Bila mafuta, hakuna mkate: WFP

Bila mafuta, hakuna mkate: WFP
Hali mbaya inayowakabili mamia kwa maelfu ya Wapalestina huko Gaza inaweza kuwa mbaya zaidi, kutokana na uhaba mkubwa wa mafuta ambao unatishia kusimamisha chakula na shughuli zingine za kibinadamu.
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP eneo linalokaliwa la Palestina Samer Abdeljaber amesema bila ya mafuta ya ziada, viwanda vya kuoka mikate vinavyofanya kazi havitaweza tena kuzalisha mikate.
“Ni viwanda vyetu viwili tu vya kuoka mikate vilivyo na kandarasi vina mafuta ya kuzalisha mikate kwa sasa na kesho huenda visiwepo. Hili litakuwa pigo baya kwa maelfu ya familia zinazoishi katika makazi ambayo yamekuwa yakitegemea usambazaji wa mikate wa kila siku.” Amesema Samer.
“Watu wa Gaza wanahitaji kufikishiwa misaada endelevu katika kiwango ambacho kinalingana na mahitaji makubwa. Ili kupunguza mateso na kuwezesha utoaji wa usaidizi wa kuokoa maisha, tunarudia wito wa Katibu Mkuu (wa UN) kusitishwa kwa mapigano kwasababu za kibinadamu,” aliongeza.

Operesheni za WFP huko Palestina tangu kuanza kwa mgogoro huo:
Mpaka sasa tayari WFP imefikisha usaidizi kwa karibu watu 630,000 wanaopatiwa hifadhi na katika jamii kote Gaza na Ukingo wa Magharibi.
Msaada huo unajumuisha chakula cha dharura, chakula cha kwenye makopo, mikate, na vocha za kielektroniki katika maeneo ambayo maduka yamefunguliwa na yana vyakula.
Kwa wastani watu 200,000 wanaopatiwa Msaada wa makazi hupokea mikate inayotolewa na WFP kila siku lakini uhaba wa mafuta unafanya kuwa vigumu zaidi kwa makampuni ya kuoka mikate kufanya kazi.
Siku ya Jumatano, (tarehe 25 Oktoba 2023) watu 150,000 pekee walipokea mkate.
Hivi sasa, ni viwanda viwili tu vya kuoka mikate vyenye mkataba wa WFP ndio vinavyofanya kazi, ikilinganishwa na viwanda 23 hapo mwanzoni mwa operesheni hiyo.
Waoka mikate wanaofanya kazi kwa sasa wanazalisha karibu mara sita zaidi ya kuwango walichokuwa wakizalisha hapo awali.

Kilio cha Mafuta
Mafuta sio muhimu tu kwa ajili ya viwanda vya kuoka mikate.
- Mafuta yanahitajika pia kwaajili ya malori yanayopokea misaada inayoingia kupitia mpaka wa Rafah na kusambaza misaada hiyo katika eneo lote la Gaza.
- Mafuta ni muhimu kwa hospitali
- Mafuta ni muhimu kwa ajili ya kuvuta maji kutoka kwenye visima katika vituo vinavyotoa maji.
Vocha za kielekroniki
Misaada muhimu ya chakula inaisha haraka katika maduka ya Gaza. Licha ya chakula zaidi kupatikana kwa wauzaji wa jumla, maduka yanayouza kwa rejareja hayawezi kununua tena kutokana na barabara kuharibika, wasiwasi wa usalama na uhaba wa mafuta.
Takriban asilimia 10 ya maduka yenye kandarasi ya WFP yamekosa chakula.
WFP inaendelea na usambazaji wa vocha za kielektroniki za chakula huko Gaza na hadi sasa asilimia 88 ya watu waliopokea vocha hizo wamezitumia.
Hata hivyo uwezo wa maduka kuendelea kutoa huduma kwa wanaolipa kwa kutumia ovocha za WFP unapungua kadri hifadhi ya chakula inavyokwisha.

Misaada ya WFP inaendelea kuwasili huko Gaza
Malori tisa ya WFP yakiwa yamebeba tani 141 za chakula tayari yamevuka hadi Gaza tangu kufunguliwa kwa mpaka wa Rafah siku ya Jumamosi tarehe 21 Oktoba.
Malori mengine 39 ya WFP yako tayari au yako karibu na mpaka wa Misri na Gaza yakingoja kuingia.
Ili WFP iweze kuongeza utekelezaji wa shughuli zake kufikia watu milioni 1.1 katika muda wa miezi miwili ijayo, malori 40 yanahitaji kuingia Ukanda wa Gaza kila siku.
Kadiri mahitaji yanavyoongezeka, WFP inarekebisha mahitaji yake ya ufadhili kwenda juu na inakadiria kuwa itahitaji angalau dola milioni 100 kwa siku 90 zijazo ili kuendeleza ufikiaji wa wahitahi kwa dharura.