Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi zatakiwa kufanya mageuzi kwenye sera na sheria kuhusu afya ya akili

Changamoto za afya ya akili katika maeneo ya kazi
WHO
Changamoto za afya ya akili katika maeneo ya kazi

Nchi zatakiwa kufanya mageuzi kwenye sera na sheria kuhusu afya ya akili

Afya

Ikiwa leo ni siku ya Afya ya Akili duniani chini ya kauli mbiu “Afya ya akili ni haki ya binadamu wote“ Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani- WHO na Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa -OHCHR wanazindua mwongozo mpya wakuzisaidia nchi kufanya mageuzi ya sheria ili kukomesha ukiukwaji wa haki za binadamu pamoja na kuongeza upatikanaji wa huduma bora za afya ya akili. 

Muongozo huo uliopewa jina “Afya ya akili, haki za binadamu na sheria: mwongozo na mazoezi” unaeleza kile kinachohitaji ili kuhakikisha jamii ina haki ya kupata huduma ya afya ya akili pamoja na kupitisha sheria za kuziwezesha taasisi za masuala ya afya ya akili kama taasisi nyingine ndani ya jamii kwa kuwapatia usaidizi wa mapato, usaidizi wa makazi na mitandao ya usaidizi wa rika.

“Afya ya akili ni sehemu muhimu kwenye haki ya afya,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, nakubainisha kuwa mwongozo huu mpya utasaidia nchi kufanya mabadiliko yanayohitajika ili kutoa huduma bora ya afya ya akili ambayo inamsaidia mtu “kupona na kuheshimu utu wake, kuwawezesha watu wenye hali ya afya ya akili na ulemavu wa kisaikolojia kuishi maisha kamili na yenye afya katika jumuiya zao.”

Msiwalazimishe mwenye matatizo ya afya ya akili

Taarifa hiyo ya pamoja imeeleza kuwa ulimwenguni kote kumekuwa na Matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu na kulazimishwa kutunzwa wale wanaogundulika kuwa na changamoto ya afya ya akili Matukio ambayo yanaungwa mkono na sheria na será zilizopo kwenye nchi hizo. 

Ofisi ya Haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa inaeleza kulazwa hospitalini bila hiari, kulazimishwa kuishi katika mazingira yasiyo safi na unyanyasaji wa kimwili, kisaikolojia na kihisia ni sifa ya huduma nyingi za afya ya akili duniani kote.

Kamishna Mkuu wa OHCHR Volker Türk, amesema matarajio ya kutoa muongozo huo ni nchi kubadili utoaji wa huduma za afya ya akili uwe wa kimaadili na sio tu kuhakikisha wanatoa huduma, bali huduma lazima ziwe na mwitikio wa kweli na hadhi. 

“Chapisho hili linatoa mwongozo wa jinsi mbinu inayotegemea haki inaweza kusaidia mabadiliko yanayohitajika katika mifumo ya afya ya akili” alisema Kamishna Türk.

Ingawa nchi nyingi zimejaribu kurekebisha sheria, sera na huduma zao tangu kupitishwa kwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu mwaka 2006, ni nchi chache mno zimepitisha au kurekebisha sheria na sera husika kwa kiwango kinachohitajika kukomesha unyanyasaji na kukuza haki za binadamu katika huduma ya afya ya akili.

Ingawa sehemu kubwa ya matumizi yaliyoripotiwa ya serikali kwa masuala ya afya ya akili yanaonekana hutengwa kwa hospitali za magonjwa ya akili (Asilimia 43 katika nchi zenye mapato ya juu), hata hivyo, ushahidi unaonesha kuwa huduma za kuwatunza katika jamii ndio zinazo patikana zaidi, hazina gharama na zina ufanisi tofauti na mifano ya kitaasisi ya huduma ya afya ya akili.