Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake ni muhimu katika mstakabali bora wa Somalia

(Picha ya Maktaba) Catriona Laing, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Somalia akitoa maelezo kwa Baraza la Usalama.
UN Photo/Eskinder Debebe
(Picha ya Maktaba) Catriona Laing, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Somalia akitoa maelezo kwa Baraza la Usalama.

Wanawake ni muhimu katika mstakabali bora wa Somalia

Wanawake

Catriona Laing, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo (UNSOM) amethibitisha kuwa Umoja wa Mataifa unashirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Maendeleo ya Wanawake na Haki za Binadamu nchini humo kuhakikisha kwamba sauti za wanawake zinasikika katika Baraza la Ushauri la Taifa (NCC) ambalo kwa sasa linaundwa na wanaume pekee akiwemo Rais wa shirikisho, marais wa majimbo na viongozi wengine wanaume wa ngazi ya juu ya uongozi.

"Baraza la Ushauri la Taifa, bila uwakilishi wa wanawake kwa kweli haliwezi kuonekana kushughulikia masula ya nchi. Kwa hivyo, lazima tuhakikishe sauti ya wanawake inasikika katika jukwaa hilo kuu – NCC.” Anasema Laing.

Aidha kiongozi mwakilishi hiyo wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia ametoa wito wa kutumia mapitio ya katiba yanayoendelea kuhamasisha kupitishwa kisheria kwa asilimia 30 ya mgawo wa wanawake katika Bunge la kitaifa, "Kuhusu asilimia 30, hii lazima iwekwe kisheria. Ni vyema kuwa na dhamira, lakini bila dhamira kisheria, tunajua kutokana na uzoefu katika nchi nyingine kwamba ni vigumu sana kusonga mbele. Nchi barani Afrika ambazo zimefanya vyema zaidi zimefanya nafasi hizi za viti maalumu kulindwa na sheria.”