Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Udadavuzi: Kuna nini ndani ya msafara wa misaada kwenye kivuko cha Gaza

Lori la UNICEF lililojaa chupa za maji linaendesha gari kwenye barabara kuu kuelekea Gaza.
© UNICEF/Mohamed Ragaa Lori likiwa limejaa chupa za maji ya kunywa likielekea Al Arish mji ulio kilometa 32 kusini mwa mpaka wa Gaza

Udadavuzi: Kuna nini ndani ya msafara wa misaada kwenye kivuko cha Gaza

Msaada wa Kibinadamu

Chini ya kilomita moja kutoka Gaza, vibao vya kuengeshean chakula, mafuta, maji, na dawa ni miongoni mwa mamia ya tani za misaada ya kuokoa maisha iliyopakiwa kwenye msafara mrefu wa malori yakiwa yamesimama kwenye upande wa Misri wa kivuko cha mpakani ch a Rafah, huku madereva wakisubiri ruksa ya Israel ili waweze kufikia Wapalestina milioni 2.3 waliozingirwa na walionaswa katika mzozo wa vita vinavyoendelea.

Tweet URL

Huku wahudumu wa kibinadamu wakiendelea kurejea wito wa haraka wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Israel kufungua njia salama ya kufikisha misaada, wakisema Gaza hivi karibuni itakosa vifaa vya msingi, kulingana na mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyoko kwenye eneo hilo, ambayo yameelezea wasiwasi kuhusu janga la kibinadamu ambalo halijawahi kushuhudiwa.

 Hakuna mifuko ya kutosha ya kufungia maiti-UNRWA

Muda mfupi baada ya kuzuka kwa ghasia tarehe 7 Oktoba, Israel ilifunga mipaka yote na Gaza, na Umoja wa Mataifa haujaweza kujazia akiba yake ya misaada ya kuokoa maisha tangu wakati huo. 

Wakati bidhaa zinaendelea kupungua katika eneo hilo kukiwa na mashambulizi kila siku, mashirika ya Umoja wa Mataifa, wadau, na mataifa yameharakisha kupeleka misaada.

Hivi ndivyo vilivyo kwenye msafara huo

Mambo muhimu 

Mwishoni mwa juma, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa El Arish wa Misri, ambao kwa kawaida huhudumia Wapalestina wanaosafiri kwenda Mecca, Saudi Arabia, kwa ajili ya Hija ya kila mwaka, umekuwa mzinga wa shughuli za kibinadamu.

Mamia ya tani za bidhaa muhimu, kuanzia chakula kilicho tayari kuliwa hadi glavu za mpira kwa ajili ya upasuaji wa dharura, vilitua katika ndege iliyotumwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa, wadau, na mataifa, ikiwa ni pamoja na Jordan, Uturuki, na Umoja wa Falme za Kiarabu, katika uwanja huo wa ndege, uliopo kilometa 45 au maili 28 kutoka mpaka wa Gaza.

Michango inayohitajika sana mepakuliwa na kuhamishiwa kwenye malori yaliyo mpakani. 

Kilichoongezwa kwenye msafara huo ni mchango wa Misri wa lori 100 zilizobeba tani 1,000 za msaada.

Zinajumuisha msaada wa mashirika ya Umoja wa Mataifa wa mahema, mablanketi, na dawa za aina mbalimbali.

Ukanda wa Gaza kabla ya kupanda kwa kasi kwa sasa, kuonyesha mipaka yake na Israeli, Misri, na Bahari ya Mediterania, na vivuko muhimu vya mpaka na vituo vya ukaguzi.
© UNOCHA Ukanda wa Gaza kabla ya machafuko ya sasa

Aidha, OCHA imeripoti mipango ya kuwapa watu 300,000 vifaa vya dharura vyenye mahitaji muhimu, na shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi UNFPA, limekuwa na vifaa tayari vya usafi na kujisafi kwa wanawake, ikiwa ni pamoja na vifaa 3,000 vya hedhi.

Karibu na msafara wa misaada, ripoti za vyombo vya habari zinasema zimeshuhudia safu za magari ya kubeba wagonjwa na wahudumu wa afya ya dharura wakisubiri kuwahudumia watu wa Gaza waliojeruhiwa.

Wafanyakazi wa WHO na Hilali Nyekundu wamesimama kwenye lami ya uwanja wa ndege karibu na ndege ya mizigo iliyojaa vifaa vya afya nchini Misri.
© WHO Vifaa vya matibabu kutoka shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO kwenye kituo chake cha Dubai vikiwasili Misri

Vifaa vya matibabu

Ndege iliyosheheni vifaa vya matibabu ilitumwa na shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO ili kujazia hifadhi yake iliyokuwa imepangwa hapo awali huko Gaza, ambayo imepungua na kufikia katika viwango vya chini vya hatari. Katika siku zilizopita, WHO ilituma shehena mbili kutoka katika kituo chake cha usafirishaji huko Dubai.

Moja ilitua Beirut, Lebanon, ikiwa imebeba dawa za upasuaji na za kiwewe na vifaa vya kuwahudumia wagonjwa 800 hadi 1,000 waliojeruhiwa, wakikabiliana na mahitaji yanayoongezeka wakati mapigano yakizidi katika mpaka na Israel.

