Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa laitisha mkutano wa dharura kuhusu Gaza
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa laitisha mkutano wa dharura kuhusu Gaza
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo mjini New York, limeitisha mkutano maalum wa dharura kuhusu mzozo baina ya Israel na Gaza, huku kukiwa na mkwamo unaoendelea katika Baraza la Usalama, na hali katika eneo hilo inazidi kuwa mbaya zaidi kila saa.
Kikao hicho maalum cha kumi cha dharura cha Baraza kuu kinatarajiwa kuanza saa 10 asubuhi, saa za New York, na kitajumuisha wazungumzaji wasemaji 110 wameandikwa kwenye orodha.
Taifa la Palestina linatarajiwa kuhutubia nchi wanachama kwanza, na kufuatiwa na Israel.
Riyad Mansour, Mwangalizi wa Kudumu wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa, akizungumza katika mkutano huo wa dharura amekumbuka maoni ya hivi karibuni ya Israel katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu jinsi watu wake wanavyoteseka, amesema Wapalestina pia wanateseka. Mwakilishi wa Israel alitoa wito wa "kuwaachilia mateka, kisha inawachukua Wapalestina milioni mbili mateka ".
Ameongeza kuwa kuna Wapalestina 1,000 wanaouawa kila siku, akiongeza kuwa hakuna kinachoweza kuhalalisha uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
"Kwa nini usihisi uharaka wa kukomesha mauaji," amehoji "Unaturudisha nyuma miaka 80 kwa kujaribu kuhalalisha kile Israeli inachofanya sasa."
Miongo ya kukaliwa
Bwana Mansur amesema Wapalestina wamenusurika kwa miongo kadhaa ya kukaliwa kwa mabavu, miaka 16 ya vizuizi na vita tano huko Gaza.
Amesisitiza kwamba suluhu ya mauaji ya Waisraeli na Wapalestina sio mauaji zaidi akiomba wanachama wa Umoja wa Mataifa kuzingatia kanuni za Umoja wa Mataifa na kuzuia vizazi vijavyo dhidi ya janga la vita.
Amesema "Njia pekee ya kusonga mbele ni haki kwa watu wa Palestina. Pigeni kura kukomesha mauaji, piga kura kukomesha wazimu huu. Chagua haki, sio kisasi. Chagua amani, sio vita zaidi. Piga kura ili kukomesha takriban wiki tatu za za kuwa naviwango viwili vibaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika miongo kadhaa. Usipoteze fursa hii. Maisha ya watu yako hatarini. Tafadhali, okoa maisha, okoa maisha, okoa maisha.”
Mkutano wakati vifo vikiongezeka Gaza: Palestina
Bwana Mansour aliyezungumza kwanza kwenye mkutano huo amesema "Tunakutana hapa wakati Wapalestina huko Gaza wanaghubikwa na mabomu. tunazungumza wakati familia zinauawa, wakati hospitali zinasimama kufanyakazi, wakati vitongoji vinaharibiwa, wakati watu wanakimbia kutoka sehemu moja kwenda nyingine bila mahali salama pa kwenda."
Ameendelea na kusisitiza kuwa "Hakuna wakati wa kuomboleza”, huku akibubujikwa na machozi, akionyesha idadi inayoongezeka ya vifo.
Amesema "Usipokomesha kwa wajili ya wale wote waliouawa, ikomeshe kwa wale wote wanaoweza kuokolewa."
Akizungumzia Maisha yake binafsi katika eneo hilo amesema misaada ya kibinadamu inahitajika sana. Hospitali zinafanya kazi bila dawa za ganzi, huku madaktari na wagonjwa wakiwa wanajiuliza ikiwa msaada uko njiani.
"Wakati huu mambo yamefurutu ada.” Amehitimisha Mansour.
Hakuna maneno kwa uovu wa Hamas
Kutoka kwenye jukwaa la Ukumbi wa Baraza Kuu, Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa Gilad Erdan aliwasilisha video kwenye Tablet yake, na kuwaonyesha wajumbe, ambayo amesema inaonyesha mauaji ya kikatili kwa kutumia kifaa cha kutengenezea bustan dhidi ya mfanyakazi wa shamba asiye na msaada kutoka Thailand.
"Hakuna maneno katika lugha yoyote ya kuelezea maovu ambayo tumeshuhudia hivi karibuni, kutoka mikononi mwa mwanamgambo wa Hamas, amesema akiongeza kuwa hayaelezeki kwa sababu hayana nafasi katika ubinadamu.
“ISIS ilikuwa dola ya Kiislamu ya Iraq na Syria na Hamas ni dola ya Kiislamu ya Gaza. Kama ilivyofanyika kwa ISIS, Hamas lazima isiwepo tena."
Akisema kwamba lengo la Israeli ni "kuondoa kabisa uwezo wa Hamas na tutatumia kila njia tuliyo nayo kutimiza hili. Si kwa kulipiza kisasi, si kwa kujibu ,mashambulizi. Lakini kuhakikisha upotovu na ukatili huo hautokei tena,”
Tuko katika vita na Hamas: Israel
Balozi Gilad Erdan, amesema mauaji ya Oktoba 7 na kile kilichotokea hayana uhusiano wowote"na Wapalestina, mzozo wa Waarabu na Israeli au suala la Palestina.
