Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bangladesh: Watu 11 wauawa kwenye maandamano, UN yalaani

Dhaka, mji mkuu wa Bangladesh.
© Unsplash/Niloy Biswas
Dhaka, mji mkuu wa Bangladesh.

Bangladesh: Watu 11 wauawa kwenye maandamano, UN yalaani

Amani na Usalama

Ofisi ya Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu, OHCHR imelaani mauaji na matukio ya ghasia kwenye maandamano yanayoendelea nchini Bangladesh wakati huu ambapo nchi hiyo inajiandaa kulekea kwenye uchaguzi mkuu. 

Msemaji wa OHCHR mjini Geneva, Uswisi Ravina Shamdasani amewaambia waandishi wa habari hii leo kuwa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu wanasiasa wote waweke wazi kuwa kuwa ghasia za hizo hazikubaliki na waepuke kauli au vitendo vyovyote vinavyoweza kuchochea vurugu.   

Kwa mujibu wa Bi. Shamdasan, hadi kufikia leo asubuhi, takriban watu 11 wamefariki kutokana na maandamano hayo katika maeneo mengi ya nchi. Miongoni mwa waliofariki ni polisi wawili, wafanyakazi sita wa chama cha upinzani na wapita njia wawili.  

Wapinzani washambuliwa na wanaodaiwa kuwa wafuasi wa chama tawala  

Zaidi ya hayo, OHCHR inasema, tarehe 28 Oktoba, waandamanaji wa upinzani walidaiwa kushambulia makazi ya Jaji Mkuu na majaji wengine, na takriban wanahabari 30 walishambuliwa na waandamanaji na watu waliojifunika nyuso zao wakiwa wamepanda pikipiki waliodhaniwa kuwa wafuasi wa chama tawala.   

Katika kujibu maandamano hayo, polisi wameripotiwa kuwashambulia waandamanaji kwa fimbo, marungu, risasi za mpira na mabomu ya sauti. Pia wamevamia nyumba za wanaharakati wa upinzani kote nchini, wakiwakamata na kuwaweka kizuizini mamia, wakiwemo wanafamilia wa wanaharakati hao.  

Nguvu itumike pale inapobidi na kwa kiasi   

“Tunawaomba polisi wahakikishe kwamba nguvu inatumika tu pale inapobidi na, ikiwa ni hivyo, kwa kufuata kikamilifu kanuni za uhalali, tahadhari na uwiano,” amesema Bi. Shamdasani.   

OHCR inasema mnamo tarehe 30 Oktoba, mkuu wa chama cha upinzani cha BNP, Mirza Fakhrul Islam Alamgir, alikamatwa na kufunguliwa mashtaka chini ya Sheria ya Vilipuzi kuhusiana na madai ya shambulio la uchomaji moto kwenye makazi ya Jaji Mkuu. Bado yuko kizuizini huku viongozi wengine kadhaa wakuu wa upinzani wakiripotiwa kujificha kwa hofu ya kukamatwa.   

Kwa hivyo Bi. Shamdasani anasema "tunaiomba serikali ijizuie kwa kiasi kikubwa inapokabili mivutano ya kisiasa wakati huu muhimu, na kuchukua hatua ili kuhakikisha kuwa haki za binadamu zinazingatiwa kikamilifu, kwa wananchi wote wa Bangladesh, kabla, wakati na baada ya uchaguzi".