Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pande zinazogombana huko Gaza zakumbushwa zina wajibu chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu na sheria za kibinadamu 

Waombolezaji wakihudhuria mazishi ya watu waliofariki kufuatia mashambulizi ya Israel huko Gaza.
WHO
Waombolezaji wakihudhuria mazishi ya watu waliofariki kufuatia mashambulizi ya Israel huko Gaza.

Pande zinazogombana huko Gaza zakumbushwa zina wajibu chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu na sheria za kibinadamu 

Haki za binadamu

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk amezikumbusha pande zote katika mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati kuzingati wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu na sheria ya kimataifa ya haki za binadamu. 

 

Katika taarifa yake aliyoitoa hii leo huko jijini Geneva Uswisi Kamishna Türk ameeleza kuwa mashambulizi ya mabomu ya jana usiku tarehe 27 Oktoba 2023 na operesheni za ardhini huko Gaza yanayotekelezwa na vikosi vya Israeli yaliripotiwa kuwa makali zaidi, na kupeleka mgogoro huu mbaya kwenye kiwango kipya cha vurugu na maumivu. 

“Tunawakumbusha wahusika wote wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu na sheria ya kimataifa ya haki za binadamu.” Amesema Turk 

Kutokana na kuendelea kwa mashambulizi Kamnishn Turk ameeleza kuwa athari za kibinadamu na haki za binadamu zitakuwa mbaya na za kudumu. “Maelfu tayari wamekufa, wengi wao wakiwa watoto. Kwa kuzingatia jinsi operesheni za kijeshi zimekuwa zikiendeshwa hadi sasa, katika muktadha wa uvamizi wa miaka 56, ninatoa angalizo la wasiwasi kuhusu matokeo ya uwezekano wa janga kutokana na operesheni kubwa za ardhini huko Gaza na uwezekano wa maelfu ya raia zaidi kufa.”

Tweet URL

Miundombinu kulipuliwa

Mkuu huyo wa masuala ya haki za binadamu ameeleza kuwa licha ya masahibu yanayo wasibu wakazi wa Gaza “Israel kushambulia kwenye mitambo ya mawasiliano ya simu na kufuatia kwa kuzimwa mtandao kumewaacha Wananchi wa Gaza bila njia ya kujua kinachoendelea katika eneo lote la Gaza na kuwatenga na ulimwengu wa nje.”

 Kulipuliwa kwa miundombinu ya mawasiliano ya simu kunawaweka raia katika hali ya hatari kubwa. Na akataja hatari hizo 

  • Magari ya wagonjwa na timu za ulinzi wa raia haziwezi tena kuwapata waliojeruhiwa, au maelfu ya watu wanaokadiriwa kuwa bado wapo chini ya vifusi. 
  • Raia hawawezi tena kupokea taarifa mpya kuhusu wapi wanaweza kupata usaidizi wa kibinadamu na wapi wanaweza kuwa katika hatari kidogo.
  • Wanahabari wengi sasa hawawezi tena kuripoti kuhusu hali inayo endelea huko Gaza.

Tumepoteza mawasiliano na wenzetu

Kama ilivyokuwa kwa wakuu wengi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa ambao jana walitoa taarifa za kutokuwa na mawasiliano na wafanyakazi wa mashirika yao wanaotoa usaidizi wa kibinadamu huzu, Kamishna Turk naye ameeleza kuwa ofisi yake imepoteza mawasiliano na wenzao walioko huko Gaza jana usiku.

“Wenzetu walikuwa tayari wameshavumilia mara kwa mara mashambulizi yanayofanywa usiku na mchana huko Gaza. Wamepoteza familia, marafiki na nyumba katika mashambulizi ambayo yameua maelfu kadhaa katika wiki tatu tu na kuharibu vitongoji vyote Gaza. Hakuna mahali salama huko Gaza na hakuna njia ya kutoka. Nina wasiwasi sana juuya wafanyakazi wenzangu, kama nilivyo na wasiwasi kwa raia wote wa Gaza.”

Maisha baada ya mashambulizi

Kamishna Turk amesema kujeruhi watu na kuwafanya maelfu ya watu wapate kiwewe haisaidii mtu yeyote. Uhasama huu utakapoisha, waliosalimika watakumbana na vifusi vya nyumba zao na makaburi ya watu wa familia zao. 

Ametanabaisha kuwa kuendelea kwa vurugu sio suluhu na kutoa wito kwa kwa pande zote pamoja na nchi tatu, haswa nchi  zile zenye ushawishi kwa wahusika kwenye mzozo, kufanya kila wawezalo kumaliza mzozo huu.

Amezihimimisha nchi hizo zenye ushawishi kufanya kazi kwa ajili ya lengo ambalo Waisraeli na Wapalestina wanaweza kufurahia kikamilifu haki za binadamu na kuishi bega kwa bega, kwa amani.