Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gaza: Maelfu wanavamia maghala ya Umoja wa Mataifa; ishara ya kukata tamaa baada ya mashambulizi ya wiki kadhaa

Mfanyakazi wa WFP akipakua misaada ya chakula ambacho kiko tayari kuliwa kutoka kwenye lori kribu na Alexandria Misri tayari kukiingiza Gaza chakula hicho
© WFP/Amira Moussa
Mfanyakazi wa WFP akipakua misaada ya chakula ambacho kiko tayari kuliwa kutoka kwenye lori kribu na Alexandria Misri tayari kukiingiza Gaza chakula hicho

Gaza: Maelfu wanavamia maghala ya Umoja wa Mataifa; ishara ya kukata tamaa baada ya mashambulizi ya wiki kadhaa

Msaada wa Kibinadamu

Mashirika ya misaada yameonya hii leo kwamba utaratibu wa kiraia unaanza kuvunjika huko Gaza baada ya maelfu ya watu waliokata tamaa kuvamia maghala yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa na vituo vingine vya usambazaji wa misaada katika eneo lililoharibiwa, wakichukua unga wa ngano, vifaa vya usafi na bidhaa nyingine muhimu za kujiokoa.

Tweet URL

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ni miongoni mwa mashirika ya kibinadamu ambayo yameripoti matukio hayo, ambayo yanafuatia kukatika kwa mawasiliano kwa saa 24 na changamoto nyingine zinazoendelea katika Ukanda wa Gaza.

Moja ya ghala ambazo iliyovamiwa, huko Deir al-Balah, ni mahali UNRWA huhifadhi misaada nayopokea kutoka kwenye misafara yenye misaada ya kibinadamu inayotoka Misri.

WFP vile vile iliripoti kuwa ghala lilikuwa na tani 80 za chakula mchanganyiko, hasa chakula cha makopo, unga wa ngano na mafuta ya alizeti, vyote vikiwa vimehifadhiwa hapo kabla ya kusambazwa kwa familia zilizo lazimika kuyakimbia makazi yao. 

 

'Watu wanaogopa na wamekata tamaa'

"Hii ni ishara inayotia wasiwasi kwamba utulivu wa kiraia unaanza kuvunjika baada ya wiki tatu za vita na mashambulizi makali huko Gaza," alisema Mkurugenzi wa Masuala ya UNRWA katika Ukanda wa Gaza, Thomas White, ambaye aliongeza: "Watu wana hofu, wamechanganyikiwa na kukata tamaa”.

Aliendelea kusema kuwa hali ya wasiwasi na hofu ilizidishwa na kukatwa kwa mawasiliano ya simu na laini za mawasiliano ya mtandao.

"Wanahisi kuwa wako peke yao, wametengwa na familia zao ndani ya Gaza na dunia nzima," alisema Bw. White, ambaye alibainisha kuwa kitendo cha kuhama kwa watu wengi kutoka kaskazini mwa Ukanda wa Gaza kuelekea kusini kumeweka shinikizo kubwa kwa jamii hizo, na kuongeza mzigo zaidi katika kuporomoka kwa huduma za umma.

Baadhi ya familia zimewapokea hadi jamaa 50 ambao wamepata hifadhi katika nyumba moja.

"Manunuzi sokoni yanaisha huku msaada wa kibinadamu unaokuja katika Ukanda wa Gaza kwa malori kutoka Misri hautoshi. Mahitaji ya jumuiya ni makubwa, ikiwa tu kwa ajili ya kujikimu kwa maisha ya kimsingi, wakati misaada tunayopokea ni kidogo na haiendani,” aliongeza Bw. White.

 

Tweet URL

Mfumo wa msafara unaelekea kushindwa

Afisa huyo wa UNRWA aliripoti kuwa hadi sasa, ni takriban malori 80 ya msaada yaliingia Gaza ndani ya wiki moja.

