Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Misaada, misaada na misaada iingie Gaza ndio ombi letu: UN

Umati wa Wapalestina unakusanyika kupinga, huku mtu mmoja mbele akiwa ameshika bango linalosomeka 'DUNIA AMKA! CNN AMKA!' na mtu mwingine juu ya lori akipeperusha bendera.
UN Photo/Eskinder Debebe Waandamanaji wanatoa maoni yao katika kivuko cha Rafah kuingia Gaza.

Misaada, misaada na misaada iingie Gaza ndio ombi letu: UN

Msaada wa Kibinadamu

Umoja wa Mataifa leo umeendelea kusisitiza ombi la kuhakikisha misaada inaruhusiwa kuingia Gaza kuokoa Maisha ya maelfu kwa maefu ya watu wenye uhitaji.

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR katika taarifa yake iliyotolewa mjini Geneva Uswisi imesema kukiwa na Zaidi ya watu 3,700 wameuawa Gaza na wengine 1,000 wanadhaniwa kufukiwa chini ya vifusi, pamoja na watu 1,300 waliouawa nchini Israel, na Wapalestina milioni moja zaidi ambapo  nusu yao ni watoto  wameripotiwa kuhama makwao, tunaziomba pande zote katika mzozo kuruhusu kupitishwa haraka na bila vikwazo kwa misaada ya kibinadamu kwa raia wote wenye uhitaji popote walipo. Wakati huo huo, tunasalia na hofu kubwa kwamba mashambulizi makubwa ya vikosi vya Israeli yanaendelea kote Gaza, ikiwa ni pamoja na kusini.

Ofisi hiyo imeongeza kuwa mashambulizi hayo, pamoja na hali ngumu ya maisha katika eneo la kusini, inaonekana kuwasukuma wengine kurejea kaskazini, licha ya kuendelea kwa mashambulizi ya mabomu huko. 

Pia tuna wasiwasi kuhusu kuendelea kurushwa kwa maroketi ya kiholela kutoka Gaza hadi Israel. Na tunasisitiza kwamba raia wote waliokamatwa na kushikiliwa na makundi yenye silaha ya Palestina lazima waachiliwe mara moja na bila masharti. Kuchukua mateka ni marufuku chini ya sheria za kimataifa.

Ongezeko la ukiukwaji wa haki za binadamu 

Ofisi hiyo ya haki z binadamu imeendelea kusema kwamba inasikitishwa sana na kuzorota kwa kasi kwa hali ya haki za binadamu katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na ongezeko la hatari la matumizi haramu ya nguvu. 

Tangu tarehe 7 Oktoba, Ofisi yetu imepokea ripoti kwamba Wapalestina 69, wakiwemo angalau watoto 15 na mwanamke mmoja, wameuawa na vikosi vya usalama vya Israel katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu. Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu, Volker Türk, amesisitiza kwamba ni muhimu sana pande zote lazima ziheshimu sheria za kimataifa za haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu. Katika mwenendo wa uhasama, kanuni za ulazima, tofauti, uwiano na tahadhari katika mashambulizi lazima ziheshimiwe wakati wote na kila mtu”.

Mfanyakazi wa misaada UN aliyevaa fulana ya bluu akiwagawia maji wanawake wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.
© UNRWA Umoja wa Mataifa unaendelea kusaidia wapalestina walionasa kwenye mapigano yanayoendelea Ukanda wa Gaza, Mashariki ya Kati

Wafanyakazi wa UNRWA wanaendelea kupoteza maisha

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA  limesema wafanyakazi wake wanaojitoa kwa hali na mali wanaendelea kupoteza Maisha katika mzozo unaoendelea huko Gaza.

Kupitia taarifa ya shirika hilo iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi wafanyakazi wengine wawili wa UNRWA wamethibitishwa kuuawa katika Ukanda wa Gaza na kufanya idadi hiyo kufikia 16 tangu vita kuanza. 

UNRWA imesema inaendelea kutetea katika ngazi za juu upatikanaji endelevu na usiozuiliwa wa kibinadamu kwa vifaa vinavyohitajika sana, ikiwa ni pamoja na mafuta, chakula, maji na madawa, kuingia katika Ukanda wa Gaza. 

UNRWA pia inaendelea kutetea uzingatiaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu na ulinzi wa raia, miundombinu ya kiraia na vifaa vya Umoja wa Mataifa. 

Makazi ya UNRWA, ambayo yanahifadhi zaidi ya watu nusu milioni, yamejaa watu wengi, hasa kusini mwa Gaza na baadhi ya waliokimbia makazi yao wameripotiwa kuanza kurejea katika maeneo mengine.