Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua za kimataifa zichukuliwe kukomesha mashambulizi hospitali Gaza: UN

Mtoto mchanga analia akiwa amefunikwa blanketi jeupe. Picha hiyo ni sehemu ya ripoti ya mtengenezaji wa filamu Bisan Ouda kuhusu changamoto za kujifungua huko Gaza.
© UNFPA/Bisan Ouda Mtoto mchanga amezaliwa katika hospitali ya Al Shifa Gaza

Hatua za kimataifa zichukuliwe kukomesha mashambulizi hospitali Gaza: UN

Amani na Usalama

Mashirika ya Umoja wa Mataifa leo yametoa wito wa dharura wa kuchukua hatua za kimataifa kukomesha mashambulizi yanayoendelea dhidi ya hospitali, huku wanajeshi wa Israel wakipambana na wanamgambo wa Kipalestina katikati mwa Ukanda wa Gaza.

Wakurugenzi wa kanda wa shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi UNFPA, wa shirika la kuhudumia watoto UNICEF na shirika la afya duniani WHO, wamesema "wametiwa hofu na ripoti za hivi karibuni ambazo zinaonyesha watu wengi wameuawa ikiwa ni pamoja na watoto katika vituo katika mji wa Gaza na kaskazini mwa maeneo ya Ukanda huo.”

Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Palestina imeripoti kwamba hospitali ya pili kwa ukubwa huko Gaza, Al-Quds, haifanyi kazi kutokana na uhaba wa mafuta huku shirika hilo lisilo la kiserikali likisema kuwa limeweza kuwasiliana na kituo hicho mara kadhaa tu.

Hakuna mawasiliano

WHO imepoteza mawasiliano na watu wake katika hospitali ya Al Shifa, ambayo ni kubwa zaidi huko Gaza, ambapo habari zinazonukuu wizara ya afya, zinasema kuwa wagonjwa watano waliojeruhiwa wamefariki dunia kwa sababu hawakuweza kufanyiwa upasuaji kutokana na ukosefu wa mafuta.

Watoto wawili katika chumba cha wagonjwa mahututi waliripotiwa kufariki dunia jana Jumamosi, huku maji, chakula na umeme vikatika.

Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus ameelezea wasiwasi wake mkubwa juu ya usalama wa wafanyikazi na wagonjwa waliokumbwa kwenye mapigano Jumamosi na kubaini kuwa vifaru vya Israeli viliripotiwa kuzunguka katika hospitali ya Al Shifa.

Jeshi la Israel limekanusha mara kwa mara kuwa vikosi vyake vinalenga hospitali, wakidai kuwa Hamas na wanamgambo wengine wanatumia vituo hivyo kama ngao na makao yao makuu yapo chini ya hospital ya Al Shifa.

"Mashambulizi makali yanayozunguka hospitali kadhaa kaskazini mwa Gaza yanazuia ufikiaji salama kwa wahudumu wa afya, waliojeruhiwa na wagonjwa wengine", ilisema taarifa iliyotolewa kwa pamoja na Laila Baker wa UNFPA, Mkurugenzi wa kikanda wa UNICEF Adele Khodr, na Dkt. Ahmed Al-Mandhari, wa WHO.

Watoto wanakufa

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya pamoja "Watoto wanaozaliwa kabla ya wakati na wanaozaliwa kwa msaada wa vifaa vya kuokoa maisha wanaripotiwa kufa kutokana na ukosefu wa umeme, oksijeni, na kukatika kwa maji katika Hospitali ya Al-Shifa, wakati wengine wako hatarini. “

Wafanyikazi katika hospitali kadhaa wanaripoti ukosefu wa mafuta, maji na vifaa vya msingi vya matibabu, na hivyo kuweka maisha ya wagonjwa wote hatarini mara moja.

Katika siku 36 zilizopita, WHO imerekodi angalau mashambulizi 137 dhidi ya huduma ya afya huko Gaza, na kusababisha vifo vya watu 521 na majeruhi 686, ikiwa ni pamoja na vifo 16 na majeruhi 38 vya wahudumu wa afya, wakurugenzi hao wa kanda wamesema.

Ulimwengu hauwezi kukaa kimya wakati hospitali ambazo zinapaswa kuwa kimbilio salama, zinabadilishwa kuwa matukio ya kifo, uharibifu na kukata tamaa.

Mashambulizi dhidi ya vituo vya matibabu na raia hayakubaliki na ni ukiukaji wa sheria za kimataifa, wamesisitiza.

Madaktari bingwa wa upasuaji waliovaa vitambaa vya bluu wakimfanyia upasuaji mgonjwa katika chumba cha upasuaji katika hospitali ya Al-Quds huko Gaza.
© WHO Mgonjwa akipatiwa huduma katika chumba cha upasuaji kwenye hospitali ya Al-Quds Gaza

Haki ya msaada wa matibabu

Taarifa yao imesema “Mashambulizi hayo hayawezi kusamehewa. Haki ya kutafuta msaada wa matibabu, haswa wakati wa shida, haipaswi kunyimwa kamwe".

Zaidi ya nusu ya hospitali katika Ukanda wa Gaza zimefungwa huku zile zilizosalia zinakabiliwa na shinikizo kubwa.

Uhaba wa maji, chakula, na mafuta pia unatishia ustawi wa maelfu ya watu waliokimbia makazi yao, ikiwa ni pamoja na wanawake na watoto, ambao wanapata hifadhi katika hospitali.

Vifo na kukata tamaa

Taarifa hiyo ya Pamoja imesisitiza kuwa "Ulimwengu hauwezi kunyamaza kimya wakati hospitali, ambazo zinapaswa kuwa mahali salama, zinabadilishwa kuwa matukio ya kifo, uharibifu, na kukata tamaa. Hatua madhubuti za kimataifa zinahitajika sasa ili kupata usitishaji mapigano wa haraka wa kibinadamu, kuzuia upotezaji zaidi wa maisha, na kuhifadhi kile kilichosalia cha mfumo wa huduma ya afya huko Gaza".

Wameongeza kuwa “Upatikanaji na uingizaji wa misaada usiozuiliwa, salama na endelevu unahitajika sasa ili kufikisha mafuta, vifaa tiba na maji kwa ajili ya huduma hizi za kuokoa maisha. Vurugu hizo lazima ziishe sasa.”

Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu katika eneo la Palestina linalokaliwa, Lynn Hastings, ameonya kwamba “mafuta sio tu kwamba yanahatarisha maisha ya watu hospitalini, lakini pampu za maji, mitambo ya kuondoa chumvi na vituo vya kusafisha maji machafu vyote vimesimama."

Ameandika kwenye ukurasa wake wa X zamani Twitter kwamba majanga ya afya ya umma yanaibuka na operesheni za kibinadamu ndizo zitakazofuata.