Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mikoko Pamoja waibuka kidedea katika tuzo ya UN ya Mtu mahiri wa Mwaka

Mshindi wa kwanza na wa pili wa UN Person of the year awards wakitunukiwa na UNIS Nairobi.
UN News/Thelma Mwadzaya
Mshindi wa kwanza na wa pili wa UN Person of the year awards wakitunukiwa na UNIS Nairobi.

Mikoko Pamoja waibuka kidedea katika tuzo ya UN ya Mtu mahiri wa Mwaka

Tabianchi na mazingira

Ofisi ya Umoja wa Mataifa jijini Nairobi, Kenya UNON, imekitunuku tuzo kikundi cha kuhifadhi mazingira cha Mikoko Pamoja tuzo ijulikanayo kama Mtu mahiri wa mwaka wa Umoja wa Mataifa au “UN Person of the year”, tuzo inayotolewa kila mwaka  kwa kazi nzuri inayofanyika katika jamii.

Mwaka huu tuzo hii imemulika juhudi za wakaazi wa eneo la Gazi katika  kaunti ya Kwale Kenya waliofanikiwa kubadili tabia iliyozoweleka ya kukata mikoko na badala yake kupanda mikoko hiyo. 

Mshindi wa kwanza na pili wa tuzo ya UN ya Mtu mahiri wa Mwaka.
UN News/Thelma Mwadzaya
Mshindi wa kwanza na pili wa tuzo ya UN ya Mtu mahiri wa Mwaka.

Uzeni hewa ukaa sio kuni 

Mradi wa Mikoko Pamoja ambao ni wa muda mrefu mpaka sasa umefanikiwa kufyonza na kuuza hewa ukaa inayoharibu mazingira na kuwafanya kunufaika kwa kipato kilichowabadilishia Maisha yao. 

Mikoko ina uwezo mkubwa wa kufyonza hewa ukaa ikilinganishwa na miti mingine ya nchi kavu. 

Hewa ukaa ina athari kubwa ikiwemo kuchangia huchangia katika ongezeko la joto ulimwenguni. 

Mikoko inategemewa sana na jamii za pwani kwa mbao, Kuni na pia ni sehemu za mazalia ya samaki. 

Saumu Ali ni mwanachama wa kikundi cha Mikoko Pamoja na anaamini kuwa tuzo hiyo itawatia moyo wengi huko Gazi na “Wanaotushika mkono msichoke tunawategemea ninyi . Mikoko Pamoja ni mrasi ambao kwa jumla inahusisha jamii kulinda mazingira, kulinda mikoko,kwa hewa safi na mazingira mazuri. Mikoko pamoja ni kikundi kilichojiunga kuiwezesha jamii kujitegemea wenyewe. Kupitia mikoko tunauza hewa ukaa na kuendeleza tusiyoweza kuyatimiza.”

Mikoko ndiyo mapafu ya bahari

Tangu mwaka 2013, Mikoko Pamoja imefanikiwa kuhifadhi na kufufua eneo la ukubwa wa ekari 117 la misitu ya mikoko. 

Kutokana na mikoko hiyo jamii za Gazi zimeweza  kupata dola laki mbili na kumi baada ya kuuza tani zisizopungua alfu 18,500 za hewa ukaa kama anavyoelezea Dr. James Kairo ambaye ni mtafiti mkuu na mwana sayansi kwenye taasisi ya utafiti na uvuvi  nchini Kenya, KMFRI kuwa, “Badala ya kuuza miti kama kuni, tuuzeni hewa ukaa. Hewa ukaa haitaki ukate mti, wewe unakaa na kulinda ule mti. Ukishaulinda mti, utavuta hewa ukaa ili kulinda mazingira yetu, italeta samaki na pia itazuwia mmomonyoko wa udongo. Bahari inapanda na mikoko iliyo Kati Kati ya nchi kavu na bahari ni kama boma. Kwahiyo wakati tunarejesha mikoko yetu tunaboresha mazingira,tunaleta uchumi endelevu kwa watu wetu na pia tunachangia samaki.” 

