Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada uko tayari kuingia Gaza ruksa tu ndiyo inayosubiriwa :UN

Lori la maji UNICEF lililoandikwa 'WATER-0801' linasambaza maji ya kunywa kwa umati wa wanaume, wanawake, na watoto katika jimbo la Rafah la Ukanda wa Gaza.
© UNICEF/Eyad El Baba Maji ya kunywa yakigawiwa kwa wakazi na wakimbizi wa ndani Rafah Kusini mwa Ukanda wa Gaza

Msaada uko tayari kuingia Gaza ruksa tu ndiyo inayosubiriwa :UN

Msaada wa Kibinadamu

Leo angalau kuna matumaini huko Gaza ambako wahudumu wa misaada ya kibinadamu wanaendelea kusubiri ruksa kwa hamasa kubwa kuingiza misaada ya kuokoa maisha kufuatia ripoti za makubaliano yaliyosimamiwa na Rais wa Marekani ya kuingiza Gaza malori 20 ya misaada kupitia mpaka wa Misri umesema leo Umoja wa Mataifa. 

Tani 3,000 za vifaa zimekuwa zikisubiri kuingia upande wa Misri wa kivuko tangu Jumamosi ambapo shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa WFP limesema liko tayari kusambaza msaada huo.

Mkuu wa UN yuko Cairo Misri

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewasili leo Cairo Misri kutekeleza juhudi zake za kidiplomasia, kufuatia wito wake wa "kusitisha mapigano mara moja" kufuatia mashambulizi katika Hospitali ya Al Ahli Arab katika mji wa Gaza siku ya Jumanne, ambayo yaliua watu 471 kulingana na mamlaka ya Gaza.

Nchini Misri atakutana na uongozi wa nchi na leo atakuwa na mazungumzo na Waziri wa mambo ya nje  Sameh Shoukry na kisha atakuwa na mkutano na waandishi wa habari.

Kesho Ijumaa anatarajiwa kuzuru uwanja wa ndege wa Al-Arish, kituo cha Umoja wa Mataifa cha masuala ya kiufundi na Jumamosi atakutana na kivukocha mpaka wa Rafah na Jumamosi atakutana na Rais wa Misri Abdel Fattah Al Sisi 

Familia za wakimbizi zinatembea kupitia barabara iliyojaa mabomoko katika kitongoji cha Tal al-Hawa kusini mwa Ukanda wa Gaza.
© UNICEF/Eyad El Baba Familia zikikimbia kutoka kwenye makazi ya muda ya Tal al- Hawa kwenda kupata hifadhi Kusini mwa Gaza

Maisha ya watu yako hatarini

Akizungumzia habari za makubaliano yaliyofikiwa na Marekani, mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amekaribisha uamuzi huo akisema "uongozi wa Marekani na makubaliano ya Israel ya kuruhusu chakula, maji na misaada ya matibabu kuingia katika eneo lililofungwa kupitia kivuko cha mpaka cha Rafah, ni muhimu sana” akisisitiza kupitia kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kwamba "maisha ya watu wengi yanategemea hilo kufanyika.”

Akitoa taarifa kwa Baraza la Usalama siku ya Jumatano, mkuu wa misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths alisisitiza haja ya wahudumu wa kibinadamu kuweza "kufikisha misaada kwa raia wanaohitaji msaada huo kote Gaza, bila vikwazo, katika maeneo watakayochagua, katika maeneo ambayo wanajiona kuwa salama na pale ambapo tunaweza kutafuta kuhakikisha usalama huo.”

Aliwaambia wajumbe kuwa karibu lori 100 za vifaa vya kibinadamu kwa siku zinahitajika ili kukidhi mahitaji ya wakazi zaidi ya milioni mbili wa eneo lililozingirwa.

Kulingana na duru za habari, vifaa vimetumwa kukarabati mashimo kwenye kivuko muhimu cha Rafah ili kuruhusu msafara wa misaada ya awali kuingia. Zaidi ya malori 100 yanasubiri ruksaya mwisho upande wa Misri ili kuingia Gaza.

Israel imesema itaruhusu msaada mdogo ndani ya eneo hilo endapo hakuna hata mmoja utakaonufaisha Hamas, ambayo inadhibiti Gaza.

Mvulana mdogo wa Kipalestina aliyevaa shati la bluu akipokea mfuko mkubwa wa mkate kutoka kwa mfanyakazi wa WFP wakati wa hafla ya usambazaji wa chakula shuleni huko Gaza.
© WFP/Ali Jadallah Mvulana akipokea msaada wa mkate kutoka WFP kwenye makazi ya muda huko Gaza

Hali ni mbaya

Idadi kubwa ya watu wa Gaza imekuwa ikikabiliwa na hali ni mbaya zaidi,hasa kutokana na kukatika kwa umeme tangu Oktoba 11, kuongezeka kwa uhaba wa chakula na mfumo wa afya ukiwa ukingoni kuporomoka.

Kulingana na shirika la kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura la Umoja wa Mataifa OCHA, wastani wa matumizi ya maji kwa mahitaji yote, ikiwa ni pamoja na kunywa, kupika na usafi inakadiriwa kuwa ni lita tatu tu kwa siku kwa kila mtu huko Gaza. 

OCHA pia imeonya kwamba watu hutumia maji kutoka vyanzo visivyo salama "hivyo kuhatarisha kifo na kuweka watu hao katika hatari ya kuzuka kwa magonjwa ya kuambukiza".