WHO: Raia, wagonjwa, na wafanyakazi wa afya huko Gaza wamelala gizani na hofu
WHO: Raia, wagonjwa, na wafanyakazi wa afya huko Gaza wamelala gizani na hofu
Wakati wa usiku wa mashambulizi makali ya mabomu na uvamizi wa ardhini ukifanyika huko Gaza, Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani WHO limesema ripoti za uhasama bado zinandelea, huku wafanyakazi wa afya, wagonjwa na raia wakikumbwa na kukatika kwa mawasiliano na kukatika kwa umeme.
Taarifa iliyotolewa leo na WHO kutoka Geneva Uswisi imesisitiza wito wake wa kusitishwa mapigano mara moja, na kuzikumbusha pande zote kwenye mzozo huo kuchukua tahadhari zote kulinda raia na miundombinu ya kiraia.
“Hii ni pamoja na wahudumu wa afya, wagonjwa, vituo vya afya, magari ya kubebea wagonjwa, pamoja na raia wanaojihifadhi katika vituo hivi. Hatua lazima zichukuliwe kuhakikisha kuwa hawadhuriwi na kunatolewa njia salama kwa ajili ya usafirishaji wa vifaa vya matibabu vinavyohitajika sana, mafuta, maji na chakula katika eneo lote la Gaza.
WHO imeripoti kuwa haijaweza kuwasiliana na wafanyakazi wake huko Gaza, kama ilivyo kwa mashirika mengine. Imeeleza kwas asa inajaribu kukusanya taarifa kuhusu athari za jumla kwa raia na huduma za afya.
Ripoti za shambulio la mabomu karibu na Hospitali za Indonesia na Al Shifa zinatia wasiwasi sana. WHO
Licha ya uwepo wa taarifa kutoka Israel zikitaka hospital kuwaondoa wagonjwa WHO imerejea maelezo yake kuwa haiwezekani kuwahamisha wagonjwa bila kuhatarisha maisha yao.
Hospitali zote huko Gaza tayari zinafanya kazi kwa kiwango cha juu zaidi kutokana na majeruhi wanaowapokea katika wiki adhaa za mashambulizi ya mara kwa mara, na kwmaba hospital hizo haziwezi kustahimili ongezeko kubwa la idadi ya wagonjwa, wakati huohuo wakitoa hifadhi kwa maelfu ya raia.
Wafanyakazi wa afya ambao wameamua kusalia ili kutoa huduma kwa wagonjwa wao huko Gaza
- Wanakabiliwa na upungufu wa vifaa,
- Hawana mahali pa kuwaweka wagonjwa wapya,
- Hakuna njia ya kupunguza maumivu ya wagonjwa wao.
- Kuna majeruhi zaidi kila saa, lakini magari ya kubeba wagonjwa hayawezi kuwafikia kutokana na kukatika kwa mawasiliano.
- Vyumba vya kuhifadhia maiti vimejaa.
- Zaidi ya nusu ya waliofariki ni wanawake na watoto.
WHO imetoa wito wa ubinadamu kwa wale wote walio na uwezo wa kukomesha mapigano kufanya hivyo hivi sasa, kwa mujibu wa azimio la Umoja wa Mataifa lililopitishwa hapo jana tarehe 27 Oktoba 2023 likitaka kusitishwa kwa mapigano kwa sababu za kibinadamu, pamoja na kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa raia wote wanaoshikiliwa mateka.