"Hii sio vita na Wapalestina. Israel iko vitani na kundi la kigaidi la wanajihadi la Hamas. Ni Israel inayotii sheria ya demokrasia dhidi ya Manazi wa siku hizi."
Ameendelea kubainisha kuwa Hamas haijali watu wa Palestina, amani wala mazungumzo. Lengo lake pekee ni kuangamiza Israeli na kuua kila Myahudi juu ya uso wa Dunia."
Bwana Erdan amezungumzia pia mauaji ya kikatili ya raia wasio na hatia wa Israel na kulenga kimakusudi timu za madaktari za Israel ambazo zilikuwa zikijaribu kuwasaidia waliojeruhiwa wakati wa shambulio la kigaidi. Amehoji "unafiki" kwamba hakuna tamko hata moja la kulaani ukatili dhidi ya Waisraeli akisisitiza kwamba "Unafiki ni wa kuvuka mipaka."
Rais wa Baraza Kuu
Rais wa Baraza Kuu Bwana Dennis Francis amesema "Amefadhaika sana na kusikitishwa na matukio yanayoendelea nchini Israel na Palestina.
"Bado tena, tunakusanyika katikati ya kuongezeka kwa ghasia na uhasama huko Mashariki ya Kati katika miongo kadhaa. Vurugu hizo lazima zikome sasa" amesema.
Ametoa wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja na bila masharti kwa sababu za kibinadamu na kufunguliwa kwa njia za kuingiza misaada kwa wenye uhitaji.
Amelaani mashambulizi dhidi ya Israel yaliyofanywa na Hamas tarehe 7 Oktoba, akisema "ukatili wa mashambulizi ya Hamas ni wa kusikitisha na haukubaliki, na hauna nafasi katika ulimwengu wetu."
Pia amelaani kulengwa kiholela kwa raia wasio na hatia huko Gaza na uharibifu wa miundombinu muhimu unaofanywa na Israeli, akisema "mashambulio ya mara kwa mara ya Ukanda wa Gaza yanayofanywa na Israeli na matokeo yake ni ya kutisha sana."
Kulinda na kuokoa maisha
Rais wa Baraza Kuu Francis amesisitiza kwamba kipaumbele kikuu cha wanachama wa Umoja wa Mataifa kwa pamoja "lazima kiwe kulinda na kuokoa maisha ya raia."
Amesisitiza kwamba "Pande zote katika mzozo huu lazima zizingatie sheria ya kimataifa za kibinadamu, na kuunda mara moja mazingira muhimu ili kuruhusu kufunguliwa kwa njia ya kufikisha msaada wa kibinadamu katika Ukanda wa Gaza."
Ameongeza kuwa msaada unaohitajika haraka wa kuokoa maisha lazima uwafikie wale wenye uhitaji.
Pia amesifu kazi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa huko Gaza, na kutoa rambirambi kwa familia za wafanyakazi 35 wa shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA waliouawa tangu kuanza kwa mgogoro huo.
Mkutanoo maalum wa dharura
Chini ya azimio muhimu la "Kuungana kwa ajili ya amani", lililopitishwa na Baraza Kuu mwaka 1950, chombo hicho kinaweza kuitisha kikao maalum cha dharura" ndani ya saa 24, ikiwa Baraza la Usalama litashindwa kutekeleza jukumu lake la msingi la kudumisha amani ya kimataifa na usalama.
Kikao maalum cha kumi cha dharura kiliitishwa kwa mara ya kwanza Aprili 1997, kufuatia ombi kutoka Qatar.
Ukafuatia mfululizo wa mikutano ya Baraza la Usalama na Baraza Kuu kuhusu uamuzi wa Israel wa kujenga mradi mkubwa wa makazi ya walowezi katika eneo la Jerusalem Mashariki.
Kikao hicho kiliitishwa mara ya mwisho tarehe 13 Juni 2018 ili kuzingatia rasimu ya azimio lenye kichwa "Ulinzi wa raia wa Palestina".
Mwishoni mwa kikao hicho, Baraza liliamua kuahirisha kikao “kwa muda na kumpa mamlaka Rais wa Baraza Kuu katika kikao chake cha hivi karibuni kurejea kikao hicho kwa ombi la nchi wanachama.”
Mgogoro unaoendelea
Kwa mujibu wa mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa yaliyopo Gaza, vifaa muhimu vya kuokoa maisha, mafuta ya kuendesha hospitali na maji ya kunywa vinaisha.
Wakati huo huo jana Jumatano, Baraza la Usalama lilishindwa kupitisha maazimio mawili kuhusu kushughulikia mzozo wa kibinadamu. China na Urusi zilipigia kura ya turufu rasimu ya azimio lililoongozwa na Marekani na azimio la pili lililoungwa mkono na Urusi halikuweza kupata kura za kutosha kuungwa mkono.
Hii ilifuatia kushindwa kuwa na umoja katika Baraza, wiki iliyopita. Rasimu ya azimio lililoongozwa na Urusi inayotaka "kusitisha mapigano mara moja" ilipigiwa kura Jumatatu iliyopita na Jumatano iliyofuata, Marekani ilipinga maandishi yaliyoongozwa na Brazil ambayo yalitaka "kusitishwa kwa uhasama kwa minajili ya kibinadamu" ili kuwasilisha misaada kwa mamilioni ya watu katika Ukanda wa Gaza.