Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya UN yakaribisha hatua ya msaada kuingia Gaza

UNICEF na wafanyakazi wa misaada wanapakia vifaa vya kibinadamu kwenye lori kwenye kivuko.
UN Photo/Eskinder Debebe Misaada ya kibinadamu ikiwa imepakiwa tayari karibu na mpaka wa Rafah Misri

Mashirika ya UN yakaribisha hatua ya msaada kuingia Gaza

Msaada wa Kibinadamu

Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths amekaribisha kuingia kwa msafara wa misaada huko Gaza leo Jumamosi, ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuanza kwa mapigano wiki mbili zilizopita kufuatia mashambulizi mabaya ya Hamas dhidi ya Israel.

Msafara wa malori 20 uliopitia mpaka wa Rafah na Misri unajumuisha vifaa vya kuokoa maisha vilivyotolewa na shirika la Hilali Nyekundu la Misri na Umoja wa Mataifa.

Bidhaa hizo zimeiidhinishwa kuvuka na kupokelewa na Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina, kwa msaada wa Umoja wa Mataifa.

Kupitia kwenye ukurasa wake wa X zamani ikijulikana kama Twitter bwana Griffis amesema "Nina imani kwamba ufikishaji huu wa misaada utakuwa mwanzo wa juhudi endelevu za kutoa vifaa muhimu ikiwa ni pamoja na chakula, maji, dawa na mafuta kwa watu wa Gaza, kwa njia salama, inayotegemewa, isiyo na masharti na isiyozuiliwa." 

Janga la kibinadamu

Uingizaji huu wa misaada wa leo Jumamosi unafuatia siku za mazungumzo ya kina na makali na pande zote husika ili kuhakikisha kuwa shughuli ya msaada zinaanza tena haraka iwezekanavyo na kwa masharti yanayofaa.

Kivuko cha mpaka cha Rafah ndicho pekee kilichofunguliwa na Gaza, na mamia ya malori yamekuwa yakingoja huko kuingiza msaada wa chakula, maji, madawa na vitu vingine muhimu kwenye eneo hilo, ambapo vifaa vya msingi vinakwisha.

Bwana Griffiths amesema hali ambayo tayari ni hatari ya kibinadamu huko Gaza "imefikia viwango vya janga tangu uadui uanze, na ni muhimu kwamba misaada ifikie watu wanaohitaji popote walipo kote Gaza, na kwa kiwango sahihi. Watu wa Gaza wamevumilia mateso ya miongo kadhaa. Jumuiya ya kimataifa haiwezi kuendelea kuwaangusha." 

Mkombozi huku kukiwa na uhaba mkubwa

Kivuko cha Rafah ndicho pekee kilichofunguliwa na Gaza, na mamia ya malori yamekuwa yakingoja huko kuleta chakula, maji, vifaa vya matibabu na vitu vingine muhimu kwenye eneo hilo, ambapo vifaa vinaisha.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus pia ametangaza kwamba vifaa vya matibabu kutoka kwa shirika hilo vimevuka mpaka "lakini mahitaji ni makubwa zaidi."

Akiandika kwenye ukurasa wake wa X, mkuu wa WHO amesisitiza haja ya kupita kwa usalama kwa misafara ya ziada, ulinzi wa wafanyakazi wote wa kibinadamu, na upatikanaji endelevu wa misaada ya afya.

Katika taarifa yake, WHO imesema kuwa hospitali ndani ya Gaza tayari zimefikia hatua mbaya kutokana na uhaba na upungufu wa dawa na vifaa vya matibabu, ambayo ni njia ya kuendelea kuishi kwa watu waliojeruhiwa au wale wanaopambana na magonjwa sugu na mengine.

Chakula kiko njiani

Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa Duniani WFP limesema malori matatu yaliyobeba tani 60 za chakula cha dharura yalikuwa kwenye msafara huo. 

Vifaa hivyo ni pamoja na samaki jodari wa makopo, unga wa ngano, tambi, maharagwe ya makopo na nyanya za makopo.

"Chakula hiki kinahitajika sana kwani hali ndani ya Gaza ni mbaya sana," amesema Mkurugenzi Mtendaji wa WFP, Cindy McCain. 

Akiangazia hitaji la kuendelea na ufikishaji salama wa msaada , amesema malori 20 yalikuwa katika "hatua muhimu ya kwanza, lakini msafara huu unapaswa kuwa wa kwanza kati ya mingi."

WFP ina tani nyingine za nafaka 930 za vyakula vya dharura katika au karibu na mpaka wa Rafah, tayari kwenda wakati wowote watakaporuhusiwa tena. 

Hifadhi hizi zinahitajika ili kujaza vifaa vya wakala vinavyopungua kwa kasi ndani ya Gaza.

Tangu kuanza kwa mzozo huo, WFP imetoa msaada kwa takriban watu 520,000 na inapanua operesheni zake ili kusaidia watu milioni 1.1 katika miezi miwili ijayo. Msaada huu unajumuisha mikate safi inayotolewa kila siku kwa watu waliokusanyika katika makazi ya Umoja wa Mataifa katika maeneo ambayo ufikishaji msaada unaruhusiwa.

Suala la uhai au kifo

WFP hutoa unga kwa viwanda vya kuoka mikate vilivyo na mkataba, ambavyo vinazalisha mikate kwa ajili ya kusambazwa. 

Lakini, ukosefu wa nishati na mafuta umelazimisha kampuni nyingi za kuoka mikate kuacha kufanya kazi, na moja ilishambuliwa Jumatano.

Zaidi ya chupa 44,000 za maji ya kunywa pia zilikuwa kwenye msafara huo, ambazo zinatosha watu 22,000 tu kwa siku moja, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF) limesema.

Kwa mujibu wa Catherine Russell, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hiloa. "Kwa watoto milioni moja huko Gaza sasa wanaokabiliwa na ulinzi muhimu na mgogoro wa kibinadamu, utoaji wa maji ni suala la maisha au kifo. Kila dakika ni muhimu."

Usafirishaji huo wa msaada maji ni tone tu la mahitaji makubwa huko Gaza, ambapo sehemu kubwa za miundombinu muhimu, pamoja na mifumo ya maji na mifereji ya maji taka, imesambaratishwa na kuwa vifusi.

UNICEF imesema uwezo wa maji uko katika asilimia tano ya viwango vya kawaida, na wakazi wa Gaza karibu milioni 2.3 sasa wanaishi kwa lita tatu za maji kwa kila mtu kwa siku.

Kulinda kila mtoto

Takriban watu milioni moja wameyakimbia makazi yao, karibu nusu yao wakiwa ni watoto, wengi wao wakiwa katika makazi yenye msongamano mkubwa wa watu ambapo upatikanaji mdogo wa maji, usafi wa mazingira na usafi unaweka maisha yao katika hatari ya milipuko ya magonjwa.

Bi. Russell amesisitiza haja ya kuwalinda watoto na wahudumu wa kibinadamu wapate fursa salama wy kuwafikia wahitaji na familia zao.

Ameongeza kuwa "Zaidi ya yote, pande zote lazima zilinde bila masharti kila mtoto dhidi ya madhara na kuwapa ulinzi maalum ambao wanastahili, kwa mujibu wa chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu." 

UNICEF imependekeza vifaa vya ziada vya dharura kwa hadi watu 250,000 kwenye kivuko cha Rafah ambapo inaweza kuletwa Gaza baada ya saa chache, na misaada zaidi iko njiani.