Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Changamoto ya mafuta inaweka hatarini msaada wa kibinadamu Gaza: UN

Mwanamume anatembea kwenye shamba la vifusi mbele ya majengo kadhaa ya ghorofa yaliyoharibiwa vibaya na kuharibiwa huko Gaza.
© WFP Majengo yaliyosambaratishwa Al-Kass Gaza

Changamoto ya mafuta inaweka hatarini msaada wa kibinadamu Gaza: UN

Amani na Usalama

Operesheni za kibinadamu huko Gaza zimekuwa hatarini kusitishwa leo Jumatano kutokana na changamoto kubwa ya mafuta inayoendelea, wakati Israeli ikiendelea kukabiliana na mgogoro wa muda mrefu wa mateka huku kukiwa na athari mbaya ya mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7.

Tahadhari kutoka kwenye hospitali kuu ya Gaza iliyo kusini mwa eneo hilo inasema kwamba shughuli za kuokoa maisha zitasitishwa leo jioni kwa sababu ya uhaba wa mafuta na tahadhari hiyo imefuatia ombi la mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres la kusitisha mapigano mara moja.

Mapigano yanahitaji kukoma, aliliambia Baraza la Usalama jana Jumanne, ili "kupunguza mateso makubwa, kufanya utoaji wa misaada kuwa rahisi na salama na kuwezesha kuachiliwa kwa mateka".

Amesema ingawa hakuna kitu kinachoweza kuhalalisha mashambulizi ya kuogofya ya Hamas ya tarehe 7 Oktoba, ni muhimu kutambua kwamba "hayakutokea katika ombwe na wala kuyahalalisha adhabu ya pamoja ya Wapalestina.”

Kufuatia maoni ya Katibu Mkuu, balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa Gilad Erdan alitangaza kuwa maafisa wa Umoja wa Mataifa,watanyimwa vibali vya kusafiri ama visa akisema kuwa hotuba ya Bwana  Guterres ilitaka kuhalalisha shambulio la kikatili la Hamas ambalo lilisababisha vifo vya watu 1,400.

Kibali cha kwenda Israel tayari kimekataliwa kwa mkuu wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya kibinadamu na masuala mya dharura Martin Griffiths, Bwana Erdan amesema katika mahojiano na vyombo vya habari.

Wafanyakazi wa UNICEF nchini Misri wanapakia vifaa katika ghala huko Gaza.
UNICEF Egypt UNICEF ikitayarisha msaada wa muhimu kwenda Gaza

Kiwewe kikubwa Israeli 

Maumivu ya walionusurika na mzigo wa kisaikolojia wa pamoja ulioletwa na mgogoto wa mateka ambapo zaidi ya Waisraeli 220 na raia wa kigeni bado wanazuiliwa huko Gaza vimesababisha mahitaji ya afya ya akili kuongezeka, amesema mwakilishi maalum wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO nchini Israel Dkt. Michel Thieren.

Alipokuwa akitembelea hospitali katika mji wa kusini mwa Israel wa Ashkelon ambayo inatibu watu kati ya 4,600 waliojeruhiwa katika mashambulizi hayo, Dkt. Thieren amesema "karibu kila mmoja wa manusura hao ameshuhudia mtu mwingine akifa kabla ya wao wenyewe kujeruhiwa".

Miji imesalia mahame

Afisa huyo wa WHO amesisitiza kwamba afya ya kiakili ya madaktari na wauguzi aliokutana nao nchini Israel imeathiriwa kiasi kikubwa na hadithi za manusura na majeraha waliyokuwa wakitibu.

Pia alitembelea kambi za kijeshi ambapo maiti nyingi za wahanga 1,400 wa mashambulio ya Hamas zimehifadhiwa kwenye makontena yaliyowekwa kwenye majokofu na kuzungumzia athari kwa madaktari na wataalam wa uchunguzi wanaohangaika kuwatambua marehemu hao.

"Nimetembelea miji mahame ya kusini ambayo watu wake wamehamishwa. Bado kuna uvundo mbaya wa vikifo. Kivuli cha mshtuko na huzuni ya kitaifa kimeitumbukiza nchi hii gizani. Afya ya akili inapoharibika, ndivyo afya ya kimwili inavyoharibika,” amesema Dkt Thieren.

Familia za Wapalestina waliokimbia makazi yao zikihifadhi katika korido ya hospitali katika Ukanda wa Gaza. Wanawake na watoto wamepumzika kwenye blanketi na magodoro kando ya sakafu ya vigae.
© WHO Hospitali ya Al Shifa inatumika kama makazi ya familia zilizohamishwa huko Gaza.

Uhaba mkubwa wa mafuta

Wakati huo huo huko Gaza, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, ambalo ndilo shirika kubwa zaidi la utoaji wa misaada ya kibinadamu katika eneo hilo, limeonya kwamba mafuta yasiporuhusiwa kuingia, litalazimika kusitisha shughuli zote kufikia leo Jumatano usiku.

Gaza imekuwa gizani kutokana na kukatika kwa umeme tangu Oktoba 11 na uhaba wa mafuta umeathiri huduma muhimu kuanzia kwenye magari ya kubeba wagonjwa hadi viwanda vya kuoka mikate na vifaa vya kupampu maji.

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari, msafara wa nne wa misaada ya kibinadamu uliwasili katika eneo hilo kupitia kivuko cha mpaka cha Rafah jana jioni, ukiwa na malori manane kutoka chama cha Hilali Nyekundu cha Misri.

Jana Jumanne pia ilishuhudiwa idadi kubwa zaidi ya vifo vilivyoripotiwa katika siku moja huko Gaza wakati wa duru hii ya uhasama, imesema ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu OCHA.

Wapalestina 704 wakiwemo watoto 305 waliuawa, na kufanya jumla ya vifo katika eneo hilo kufikia 5,791 kulingana na wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas.