo tangu tarehe 7 Oktoba. 

Kulingana na vyanzo rasmi vya Israel, wanajeshi 47 wameuawa tangu kuanza kwa operesheni za ardhini.

Mamia ya maelfu ya watu waliosalia kaskazini wanahaha kuishi, OCHA imesema.

Pia unywaji wa maji kutoka vyanzo visivyo salama “Umezua wasiwasi mkubwa kuhusu upungufu wa maji mwilini na magonjwa yanayosambazwa na maji, njaa imekithiri, na shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa WFP limetoa tahadhari juu ya hatari za utapiamlo na njaa.

Makumi ya maelfu ya watu waliokimbia makazi yao mwishoni mwa juma waliendelea kutoroka kaskazini kupitia "upenyo uliofunguliwa na jeshi la Israel lakini maisha yao bado yalikuwa hatarini kusini mwa nchi hiyo kutokana na mashambulizi ya mabomu na makazi yaliyojaa watu. Hakuna sehemu yoyote katika Gaza iliyo salama," amesema Bwana Lazzarini wa UNRWA.