Simulizi kutoka Gaza: “Ninatafuta mtandao ili kuangalia maeneo yaliyoathirika huku nikitumai sitaona jina la mume wangu wala familia yangu kwenye orodha”

Simulizi kutoka Gaza: “Ninatafuta mtandao ili kuangalia maeneo yaliyoathirika huku nikitumai sitaona jina la mume wangu wala familia yangu kwenye orodha”
Hebu vuta tasirwa, mama akiwabembeleza watoto wake usiku, hofu ya kutengana nao ikija kama kivuli, kujaribu awezavyo kujilinda yeye na familia yake, ili ‘wasiwe kumbukumbu’ hata hivyo, hadithi yetu ni kumbukumbu tu sasa, lakini wakati ujao bado haujaandikwa, nikiamka kesho, nataka hili limalizike, ilinirejee mahali patakatifu, kwenye nyumba yetu.
Ndivyo inavyoanza simulizi ya Shahd, mwenye umri wa miaka 34 ambaye kwa muda wa siku 17 zilizopita, yeye na watoto wake wamekuwa katika safari ya kutisha, kujikinga na mashambulizi ya makombora yasiyokoma, wamehama kutoka makazi ya muda hadi sehemu nyingine kusaka usalama.
Shahd na watoto wake wamejiunga na maelfu ya watu wengine waliojazana katika makazi hayo ya muda, na vifaa vichache, hakuna umeme, na hakuna mahali pa kulala, wanaishi na zaidi ya wafanyakazi wenza 100 na familia zao katika vyumba viwili vya makazi, wana umeme kwa saa chache wakati wa mchana, lakini usiku, kupunguzwa kwa nguvu, joto hupungua, na hawana chochote. Hawajui kesho itakuwaje.
Shahd amefanya kazi katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo UNDP kwa Watu wa Palestina kwa miaka 10 na ametumia maisha yake yote huko Gaza, Mji huu umekuwa makazi yake, hapa ndipo alipokulia, akaolewa, na sasa analea watoto wake, walakini, siku ambayo alitoroka nyumbani kwake, ilionekana tofauti, kana kwamba sura moja ilikuwa imefungwa kabisa.
“Ilikuwa jambo la kuhuzunisha sana kuondoka nyumbani kwangu, bila uhakika kama tungewahi kurudi salama, au kama tungeweza kurudi na kupata nyumba zetu zingalipo baada ya uharibifu mkubwa uliokuwa ukiendelea, ni ngumu sana kwa njia nyingi, ina athari nyingi na utata wake unatulemea sana, unaathiri maisha yetu na chaguzi tunazofanya kama Wapalestina wanaoishi Gaza.”

Safari ya Shahd kutoka kwenye makazi ya dharura hadi nyingine inafichua ukweli wa kutisha wa mgogoro wa kibinadamu.
“Kuna mzozo wa kweli wa kibinadamu, makazi ni zaidi ya uwezo, maelfu ya watu katika nafasi ndogo, hatukuweza kupata chochote cha kutumia hapa, hakuna magodoro, hakuna mito, maji yalikuwa machache sana, vyoo viliziba na bila shaka hakukuwa na chakula, ilikuwa ni unyama sana kwetu na kwa wengine,”
Shahd aliongeza “tulikaa hapo kwa usiku mmoja na kushiriki nafasi moja na mwenzangu, watoto wake na watoto wangu wawili, kulikuwa na giza, hakuna umeme, hakuna chakula na hakuna uhusiano na muhimu zaidi, hakuna usalama”.
Takriban watu 600,000 wanahifadhi katika baadhi ya vituo 150 vya UNRWA katika Ukanda wa Gaza, na idadi inaendelea kuongezeka, majengo haya hayana vifaa kama makazi ya dharura, mahitaji ya kimsingi na muhimu ya familia kama vile umeme, maji, mafuta, nishati na huduma za matibabu hazipatikani.
Vita vinavyoendelea dhidi ya Gaza vimesababisha madhara makubwa kwa raia, zaidi ya Wapalestina 5,000 wamepoteza maisha, huku wengi wao wakiwa ni watoto, wanawake na wazee, huku zaidi ya watu 15,000 wakijeruhiwa, wakati wengi wamefukiwa na vifusi, wengine wamezikwa bila kutambuliwa majina yao.
“Nilipoteza binamu zangu wawili, binamu yangu Yousef, kijana mrembo ambaye mtoto wake, Misk, sasa ni yatima, na binamu yangu Abeer na watoto wake wawili, na kuwaacha wengine wawili hai wakihangaika kuishi bila yeye, siku tulipowapoteza, nilishika simu mkononi, nikaisoma habari na majina yao hayakutajwa, zilikuwa namba tu, lakini kwetu sisi, wana majina, walikuwa wanadamu, wapendwa, sehemu ya familia yetu ambao hatutasahau kamwe,” Shahd alisema.
Tangu mzozo huo uanze, takriban watu milioni 1.4 kati ya wakazi milioni 2.2 wa Gaza wameyakimbia makazi yao, maduka yanakosa vifaa kutokana na mahitaji makubwa ya chakula na maji.
Shahd ametenganishwa na mumewe na familia yake yote, anaishi na watoto wake wawili katika makao ya dharura, huku mume wake na wengine wa familia wakiishi maili nyingi katika eneo lisilo salama, na si kwa hiari, ana wasiwasi juu yao kila wakati.
“Mume wangu na familia yake hawana huduma ya umeme wala mtandao, mume wangu hunitumia jumbe za maandishi (SMS) na kuniomba nimhabarishe kwa sababu ninaweza kufikia baadhi ya vyanzo, kila usiku ninajaribu kulala, ninasubiri hadi saa nane mchana ili niweze kupata mtandao kuangalia maeneo, majina au familia ambazo zililengwa, nikitumaini kwamba jina la familia yangu, mume wangu, halitakuwepo kwenye orodha ya majeruhi.”

Huku akiwa anakimbia, Shahd anaendelea kujaribu kuhudumia jamii yake, akiwa mstahimilivu katika kukabiliana na matatizo, hata huku akiwa hawezi kupata mahali salama katika Jiji lake na Kitongoji chake.
"Ninatumai kwamba ulimwengu hautatuona tu kama idadi, au wanaotafuta misaada ya kibinadamu, lakini kama watu binafsi wenye hadithi na ndoto, ninaomba jumuiya ya kimataifa kusikiliza na kuelewa kinachoendelea hapa na kukomesha vita hivi.”
"Katika usiku wetu wa kukosa usingizi kwenye makazi, sote mara nyingi tunajiuliza tunafanya nini hapa, jinsi tuliishia hapa, tunatamani haki yetu ya kurudi nyumbani kwetu, Gaza, Gaza tunaipenda na tunaikosa!”