Jumamosi, Oktoba 28, hakukuwa na msafara kutokana na kukatika kwa mawasiliano. UNRWA, ambayo ni mhusika mkuu wa upokeaji na uhifadhi wa misaada katika Ukanda wa Gaza, haikuweza kuwasiliana na pande mbalimbali za kuratibu upitishaji wa msafara huo.

"Mfumo wa sasa wa misafara unaelekea kushindwa," alisema Bw. White, akifafanua kuwa malori machache sana, taratibu za polepole, ukaguzi mkali, vifaa ambavyo havilingani na mahitaji ya UNRWA na mashirika mengine ya misaada, na zaidi ni marufuku inayoendelea ya mafuta, "yote ni kichocheo cha kuwa na mfumo utakaoshindwa."

"Tunatoa wito wa usafirishaji wa mara kwa mara na usambazaji wa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza ili kukabiliana na mahitaji hasa wakati huu ambapo mvutano na masikitiko yanaongezeka," alihitimisha.

Wakati huo huo, timu za UNRWA huko Gaza zimeripoti kuwa huduma za mtandao na miunganisho zilirejeshwa, na watatathmini upya hali hiyo kwa lengo la kuanzisha tena misafara na usambazaji wa misaada.

 

Misaada isichuruzike itiririke

Samer Abdeljaber ni Mwakilishi wa WFP na Mwakilishi Mkazi nchini Palestina, alitoa ombi saw ana lililotolewa na UNRWA akisema "Tunahitaji kusitishwa mapigano kwa sababu za kibinadamu ili kuweza kuwafikia watu wanaohitaji chakula, maji na mahitaji muhimu kwa usalama na kwa ufanisi. Ufikiaji mwingi zaidi unahitajika haraka, na misaada inatakiwa kuacha kuchuruzika na kuanza kutiririka.

Kuvamia kwa ghala za usambazaji misaada huko Gaza ilikuwa "ishara ya watu kupoteza matumaini na kukata tamaa zaidi kila dakika. Wana njaa, wametengwa, na wamekuwa wakiteseka kwa mashambulizi na taabu nyingi kwa majuma matatu.”

Akiongeza wasiwasi wa jumla, WFP imesema kuwa uhaba wa mafuta na kupotea kwa mawasiliano pia kunatishia kusimamisha shughuli za kibinadamu. Bila misaada ya ziada ya mafuta, mikate inayozalishwa katika maduka ya kuoka mikate yanayolipwa na WFP huko Gaza hayataweza kufanya kazi tena na wasafirishaji hawawezi kutoa chakula inapohitajika.

WFP iliripoti kuwa inapanga kutoa Msaada wa chakula cha kuokoa maisha kwa zaidi ya watu milioni moja ambao wanakabiliwa na njaa sasa na shirika hilo linahitaji usambazaji wa kutosha wa chakula na angalau malori 40 ya yanatakiwa kuvuka kila siku hadi Gaza ili kuweza kukidhi mahitaji yanayoongezeka.

Maombolezo kwa wafanyakazi waliopoteza maisha 

Hii leo, katika mji mkuu wa Jordan, Amman, UNRWA, ikiongozwa na Kamishna Jenerali Philippe Lazzarini, iliandaa hafla ya kumbukumbu yakuwaenzi wafanyakazi wake 59 waliopoteza maisha huko Gaza tangu mzozo huo kuzuka tarehe 7 Oktoba 2023.

“Kila siku inakuwa giza kwa Umoja wa Mataifa na UNRWA huku idadi ya wenzetu wanaouawa ikiongezeka. Mazungumzo ya mateso yasiyoelezeka yanatoka Gaza kila saa,” shirika hilo lilisema.

Wafanyakazi wa UNRWA mjini Amman, Jordan, wanahudhuria hafla ya kuwakumbuka wafanyakazi wenzao waliopoteza maisha huko Gaza.
UNRWA/Shafiq Fahed
Wafanyakazi wa UNRWA mjini Amman, Jordan, wanahudhuria hafla ya kuwakumbuka wafanyakazi wenzao waliopoteza maisha huko Gaza.