Mwanamume aliyevaa shati jekundu amesimama kwenye ghala huku gari la kubebea mizigo likipakia godoro za vifaa vya msaada UNICEF , ikiwa ni pamoja na dawa na vimiminika vya IV, kwa ajili ya kupelekwa Gaza.
© UNICEF/Mohammad Ajjour Vifaa vya matibabu ambavyo tayari vilikuwa Gaza vinagawiwa na shirika la UNICEF

Hiyo ilifuatia uwasilishwaji wa mwishoni mwa wiki wa mita za ujazo 78 za msaada wa dharura kwenye uwanja wa ndege wa El Arish, ambavyo ni vifaa vya kutosha kusaidia zaidi ya Wapalestina 300,000. 

Ili kusaidia kupata fursa ya kuwafikia walengwa kupitia eneo la mpaka wa Rafah, mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus alikutana wiki iliyopita na Rais wa Misri Abdel Fattah El-Sisi, ambaye alikubali ombi lake.

Kila saa ambayo shehena hii inasalia kwenye upande wa Misri wa mpaka wasichana na wavulana, wanawake na wanaume zaidi hususan walio hatarini au wenye ulemavu watakufa-Mkurugenzi Mkuu WHO

Shehena iliyo tayari kusafirishwa ina vitu muhimu vya msingi vya kiafya pamoja na vifaa vya dharura. 

Vifaa hivyo ni pamoja na dawa za kiwewe za kutosha na vifaa vya afya kutibu wagonjwa 1,200 waliojeruhiwa na wagonjwa wengine 1,500 wanaosumbuliwa na magonjwa ya moyo, shinikizo la damu, kisukari, matatizo ya kupumua pamoja na mikoba ya majeraha tayari kutibu watu 235 waliojeruhiwa.

Chakula

Pia likikabiliana na uhaba, shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani (WFP) limetuma vifaa vya kujaza akiba yake iliyokaribia kuisha.

Mapema Jumatatu asubuhi, ndege iliyokodishwa na WFP ilitua katika Uwanja wa ndege wa El Arish, ikishusha tani 22 za msaada wa kibinadamu, ikiwa ni pamoja na tani 15 za biskuti zilizoimarishwa na sehemu mbili za kuhifadhi ili kukabiliana na uhaba huko Gaza, kulingana na shirika la kibinadamu la huduma za anga za Umoja wa Mataifa UNHAS.

Mwanamke aliyevaa gauni jekundu akiwapa chakula watoto watatu walioketi kwenye blanketi katika chumba kilichojaa watu katika Shule ya Al-Shati huko Gaza.
© UNICEF/Hassan Islyeh Chakula kinakwisha haraka sana Gaza

Shirika hilo la chakula la Umoja wa Mataifa lilianzisha operesheni ya dharura ya kupata chakula, maji, na vifaa vingine muhimu kwa Gaza na Ukingo wa Magharibi, na pia linasubiri malori matano yanayobeba, miongoni mwa mambo mengine, tani 100 za vifurushi vya chakula.

Maji na mafuta

Kwa siku ya tano mfululizo, eneo hilo lililozingirwa lilikuwa halina umeme na wakazi "wana upungufu mkubwa wa upatikanaji wa maji safi ya kunywa", kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Palestina, UNRWA, ambalo linafanya kazi Gaza na Ukingo wa Magharibi.

Ili kujiandaa kwa uwezekano wa kufunguliwa kwa upenyo wa kibinadamu kuingiza vifaa vya msaada katika Ukanda huo, timu ya mapema imetumwa Misri, kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya  UNRWA.

UNRWA imesema “Mafuta ni muhimu sana kwa mtambo wa kuondoa chumvi na vituo vya kusukuma maji”. 

Usafirishaji wa mafuta pia unangoja kujaza vifaa vinavyopungua haraka ambavyo vimetumika kuwasha jenereta za dharura, zikiwemo katika hospitali kote Gaza.

Watoto wa Kipalestina wakijaza kopo la manjano na maji kutoka kwenye bomba la umma huko Gaza.
© UNICEF/Mohammad Ajjour Kuna uhaba mkubwa wa maji katika ukanda mzima wa Gaza

Wakati huo huo, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF nchini Misri limetuma malori kwa shirika la Hilali nyekundu la Misri, mshirika wake nchini humo, ili kupanua wigo wa msaada wa UNICEF huko Gaza, pamoja na vitu muhimu kama vile maji, vyoo tembezi, na vifaa vya hedhi kushughulikia mahitaji ya haraka ya watu 150,000.

 Kilicho muhimu sana ni kuinua hali ya kuzingirwa, Umoja wa Mataifa unapaswa kuruhusiwa kuleta vifaa vinavyohitajika sana. - Msemaji wa UNRWA

Wakati huo, shirika la OCHA, linaandaa kituo chake cha huduma huko Rafah na mnyororo wa kutoka kutoka soko la ndani na hisa za shirika hilo, ukijumuisha mafuta, maji ya chupa, vifaa vya usafi, na matangi ya vifaa vya usafi, na matangi ya kuhifadhia maji. 

Shirika hilo lilikuwa likikagua na kuangalia shughuli za usafirishaji wa maji.

Wakati mzingiro ukiendelea, UNRWA haijaweza kuwasilisha vifaa tangu tarehe 7 Oktoba, kwa mujibu wa msemaji wa shirika hilo Juliette Touma. 

Wakati kukiwa na amri ya Israel ya kuwataka watu kuhama iliyotolewa mwishoni mwa juma, UNRWA ilihamisha kituo chake cha operesheni hadi kusini mwa Gaza, karibu na kivuko cha mpaka cha Rafah.

Ameongeza kuwa "Kilicho muhimu sana ni kuondoa hali ya kuzingirwa. Umoja wa Mataifa unapaswa kuruhusiwa kuingiza vifaa vinavyohitajika zaidi."