Udadavuzi: Ndani ya msafara wa misaada katika kivuko cha Rafah Gaza
Udadavuzi: Ndani ya msafara wa misaada katika kivuko cha Rafah Gaza
Mamia ya malori yanasubiri ruksa kwenye mpaka wa Rafah nchini Misri, yakiwa tayari kupeleka msaada wa kuokoa maisha kwa watu milioni 2.3 waliozingirwa katika Ukanda wa Gaza.
Kuna nini ndani ya malori?
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amewaambia waandishi wa habari kwamba hivi sasa, mlori hayo yanahitaji haraka kuhamia upande wa pili wa mpaka ikiwa ni suala la Uhai na kifo.
Hali inayoendelea ya kuzingirwa Gaza iliyowekwa muda mfupi baada ya kuzuka mzozo kuanza tarehe 7 Oktoba imesababisha mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wake kukibizana kutuma tani za vifaa vya msaada.
Mashirika katika eneo hilo yanaripoti kuwepo viwango vya chini vya mahitaji ya msingi, kama vile chakula na maji huku kukiwa na mashambulizi ya anga na mabomu yanayoendelea.
UN News imeangalia upya kile kilicho ndani ya msafara wa malori yanayosubiri mpakani. Hiki ndicho tulichobaini:
Maji
Malori yaliyosheheni maji ya kunywa ya chupa pekee ni sehemu ya msafara huo. Hii inajumuisha shehena nyingi, huku kila lori likiwa limepakia chupa 5,544 za maji, kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF.
Maji yanaendelea kuwa miongoni mwa bidhaa zenye thamani kubwa, kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la kutoa misaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, linalofanya kazi Gaza na Ukingo wa Magharibi.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaonya kwamba mgao wa kila siku huko unaweza kushuka hadi lita moja kwa kila mtu, ikilinganishwa na kiwango cha chini cha lita 15 kwa siku.
Pia yameonyesha wasiwasi mkubwa juu ya kuzuka kwa magonjwa yanayotokana na maji.
Wakati shehena zikiwa tayari kupelekwa Gaza, shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu, na masuala ya dharura OCHA, limekuwa likifanya kazi ya kukagua vifaa zaidi kwa ajli ya shughuli za usafirishaji wa maji.
Chakula
Tayari kwa kupelekwa Gaza ni tani 951 za chakula cha dharura, kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani WFP.
Ili kupima kiasi, msafara wa malori matano umebeba pamoja na mambo mengine, tani 100 za vifurushi vya chakula.
Hiyo ni takriban tani 20 za chakula kwenye kila lori. Magari mengine yana misaada mingine ya ziada ya vyakula vilivyo tayari kuliwa vinavyoendelea kuwasili.
Shehena hizo za WFP zina mahitaji mbalimbali, ikiwa ni pamoja na tani 300 za chakula ambacho kinaweza kulisha watu 250,000 kwa wiki moja, tani 22 za misaada ya kibinadamu, tani 15 za biskuti, na vitengo viwili vya kuhifadhi vitu ili kukabiliana na uhaba huko Gaza. Shirika hilo pia lilipanga kutoa tani 40 za vifurushi vya chakula vilivyotolewa Msaada na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Makazi
Mapigano yanayoendelea yamewakosesha makazi Wagaza milioni moja, hii ni takriban nusu ya idadi ya wananchi wa eneo hilo. Amri iliyotolewa na Israel ya kuwahamisha raia wa Gaza kuelekea maeneo ya kusini mwa Gaza ilisababisha watu wengi hivi sasa kulala mitaani huku kukiwa na mashambulizi ya mabomu.
Huku maelfu ya raia wakingoja upande wa pili kufunguliwa kwa mpaka wa Rafah na wengine wengi wakihitaji misaada ya kibinadamu, wasaidizi wa kibinadamu walisafirisha bidhaa mbalimbali kusaidia kuwahudumia na kuwapa vitu muhimu tu.
Vitu hivyo vinajumuisha tani 15 za turubai, zilizotumwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) na vifaa vya dharura 300,000 vyenye vitu muhimu kutoka OCHA.
