Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali huko Gaza 'inakuwa ya kukatisha tamaa kila saa', asema Mkuu wa Umoja wa Mataifa 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia wanahabari mjini Kathmandu, Nepal.
UN Nepal
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia wanahabari mjini Kathmandu, Nepal.

Hali huko Gaza 'inakuwa ya kukatisha tamaa kila saa', asema Mkuu wa Umoja wa Mataifa 

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameanza ziara yake rasmi nchini Nepal kwa kutoa salamu za rambirambi kwa familia za wanafunzi 10 wa Nepal waliouawa katika mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa na Hamas nchini Israel, na kwa mara nyingine tena kutoa wito wa kulindwa kwa raia wote huko Gaza akisema, “hali inakua ya kukatisha tamaa kila saa.”

Ziara ya Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa inakuja wakati mgogoro katika Ukanda wa Gaza ukiingia wiki yake ya tatu kufuatia uvamizi uliofanywa tarehe7 Oktoba 2023 na wapiganaji wa Hamas ndani ya Israel na baadae Israel kutangaza vita.

Mwishoni mwa wiki iliyopita (27 Oktoba 2023) Umoja wa Mataifa ulipitisha azimio la kutaka kusitishwa kwa mapigano kwasababu za kibinadamu, lakini siku chache zilizopita kumeshuhudiwa mashambulizi makubwa ya mabomu na ripoti za operesheni za ardhini zinazofanywa na Israel ndani ya Gaza.

"Ninajua kwamba ingawa mzozo wa Mashariki ya Kati uko umbali wa maelfu ya maili, umepiga karibu sana na nyumbani kwa watu wa Nepal," alisema Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa katika mkutano na waandishi wa habari hii leo jumapili akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Pushpa Kamal Dahal.

Pia akitoa salamu za heri za kurejea salama kwa Bipin Joshi, raia wa Nepal ambaye ametoweka na aliapa ataendelea kusisitiza kuachiliwa huru mara moja na bila masharti kwa mateka wote huko Gaza.

"Na ninarudia kulaani kwangu kabisa mashambulizi ya kutisha yanayofanywa na Hamas. Hakuna uhalali wowote, kwa mauaji, kujeruhi na kutekwa nyara kwa raia," alisema.

Wakati huo huo, Bwana Guterres alibainisha hali mbaya sana ya Gaza na kueleza masikitiko yake kwamba badala ya kustekelezwa kwa sitisho muhimu kwa sababu za kibinadamu azimio lililoungwa mkono na jumuiya ya kimataifa, Israel imezidisha operesheni zake za kijeshi.

"Idadi ya raia ambao wameuawa na kujeruhiwa haikubaliki kabisa. Pande zote lazima ziheshimu wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu ... ambayo iliibuka kutokana na janga na uzoefu mbaya wa vita." 

Akisisitiza wito wake thabiti wa kufuata kikamilifu sheria za kimataifa za kibinadamu, Katibu Mkuu alisema: “Sheria za Vita huweka sheria wazi za kulinda maisha ya binadamu na kuheshimu masuala ya kibinadamu. Sheria hizo haziwezi kubadilishwa kwa ajili ya manufaa.”

Bwana Guterres alisema kuwa huko Gaza zaidi ya watu milioni mbili wasio na mahali popote salama pa kwenda, wananyimwa mahitaji muhimu ya maisha - chakula, maji, malazi na matibabu - huku wakikabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara.

"Ninawasihi wale wote walio na wajuibu kuondoka kutoka ukingoni," alisema akiitaja hali hiyo "janga la kibinadamu."

Katibu Mkuu alisisitiza ombi lake la kusitishwa kwa mapigano mara moja kwa sbabu za kibinadamu, kuachiliwa huru bila masharti kwa mateka wote, na utoaji wa misaada endelevu ya kibinadamu kwa kiwango ambacho kinakidhi mahitaji ya watu wa Gaza.

"Lazima tuunganishe nguvu ili kukomesha jinamizi hili kwa watu wa Gaza, Israel na wale wote walioathirika duniani kote, ikiwa ni pamoja na hapa Nepal," alisema.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kulia) akihutubia wanahabari mjini Kathmandu, akiwa ameambatana na Waziri Mkuu Pushpa Kamal Dahal.
UN Nepal
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kulia) akihutubia wanahabari mjini Kathmandu, akiwa ameambatana na Waziri Mkuu Pushpa Kamal Dahal.

Kujitolea kwa Nepal kwenye ushirikiano wa kimataifa na SDGs

Katibu Mkuu amesifu utamaduni wa muda mrefu wa nchi hiyo iliyoko Himalaya kwa kutetea amani na ushirikiano wa pande nyingi na kuitaka dunia "kuwa rafiki bora wa Nepal", ambayo imekumbwa na machafuko ambayo haijajiletei yenyewe, ikiwa ni pamoja na tishio la machafuko yatokanayo na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Guterres alimshukuru Waziri Mkuu Dahal na kusema kwamba Umoja wa Mataifa unaishukuru sana Nepal kwa uungaji mkono wake kwa masuluhisho ya pande nyingi – pamoja na kuwa iliunga mkono mchango wake mkubwa katika misheni za kulinda amani duniani kote.

Mwanzoni mwa ziara yake ya siku nne nchini humo, mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa pia alisifu "maendeleo ya kustaajabisha" ya Nepal katika miongo miwili iliyopita, kwani imekuwa jamhuri, imeanzisha amani, na kujidhatiti kwenye utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. 

 

'Kuhitimu' kunakaribia

"Na kuna mengi zaidi yajayo," Bwana Guterres aliendelea, akielezea kwamba "miaka michache ijayo itakuwa ya maamuzi, wakati Nepal inajiandaa kuhitimu kutoka hadhi ya Nchi Zenye maendeleo duni."

Katibu Mkuu alikuwa akizungumzia mchakato unaowezeshwa na Umoja wa Mataifa ambapo mataifa yaliyo hatarini zaidi duniani yakishakidhi vigezo (juu ya kipato, mali ya binadamu na udhaifu wa kiuchumi na kimazingira), yanaweza kuchukua hatua za kuelekea 'kuhitimu' inawakilisha hatua muhimu katika njia ya maendeleo ya LDCs.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa aliendelea kubainisha kuwa katika miaka michache Ijayo, Nepal pia itaanza hatua za mwisho za mchakato wa amani: mpito wa kuelekea kwenye haki.

"Mpito kuelekea kwenye haki lazima usaidie kuleta amani kwa waathiriwa, familia na jamii," alisema, akisisitiza kwamba "Umoja wa Mataifa uko tayari kuunga mkono Nepal kuandaa mchakato unaokidhi viwango vya kimataifa, maamuzi ya Mahakama ya Juu, na mahitaji ya waathirika - na kuyatekeleza kwa vitendo.”