Jamii zina uwezo wa kusaka suluhu za kudumu

Mapato ya mradi wa Mikoko Pamoja yameigeuzia jamii ya Gazi maisha kwa kufadhili ujenzi wa shule, hospitali na huduma za maji safi kwa wakaazi zaidi ya elfu 7.

Kwa upande wake, ofisi ya Umoja wa Mataifa Jijini Nairobi, UNON, imesema imeutunza mradi wa Mikoko Pamoja kwani ni mfano mzuri wa jinsi jamii zinavyoweza kuleta mabadiliko katika maendeleo endelevu na kuhifadhi mazingira. 

Sandra Macharia ni mkuu wa kitengo cha habari cha Umoja wa Mataifa katika ofisi ya Nairobi anaelezea umuhimu wa siku ya Umoja wa Mataifa kutambua juhudi kama za Mikoko Pamoja.

“Tunapokumbuka umuhimu wa siku ya Umoja wa mataifa, tunajitahidi kuwatambua watu kuleta mabadiliko katika jamii, kuwa mfano na kusogeza mbele juhudi za kutimiza malengo endelevu ya maendeleo , SDGs, kwani ndio maana ya jamii kuwa mstari wa mbele kutambua changamoto na suluhu zake. Kwahiyo kwetu sisi, hiyo ndio maana ya mtu mahiri wa Umoja wa mataifa kwa Kenya “.

Kwa mujibu wa shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP, Juhudi za kuhifadhi mazingira zina mchango mkubwa katika jamii ukizingatia kuwa wanawake ndio wanaohusika zaidi kwenye miradi hiyo.

Mshindi wa pili wa tuzo ya UN ya Mtu mahiri wa Mwaka Mary Mariach kutoka West Pokot akiwa na Sandra Macharia mkuu wa UNIS.
UN News/Thelma Mwadzaya
Mshindi wa pili wa tuzo ya UN ya Mtu mahiri wa Mwaka Mary Mariach kutoka West Pokot akiwa na Sandra Macharia mkuu wa UNIS.

Wanawake wana mchango mkubwa

Aliyejinyakulia nafasi ya pili katikatuzo hiyo ya mtu mahiri wa mwaka wa Umoja wa Mataifa ni Mary Mariach ambaye ni mtetezi wa haki za wanawake za kumiliki ardhi aliteuliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO , kwa kazi yake. 

Mary anaafiki kuwa, ”Kina Mama Sasa hivi wanaelewa haki zao hasa kwa upande wa mashamba. Tuliwaambia wazee kuwa Kina Mama ndio wanao tunza Mali katika jamii. Kwahiyo wakilinda shamba Kina Mama watakuwa na ulinzi fulani.ama akiwa na sehemu ndogo ya kulima au kufuga wanyama , mama akipewa ile nafasi ataweza kufanya mambo mengi katika jamii. Imekuwa Safari ndefu lakini Tumefanikiwa.”

FAO, imekuwa mwenyeji wa mradi wa usimamizi wa ardhi ili kushajiisha maendelo na ulinzi wa haki za kina mama za kumiliki ardhi. 

Husna Mubarak ni afisa wa masuala ya kumiliki ardhi katika uhifadhi wa mifumo ya chakula kwenye shirika la FAO, anaamini kuwa hii ni hatua ya msingi na,”Wanawake ndio wanaotumia ardhi kwa kiwango kikubwa sana. Hili ni onyesho kuu kuona hapa mama ameweza kujitokeza kama mwanamke na pia jamii yake kuweza kuhakikisha kuwa wameweza kumiliki na kutumia na kusimamia ardhi vile inavyotakiwa. Mradi huu sio wa Kenya Tu na kwa West Pokot eneo Hilo Lina ardhi kubwa ya jamii na wengi hi wafugaji “.

Soundcloud

Tuzo hii ya Umoja wa mataifa ni dhihirisho kuwa mahitaji ya binadamu na uhifadhi wa mazingira ni lila na fila havitengamani na vinahitaji ushirikiano wa jamii na ubunifu.