Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ongezeko la wakazi wa mijini ni fursa kwa wenye maeneo ya kulima bustani

Lucas Malembo akimwagilia mboga katika shamba la mjini nchini Tanzania kwa kutumia kopo la kumwagilia.
UN News Mkurugenzi wa Taasisi ya Malembo Farm, Lucas Malembo.

Ongezeko la wakazi wa mijini ni fursa kwa wenye maeneo ya kulima bustani

Tabianchi na mazingira

Zaidi ya nusu ya uso wa dunia imeundwa na maji, maji hayo yanatumika kama chakula, nishati na yanasaidia jamii kustawi lakini watu wengi hawana kabisa rasilimali hii adhimu, huku wengine wanayachukulia kawaida.


 

Soundcloud

Maji ni uhai, Maji ni chakula ndio kauli mbiu ya mwaka 2023 katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya chakula dunia iliyochaguliwa mahususi kuhimiza jamii kutunza maji kwa mustakabali endelevu wa ulimwengu hususan wakati huu dunia ikikabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Wakati idadi ya watu duniani ikiwa bilioni 8 na inaendelea kuongezeka, shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO limekumbusha kuwa maji ni rasilimali yenye mwisho hivyo jamii inapaswa kuichukulia kwa umuhimu mkubwa.

Kupitia wavuti wake FAO imependekeza namna makundi mbalimbali ndani ya jamii yanavyoweza kusaidia katika utunzaji maji kwa mustakabali wa ulimwengu mzima. Makundi hayo ni pamoja na serikali, asasi za kiraia, wasomi, wanafunzi, wafanyabiashara na wakulima,

Katika kundi la wakulima FAO inapigia chepuo ukulima unazingatia matumizi ya maji kwa ufanisi, kutotupa chakula, kupunguza upotevu wa maji na njia nyingine nyingi.

Lucas Malembo na mhitimu Ilakiza Jackson wakichunguza mimea kwenye chafu katika Taasisi ya Shamba la Malembo nchini Tanzania.
UN News Mkurugenzi wa Taasisi ya Malembo Farm, Lucas Malembo na Mmoja wa wahitimu wa mafunzo ya kilimo cha kisasa kutoka Malembo Farm Academy Ilakiza Jackson.

Ukulima wa kisasa

Ukulima wa kisasa hususani mijini umeelezwa kuchangia si tu upatikanaji wa chakula bali pia unatumia maji kidogo na wakazi waishio mijini wanahimizwa kujihusisha na kilimo kwani kinafaida nyingi za kiafya, kiuchumi na kimazingira.

Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa Mkurugenzi wa Taasisi ya Malembo Farm, Lucas Malembo amesema katika ulimwengu wa sasa ambao dunia inapambana na athari za mabadiliko ya tabianchi na changamoto za kiuchumi wananchi wanaweza kujipatia chakula kwa kutumia eneo dogo na kwa gharama nafuu pamoja na kuuza ziada ya kile walicholima na kujipatia kipato. 

“Hapa nchini Tanzania katika miaka 30 iliyopita idadi ya watu mijini imeongezeka kwa asilimia 40 tafsiri yake ni kuwa kilimo cha mjini kinaenda kushika kasi ili kukidhi mahitaji ya wakazi wake.” Amesema Bwana Malembo

Tafiti zinaonesha kuwa kwa siku mtu mmoja anahitaji kutumia lita 4-6 za maji lakini uzalishaji wa chakula cha mtu mmoja kwa siku unahitaji lita za maji takribani 3,000 kiwango ambacho ni kikubwa katika ulimwengu wa sasa ambao maeneo mengi yanakabiliwa na ukame uliosababishwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ni kutokana na hali hiyo ndio maana Malembo anaunga mkono wito wa FAO wa matumizi bora ya maji akitolea mfano kilimo cha nyanya “Kuzalisha kilo moja ya nyanya kwa njia ya kawaida Unahitaji kutumia lita 400 lakini kwa kutumia teknolojia ya kisasa utahitaji kutumia lita 70 tu za maji kwahiyo utaona unaokoa maji kiasi gani kwahiyo kilimo cha mjini kimekuwa ni suluhisho la kupunguza matumizi ya maji.”

Malembo anahitimisha mahojiano ya Idhaa ya Kiswahili kwa kueleza kuwa kwa uzoefu wake wa shuguli za kilimo, ukulima wa kisasa una tija kwa mkulima mara 3 mpaka 10 ya mtu anayefanya kilimo cha kawaida.

Ilakiza Jackson hutunza mimea ya lettuce kwenye chafu katika Chuo cha Malembo Farm nchini Tanzania.
UN News Ilakiza Jackson, mmoja wa wahitimu wa mafunzo ya kilimo cha kisasa kutoka Malembo Farm Academy.

Vijana limeni

Taasisi hiyo ya Malembo Farm inatoa mafunzo ya kilimo cha mijini kwa rika zote ikiwemo vijana na watoto.

Mmoja wa wahitimu wa mafunzo ya kilimo cha kisasa kutoka Malembo Farm Academy Ilakiza Jackson anasema mbali na kupata faida ya mbogamboga na matunda lakini kilimo cha mjini kinafaida kiafya sababu mkulima hatumii mbolea za kemikali.

“Katika masomo yangu nimejifunza kulima kwa kutumia mbolea ya mboji, ambayo inatokana na mabaki ya chakula na mbolea hii inasaidia shamba lako la nyumbani mazao yaote vizuri na unapata chakula chenye virutubisho visivyo na mbolea za viwandani ambazo pengine zinaweza kuwa na athari hasi katika mazingira yetu.” Amesema Bi. Jackson

Muhitimu huyo amewashawishi vijana wenzake kujikita katika ukulima wa mjini. “Kama unajiuliza utaanzaje kilimo cha mjini ni rahisi, unaweza kuchukua makopo na ukawa unapanda mboga mboga na kama una nafasi kubwa kidogo hapo nyumbani kwako ni vizuri ikianzisha shamba dogo.”

Akieleza mafanikio yake mpaka sasa Ilakiza Jackson ameeleza kwa sasa anaweza mbali na kujua mbinu mbalimbali na aina tofauti za kilimo cha mjini lakini pia anaweza kutengeneza mbolea ya mboji na imemrahisishia katika kilimo chake cha mjini na haingii gharama ya kununua mbolea za viwandani.