Ili kuhudumia mahitaji ya wasichana na wanawake, shirika la Umoja wa Mataifa la afya ya uzazi na idadiya watu, UNFPA, lilituma vifaa 3,000 vya kujihifadhi vikiwa na miongoni mwa mambo mengine, pedi za hedhi, sabuni ya kuogea, jozi nyingi za chupi, sabuni za kufulia, tochi, dawa ya meno na miswaki.
Pia ziko tayari shehena za UNICEF za vyoo vinavyohamishika, na vifaa vya kujihifadhi kwa ajili ya kusaidia mahitaji ya haraka ya watu 150,000.
Afya
Baadhi ya malori kwenye mpaka wa Rafah yamebeba vifaa vya matibabu vya kuokoa maisha. Tangu tarehe 7 Oktoba, mashirika ya Umoja wa Mataifa yananukuu mamlaka huko Gaza ambapo wameripoti takriban vifo 4,000 na maelfu zaidi ya majeruhi.
Agizo la wananchi kuhama limezidisha hali mbaya Zaidi kwa mfumo wa afya ambao tayari ni dhaifu, kuzidiwa, na ulioharibika, huku vifaa tiba vikiwa vinapungua kwa kasi katika eneo lote.
Miongoni mwa viongozi wa kwanza wa mashirika ya Umoja wa Mataifa kufika kwa Rais wa Misri ili kuwezesha utoaji wa misaada, alikuwa ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus ambaye alisema shehena ya awali ya mita za ujazo 78 za msaada wa dharura itasaidia zaidi ya Wapalestina 300,000.
Shehena za mizigo katika mpaka wa Raha zina dawa mbalimbali ikiwemo za kiwewe, vifaa vya afya, na bidhaa za matibabu za dharura za kuwatibu waliojeruhiwa. Kwa kuongezea, WHO nchini Misri imepokea nyongeza ya tani tisa za vifaa vya dharura vya kiwewe.
Mafuta
Baadhi ya malori yanayosubiri kibali Rafah yamebeba makontena ya mafuta yanayohitajika sana.
Kwa karibu wiki mbili, wahudumu wa wa misaada ya kibinadamu katika eneo la Gaza wameonya juu ya uhaba wa mafuta.
Kuzingirwa kunaoendelea kulisababisha kukatwa kwa maji, umeme, na huduma zingine muhimu, kwa hivyo jenereta sasa zinasambaza nishatiu.
Mafuta yanahitajika kwa dharura ili kuwawezesha kuhudumia hospitali, mitambo ya kuondoa chumvi, na pampu za maji, kulingana na mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa.
Je, misaada inafikaje kwenye kivuko cha Gaza?
Kabla ya mzozo wa sasa, malori 100 yalikuwa yakiingia katika eneo hilo kila siku kwa sababu zaidi ya asilimia 60 ya watu walitegemea msaada wa UNRWA. Hakuna usafirishaji wowote wa misaada ambao umefika tangu tarehe 7 Oktoba, kulingana na UNWRA.
Huku vivuko vya Israel vya Erez na Kerem Shalom kuingia Gaza vimefungwa tangu mzozo huo uanze, mpaka wa Rafah ndio mkuu wa Umoja wa Mataifa aliouita kitovu cha uhai kwa wakazi waliozingirwa.
Ili kuwezesha usafirishaji, Huduma ya usafiri wa anga ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya masuala ya kibinadamu UNHAS imepanga safari za ndege zenye mamia ya tani za msaada hadi uwanja wa ndege wa El Arish nchini Misri, ulioko kilomita 45 sawa na maili 28 kutoka kivuko cha Rafah.
Wiki iliyopita, Misri, Jordan, Uturuki, na Umoja wa Falme za Kiarabu wamekuwa miongoni mwa wafadhili pamoja na kuongezeka kwa idadi ya mashirika mengine ya kibinadamu.
Leo Ijumaa, vifaa vinaendelea kuwasili. Makasha yanaendelea kupakiwa kwenye malori zaidi yanayosubiri. Kisha madereva wamnaelekea kwenye msafara wa kusubiri huko Rafah, ambapo watakuwa tayari hadi makubaliano ya kufungua mpaka yafikiwe.