Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usawa ndani ya jamii utasaidia kupambana na athari za majanga

Madhara ya vimbunga sasa  ni dhahiri na sababu ni mabadiiko ya tabianchi na pichani Katibu Mkuu Antonio Guterres alipotembelea eneo la Codrington huko Antigua na Barbuda kuona hali halisi.
UN /Rick Bajornas
Madhara ya vimbunga sasa ni dhahiri na sababu ni mabadiiko ya tabianchi na pichani Katibu Mkuu Antonio Guterres alipotembelea eneo la Codrington huko Antigua na Barbuda kuona hali halisi.

Usawa ndani ya jamii utasaidia kupambana na athari za majanga

Tabianchi na mazingira

Leo ni Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Hatari ya Majanga ambapo mwaka huu siku hii inaadhimishwa kwa jamii kuhimizwa kushughulikia uhusiano kati ya majanga na ukosefu wa usawa kwani maafa na ukosefu wa usawa ni pande mbili za sarafu moja. 

Hii ni sawa na kusema kila dhiki huimarisha dhiki nyingine: upatikanaji usio sawa wa huduma huwaacha walio hatarini zaidi katika hatari ya majanga; huku athari za majanga zikizidisha ukosefu wa usawa na kuwasukuma walio hatarini zaidi katika umaskini.

Katika ujumbe wake wa siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema mwaka 2023 umeshuhudia kuongezeka kwa viwangov ya joto, ukame na mafuriko majanga ambayo yanaongeza umasikini na ukosefu wa usawa. 

“Wale wasionacho mara nyingi wako wako kwenye hatari kubwa kutokana na hali mbaya ya hewa. Wanaweza kuishi katika maeneo ambayo huathirika zaidi na mafuriko na ukame, na wana rasilimali chache za kukabiliana na uharibifu na kuweza kurejea katika hali yao ya awali.” Amesema Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa. 

Hali mbaya ya tabianchi Sudan Kusini inaharibu maisha ya baadhi ya watu walio hatarini zaidi duniani.
© UNICEF/Sebastian Rich
Hali mbaya ya tabianchi Sudan Kusini inaharibu maisha ya baadhi ya watu walio hatarini zaidi duniani.

Tuongeze ufahamu

Kwa kuwa nchi nyingi zilizo katika hatari kubwa ya maafa pia ni miongoni mwa nchi zilizo na idadi kubwa ya watu wanaoishi chini ya mstari wa kitaifa wa umaskini, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupunguza hatari za majanga UNDRR inahimiza watu kuchukua hatua ili kuondokana na mzunguko wa maafa na kuongezeka kwa ukosefu wa usawa.

UNDRR inahamasisha hatua zaidi kuchukuliwa ikiwemo kuongeza ufahamu juu ya ukatili wa ukosefu wa usawa na inatoa wito wa kupambana na ukosefu wa usawa kwa mustakabali thabiti, ambayo ndiyo kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu 2023.

Kaulimbiu ya Siku hii inawiana na Mfumo wa Sendai ambao ni makubaliano ya kimataifa ya kuzuia na kupunguza hasara za maisha, kiuchumi na miundombinu ya kimsingi. Mkataba huo una malengo saba ya kimataifa na viashiria 38 vya kupima maendeleo na unakamilisha Mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi, na mifumo yote miwili ikiunganishwa itasaidia kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs ifikapo mwaka 2030.

Katibu Mkuu Guterres amesema nchi lazima ziheshimu makubaliano ya Paris ili dunia iweze kufikia malengo ya maendeleo endelevu. “Lazima pia tukabiliane na ukosefu wa usawa katika ngazi ya kimataifa, kwa kutekeleza ahadi za kuwa na hazina ya Hasara na Uharibifu utakanao na athari za mabadiliko ya tabianchi katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi - COP28 na kuhakikisha kwamba kila mtu Duniani anafunikwa na mfumo wa tahadhari ya mapema ifikapo 2027.”

Maadhimisho hayo yanafanyika muda mfupi baada ya Mapitio ya Muhula wa Kati wa Mfumo wa Sendai wa Kupunguza Hatari za Maafa 2015-2030, ambapo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Mei 2023 lilipitisha tamko la kisiasa ili kuharakisha hatua za kuimarisha ustahimilivu wa majanga.

“Siku hii ya Kimataifa ya Kupunguza Hatari za Maafa hebu tuthibitishe dhamira yetu ya kuwekeza katika ustahimilivu na kukabiliana na hali, na kujenga mustakabali salama na wa haki kwa kila mtu, kila mahali”. 

Fuatilia kwenye mitandao ya kijamii matukio ya kuadhimisha siku hii kwa kufuata #DRRDay #UstahimilivuKwaWote #BreakTheCycle