Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan: Wanamgambo waasi wa RSF wahusishwa na ukatili wa kupindukia

Baadhi ya familia jimboni Darfur nchini Sudan zimefurushwa makwao mara kadhaa kutokana na mapigano yanayoendelea nchini mwao
WFP/Abdulaziz Abdulmomin
Baadhi ya familia jimboni Darfur nchini Sudan zimefurushwa makwao mara kadhaa kutokana na mapigano yanayoendelea nchini mwao

Sudan: Wanamgambo waasi wa RSF wahusishwa na ukatili wa kupindukia

Haki za binadamu
  • Utekaji wa wasichana na wanawake
  • Wanawake na wasichana wanafungwa minyororo
  • Matukio 50 ya unyanyasaji wa kingono

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR) imesikitishwa sana na ripoti kwamba huko Darfur nchini Sudan wanawake na wasichana wanatekwa nyara na kushikiliwa katika mazingira ya kinyama katika maeneo yanayodhibitiwa na wanamgambo waasi (RSF). 

Msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Liz Throssell (Elizabeth Throssel) hii leo Ijumaa asubuhi saa za Geneva, Uswisi akizungumza na waandishi wa habari anasema, “habari za kuaminika kutoka kwa walionusurika, mashahidi na vyanzo vingine vinaeleza kwamba zaidi ya wanawake na wasichana 20 wametekwa, lakini idadi inaweza kuwa ni kubwa zaidi ya hiyo iliyotajwa.” 

Wanawake na wasichana wanafungwa minyororo kwenye magari

Bi. Throssel anaendelea kueleza kuwa vyanzo vingine vimeripoti kuwaona wanawake na wasichana wakiwa kwenye minyororo kwenye magari ya kubebea mizigo na magari madogo. 

Taarifa hizi za kushtua zinakuja huku kukiwa na ongezeko la visa vya unyanyasaji wa kingono nchini humo tangu mapigano yazuke kati ya Jeshi la Sudan na Vikosi hivyo vya wanamgambo wa RSF miezi sita iliyopita. 

Kwa mujibu wa takwimu walizonazo, Msemaji huyo wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, anasema, “takribani watu 105 wamefanyiwa ukatili wa kingono tangu uhasama huo uanze tarehe 15 Aprili 2023.” Wanawake wanatekwa, wanalazimishwa kuolewa na kushikiliwa huku watekaji wakidai kikombozi. 

Matukio 50 ya unyanyasaji wa kingono

Kufikia tarehe 2 Novemba, Ofisi ya Haki za Kibinadamu nchini Sudan ilikuwa imepokea ripoti za kuaminika za zaidi ya matukio 50 ya unyanyasaji wa kingono yanayohusishwa na uhasama, na kuathiri takribani watu 105 - wanawake 86, mwanamume mmoja na watoto 18. Matukio 23 kati ya hayo yalihusisha ubakaji, 26 yalikuwa ya ubakaji unaotekelezwa na watu wengi yaani genge na matatu ya kujaribu kubaka. 

SAF, RSF na makundi mengine acheni ukatili na unyanyasaji

Ofisi hiyo ya haki za binadamu imelaani vikali vitendo hivyo na kuwataka viongozi wa juu wa Jeshi la Sudan na wa Vikosi vya wanamgambo waasi wa RSF pamoja makundi mengine yenye kujihami kwa silaha ambayo yana uhusiano na pande hizi mbili kuchukua hatua za haraka kukomesha unyanyasaji wa kingono ikiwa ni pamoja na kuwaachia huru waliotekwa nyara, kuwapatia huduma ya matibabu na kisaikolojia na kuwafikisha katika mikono ya sheria wahusika wa matukio haya mabaya ya kikatili.