Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jinsi shirika la posta duniani linavyosongesha teknolojia ya kidijitali kwenye huduma za posta

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirikiano kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la Posta, (UPU) Bwana Mutua Muthusi.
UPU
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirikiano kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la Posta, (UPU) Bwana Mutua Muthusi.

Jinsi shirika la posta duniani linavyosongesha teknolojia ya kidijitali kwenye huduma za posta

Ukuaji wa Kiuchumi

Leo ni siku  ya posta duniani ambapo maudhui ni Pamoja kwa kuaminiana:Ushirikiano kwa mustakabali salama na uliounganika. Lengo la maudhui haya ni kuchagiza serikali na huduma zao za posta kusaidia maendeleo ya posta ya kidijitali ambayo itaboresha mtandao wa kale wa posta ulioendelezwa karne na karne, ukihitaji kwa kiasi kikubwa mtoa huduma na mhudumiwa kuonana uso kwa uso, jambo ambalo sasa kwa kiasi kikubwa limebadilika, huduma za posta mtandao zikichukua fursa. Shirika la Umoja wa Mataifa la Posta, UPU linataka ofisi za posta zichochee uchumi wa kidijitali.  

Katika kufahamu UPU inafanya nini kusongesha hilo Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirikiano kutoka shirika hilo, Mutua Muthusi anazungumza na Evarist Mapesa wa Idhaa hii na anaanza kwa kuelezea hali ya huduma ya posta hususan katika nchi zinazoendelea au maskini katika zama za sasa za maendeleo ya kidijitali. Mahojiano haya yamefanikishwa na Kayla Redstone wa UPU.

Hali ya huduma za posta katika zama za sasa za maendeleo ya kidijitali hasa katika nchi maskini iko vipi?

Kiwango cha huduma za posta kwa nchi zinazo endelea hasa Afrika, bado kiko chini sana na hata wakati huu wa mambo ya kidijitali bado iko chini, sababu wakati wa digitali kunahitaji kwanza mambo ya kuunganisha mtandao inayoweza kufanya kazi vizuri na watumiaji wa hizo  huduma wawe na vifaa vya kuunganisha mtandao.

Sasa kiwango cha mtandao kwa nchi zinazoendelea kiko chini, pia kiwango cha uboreshaji wa digitali pia kiko chini, kwa hivyo hii imeathiri sana mambo ya kuendeleza posta kwa njia ya kidigitali 

Sasa shirika la posta duniani linatumia vipi maendeleo haya ya kidigitali kuimarisha huduma za posta?

Mambo yote, huduma zote, biashara zote duniani kote zinatumia sana huduma ya mtandao, kwa hivyo posta nayo haijaachwa nyuma sababu kuna huduma kama e-commerce, hii ni biashara inayofanyika kwenye mitandao, wateja wanaweza ingia huko kwenye mtandao  kutafuta bidhaa ama huduma wanazohitaji na kuagina na kupata kwa hiyo njia, ndiyo posta iweze kuwapelekea bidhaa zile wamenunua 

Sasa katika mfumo huu wa mtandao, inapaswa posta pia iwe katika msingi wa mbele kujiendeleza, ndiyo iweze kuhudumia wateja wale ambao wanategemea njia hii, na wateja wanaotegemea njia ya mtandao ni wengi na wanazidi kukua hasa vijana na watu ambao wameendelea kwa njia nyingi, kwahiyo watu wengi wanatumia hii huduma na endapo posta itabaki nyuma kuunganisha mambo ya internet katika biashara zao watakuwa wamebaki nyuma maana yake kuna biashara nyingine nyingi ambazo ziko karibu zinafanya kama posta na zinaweza kuwa na huu muunganiko ya mtandao kwa njia ya kisasa.

Sasa itabidi kama posta hawawezi kuunganisha wateja wao kwa njia yay a mtandao, basi wale ambao wanashindana na wao kwa biashara watakuwa wanawapatia biashara ya juu zaidi kuwashinda, maana yake watu wengi sasa hawategemei sana hii biashara ya kawaida ya mfumo wa kale, watu wengi wanaingia kwenye mambo ya kimtandao maana yake yanaenda kwa haraka na nirahisi sana kuhudumiwa.

Na kwa nchi zinazoendelea, shirika hili la posta duniani linazisaidia vipi kunufaika na maendeleo ya teknolojia?

Kwa sababu ya maendeleo ya kimtandao kote ulimwenguni na kwa biashara zote UPU tupo na kitengo cha usaidizi wa kiufundi hapa kwa UPU ambacho kinaangazia sana kusaidia nchi zile zilizobaki nyuma kwa mbinu mbalimbali za kibiashara na kujiendeleza kwa posta, na moja wapo ni hii ya kidigitali na tunasaidia sana, tunatafuta wafadhili, tunapata hela, tunaweza kusaidia nchi ama mashirika ya posta ya nchi hizi zinazoendelea kwa kuwanunulia vyombo (vifaa), ambavyo vinaweza kuwasaidia kuunganisha hii na pia kuwasaidia kwa njia nyingi kama kuwaelimisha namna na jinsi ya kufanya biashara katika mfumo wa mtandao