Guterres: Badala ya kusitishwa kwa mapigano huko Gaza nimeshangazwa na ongezeko lisilo la kifani
Guterres: Badala ya kusitishwa kwa mapigano huko Gaza nimeshangazwa na ongezeko lisilo la kifani
Licha ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hapo jana kupitisha azimio la kutaka mshambulizi kusitishwa kwa sababu za kibinadamu huko Ukanda wa Gaza, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza kusikitishwa kwake na ongezeko lisilo la kifani la mashambulizi.
Guterres ametoa kauli hiyo hii leo huko Doha nchini Qatar wakati wa mkutano wake na Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al-Thani ambaye pia ni Waziri wa mambo ya nje wan chi hiyo.
Guterres ambaye yupo safarini kuelekea nchini Nepal ametoa shukran zake za dhati kwa serikali ya Qatar kwa juhudi zake za mashauriano kuhusu mgogoro wa Mashariki ya Kati. “Nimewashukuru kwa mchango wao kwenye mipango wa upatanishi ya Qatar, ambayo ni kwa mateka wote walioko Gaza kuachiliwa.”
Akizungumzia kuhusu hali ya Gaza, Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema alipata moyo kwa siku za hivi karibuni kwa jinsi kulikuwa na ongezeko la uungwaji mkono wa jumuiya za kimataifa ikiwepo nchi zinazo iunga mkono Israel ambazo ziliona ipo “haja ya angalau kusitishwa kwa mapigano kwa sababu za kibinadamu ili kuwezesha mateka kuachiliwa huko Gaza, raia wa nchi ya tatu waweze kutoka eneo hilo la machafuko na ongezeko kubwa la lazima la utoaji wa misaada ya kibinadamu kwa watu huko Gaza.”
Guterres anasema “Cha kusikitisha, badala ya kusitishwa, nilishangazwa na ongezeko lisilo na kifani la mashambulizi ya mabomu na athari zake mbaya, na kudhoofisha malengo ya kibinadamu.”
Kutokuwepo kwa mawasiliano na walioko Gaza
Tangu hapo jana 27 Oktoba 2023 mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa yanayofanya kazi huko katika Ukanda wa Gaza yameeleza kutokuwa na mawasiliano na timu za wafanyakazi wao walioko Gaza.
Guterres amezungumzia pia suala hilo na kusema “Kwa kuzingatia kukatika kwa mawasiliano, pia nina wasiwasi mkubwa kuhusu wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa ambao wako Gaza kutoa msaada wa kibinadamu.”
Mkuu huyo wa UN amesema hali hii lazima ibadilishwe. “Ninasisitiza ombi langu kubwa la usitishaji mapigano wa haraka kwa sababu za kibinadamu, pamoja na kuachiliwa huru bila masharti kwa mateka na utoaji wa misaada ya kibinadamu katika kiwango kinacholingana na mahitaji makubwa ya watu huko Gaza, ambapo janga la kibinadamu linatokea mbele ya macho yetu.”
Amehitimisha taarifa yake kwa kwa kurejea kauli yake aliyoitoa hapo jana “Huu ni wakati wa ukweli. Kila mtu lazima atekeleze wajibu wake. Historia itatuhukumu sote.”