Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa ufupi:

Mashambulizi ya makombora kutoka angani yamesababisha uharibifu mkubwa kwenye mji wa kusini wa Rafah ulioko Ukanda wa Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa na Israel
© UNICEF/Eyad El Baba
Mashambulizi ya makombora kutoka angani yamesababisha uharibifu mkubwa kwenye mji wa kusini wa Rafah ulioko Ukanda wa Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa na Israel

Habari kwa ufupi:

Amani na Usalama

Mkutano wa kimataifa  kuhusu Gaza wafanyika jijini Paris Ufaransa, FAO inakabiliana na changamoto ya El Niño kwa wakulima na WHO kujenga mifumo ya afya yenye mnepo

Mkutano wa kimataifa kuhusu Gaza mjini Paris

Kufuatia athari za mzozo unaoendelea huko Mashariki ya Kati  leo serikali ya Ufanransa leo imeamua kuitisha mkutano wa kimataifa wa masuala ya kibinadamu kwa ajili ya Gaza unaofanyika mjini Paris ambao lengo lake ni kuomba usitishwaji wa uhasama kwa minajili ya kibinadamu, kutanabaisha wasiwasi juu ya usalama wa raia ambao wamekimbilia Gaza Kusini na kuzungumzia Waisrael 240 ambao bado wanashukiliwa matena na Hamas tangu Oktoba 7. 

Umoja wa Mataifa unawakilishwa na Martin Griffith Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura  wa Umoja huo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametuma ujumbe wa video kwenye mkutano huo wa siku moja akisema” Ni lazima tujitokeze kusaidia na kuwalinda raia huko Gaza. Hiyo ina maana ya usitishaji mapigano wa kibinadamu haraka. Inamaanisha kuhakikisha heshima kamili ya sheria za kimataifa za kibinadamu. Inamaanisha kulinda hospitali, vifaa vya Umoja wa Mataifa, makazi, na shule. Inamaanisha ufikishaji usio na vizuizi, salama, na endelevu wa kuleta na kusambaza vifaa kwa kiwango kikubwa  ikijumuisha mafuta. Na inamaanisha kuwekeza katika ombi la kibinadamu la dola bilioni 1.2 ambalo Umoja wa Mataifa umezindua hivi punde kuwasaidia watu wa Gaza. Naomba uungwaji mkono wenu wenu. Sasa ni wakati wa kuchukua hatua madhubuti.”

Ukame unaosababishwa na El Niño huko Ziway Dugda, eneo la Oromia nchini Ethiopia, unaathiri kila familia na hawana chakula cha kutosha nyumbani cha kujilisha.
OCHA/Charlotte Cans
Ukame unaosababishwa na El Niño huko Ziway Dugda, eneo la Oromia nchini Ethiopia, unaathiri kila familia na hawana chakula cha kutosha nyumbani cha kujilisha.

FAO kuwalinda wakulima dhidi ya  El Niño

Wakati hivi sasa kukiwa na tishio kubwa la El Niño inayotarajiwa kuathiri mamilioni ya watu shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO leo limezindua hatua mpya za matarajio na mpango wa kukabiliana na athari hizo zinazotarajiwa katika Maisha ya wakulima na uhakika wa chakula hususan kwa watu walio hatarini Zaidi. 

Mpango huo unahitaji dola milioni 160 kusaidia watu Zaidi ya milioni 4.8 katika nchi 34 hadi March 2024

Mtoto akipatiwa chanjo katika kituo cha afya cha Dar Sa’ad  Aden
© UNICEF/UN0679318/Hayyan
Mtoto akipatiwa chanjo katika kituo cha afya cha Dar Sa’ad Aden

Mifumo ya afya na mabadiliko ya tabianchi

Katia kukabiliana na chanamoto za mabadiliko ya tabianchi zinazotokea mara kwa mara kote duniani , leo shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO limezindua mkakati mpya wa kujenga mifumo ya afya yenye mnepo na inayozalisha kiwango kidogo cha hewa ukaa.

Lengo kubwa la mkakati huo mpya ni  lengo kuzilinda jamii dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, kuimarisha mifumo ya afya na kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.