Jinamizi la hofu ya kifo limetanda Gaza, msaada lazima ufakikie wenye uhitaji:UN
Jinamizi la hofu ya kifo limetanda Gaza, msaada lazima ufakikie wenye uhitaji:UN
Martin Griffiths, mratibu wa masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa, ameonya leo kwamba” hofu ya kifo inatanda Gaza, na bila maji, umeme, chakula na dawa, maelfu watakufa."
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanatoa wito wa kuanzishwa kwa upenyo wa kibinadamu ili kufikisha misaada ya kuokoa maisha kwa watu wa Gaza.
Ndege zilizosheheni chakula kutoka shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa duniani WFP, zimewasili katika uwanja wa ndege wa Al-Arish wa Misri karibu na kivuko cha mpaka cha Rafah na Gaza.
Shirika hilo limesema timu zake zitatoa msaada wa dharura wa chakula kwa familia punde tu fursa ya kuingia kwa usalama kwa msaada wa kibinadamu itakapopatikana.
Ndege iliyobeba vifaa vya afya kutoka shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO, iliwasili katika uwanja wa ndege wa Al-Arish jana ili kufikishwa Gaza kupitia kivuko cha Rafah mara baada ya ukanda wa kibinadamu kuanzishwa ili kutoa msaada.
Shirika hilo limeonya kuwa kucheleweshwa kwa vifaa hivi katika upande wa mpaka wa Misri kungesababisha watu wengi zaidi kufariki huku vifaa vinavyoweza kuwaokoa vikiwa chini ya kilomita 20 sawa na maili 12.
Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA, limeripoti kuwa takriban watu milioni moja walikimbia makazi yao huko Gaza katika wiki moja iliyopita.